HAPO
mwanzo, wakati Tanganyika inapata uhuru kulikuwapo na chama cha ukombozi wa
Waafrika wa Tanganyika (TANU) ambacho kiliweza kuwaunganisha wananchi! Baadaye,
TANU iliungana na ASP
kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa falsafa yake kiliamua kuandaa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977.
Katiba
ya 1977 iliipa CCM haki ya kipekee ya kushika hatamu za uongozi (kama
ilivyokuwa kwenye Ibara ya 10 ya Katiba ya JMT, 1977).
Katiba
ya 1965 na ya 1977, TANU kwa upande wa Tanganyika ilijipendelea na haikuruhusu
maoni ya wananchi isipokuwa ilichukua mamlaka wa watu na kuyafanya kuwa sehemu
ya itikadi ya chama kwa madai ya kuwashirikisha wakulima na wafanyakazi.
Kwa
upande wa Zanzibar,
baada ya mapinduzi ya Januari 11 na 12, 1964 vyama vyote vya siasa vilipigwa
marufuku na ASP iliendesha nchi kwa kutumia mawazo na maoni ya watu 14 (maarufu
kama, Baraza la Watu 14 au Baraza la Mapinduzi). Fikra za watu wawili (Nyerere
na Karume) zilitawala fikra za wananchi wote wa Tanzania!
Mwaka
1977, kama kawaida ya vyama vinavyopora uhuru, haki na usawa wa wananchi kwa
muundo wa chama kushika hatamu, CCM ilijipa haki za kipekee (exclusive rights)
za kutawala na kwa kutumia katiba iliyotungwa kukidhi utashi huo iliendelea
kufaidi haki za kipekee kwa muda mrefu hata sasa!
Japokuwa
CCM ilifanya ufisadi mkubwa kwenye mfumo wa serikali zake (ya muungano na ya
mapinduzi), jambo
kubwa lililowekwa na CCM kwenye Katiba ya 1977 ni nafasi ya kipekee ya kuongoza
mabadiliko!
Mkakati
wa kujipa mamlaka ya kipekee katika kufikia mujtamaa wa watu kwa uhuru, haki na
usawa ulikuwa ufisadi wa kutisha ambao CCM imeendelea kuutumia hata wakati huu
nchi inapotarajia kuandika Katiba Mpya!
Kazi
ya kuandika katiba ya wananchi ni kazi ngumu kama kuna mikingamo inayotokana na
ufisadi wa kimfumo na wa kimuundo uliyojengwa kwa miaka mingi na chama
kinachoongoza kwa propaganda,
hila, mizengwe, woga na ukiritimba wa kisiasa!
CCM
imejenga mazingira ya kutumia uongo wa kimasilahi na kuwafanya wanachama wake
waamini kila chama hicho kinachoamini na kukitetea! Tazama, wakati
lilipofanyiwa upitizi Azimio la Arusha,
mwenyekiti wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi alisema: Azimio la Arusha, kama
tunavyojua, limetangazwa mwaka 1967. Hii leo tuko katika mwaka 1991.
Imepita
miaka mingi, zaidi ya 20 tangu kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Na katika
kipindi cha miaka 20 yametokea mabadiliko mengi duniani na pia katika hali ya
maisha yetu (rejea hotuba ya Februari,25, 1992, Diamond Jubilee, Dar es Salaam).
Hotuba
ya mzee Ali Hassan Mwinyi, ililenga katika kuonesha mabadiliko yaliyotokea na
yanayohitaji mabadiliko katika kufanya upitizi wa marekebisho ya Azimio la
Arusha ili kwenda na wakati!
Inashangaza,
CCM iliona busara kubadilisha falsafa ya kuendesha Siasa ya Ujamaa na
Kujitegemea kwa kubadilisha baadhi ya miiko na maadili ya uongozi wa umma kwa
kuzingatia mabadiliko ya wakati. Huku ikisisitizwa kwamba, ‘kila zama na kitabu
chake.’





