MIGIRO, TIBAIJUKA,
NAGU WATAJWA
Dr. Asha-Rose Migiro |
HARAKATI
za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeingia katika hatua mpya baada
ya kuvuja kwa taarifa za kuwapo mkakati wa kuwapa nafasi wanasiasa wanawake na
kuwatosa wanaume kwa kile kinachodaiwa kuvunja makundi yenye uhasama.
Habari
za ndani ya makundi makuu ya wataka urais ndani ya CCM, zimethibitisha kuwapo
taharuki kubwa miongoni mwao baada ya taarifa za wanawake kupewa nafasi kubwa
kuzidi kushika kasi siku zinavyozidi kwenda.
Prof. Tibaijuka |
”Kuna
mpango wa kuwatosa wanaume kwa nia ya kuwapa fursa wanawake ndani ya CCM ili
baadae atakayepatikana, akishinda akasaidie kulinda maslahi ya wale wasio na
uadui wa kudumu, lakini wana maslahi ya kudumu (permanent interests),"
alieleza mtoa habari wetu.
Habari
zinaeleza kwamba, nguvu kubwa iliyotumika katika maeneo mbalimbali nchini
katika chaguzi za ndani ya CCM ni moja ya mikakati ya maandalizi ya mpango huo
wa kuwasimika wanawake.
Dr. Mary Nagu |
Wataka
urais wanaolengwa kuzimwa ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa,
Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wanawake
wanaotajwa kufanikisha mpango huu ni Dk. Mary Nagu, Prof. Anna Tibaijuka na Dk.
Asha Migiro ambao wote watasukumwa na makundi yenye fedha nyingi ili angalao
wawili kati yao waingie hatua ya mwisho.
”Ambao
wanatajwa kutaka kuingizwa hatua za mwisho ni Migiro na Tibaijuka ili wapate
nafasi ya kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM ambao kwa kiasi
kikubwa wameandaliwa kwenye chaguzi za CCM zinazoendelea kwa mikakati maalum na
kwa nguvu kubwa ya fedha,” kilisema chanzo chetu.
Uchaguzi
unaoendelea ndani ya CCM kwenye nafasi mbalimbali, una umuhimu wa peke yake
mwaka huu kutokana na ukweli kwamba ndio uchaguzi wa mwisho ambao utaonesha
sura halisi ya kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa
tiketi ya CCM mwaka 2015.
Tayari
makundi yameshajipanga kwa kuanza kufitiniana, kuwekeana mizengwe na mengi
yanayofanana na hayo ili mradi tu watu wao wapite kwenye chaguzi hizi za ndani
ya chama ili iwe rahisi kupata mtu wa kulinda maslahi yao au kujihakikishia
ulaji pindi mtu wao atakapopita.
Wakati
akitetea kiti cha uspika, Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, alikuwa mstari wa mbele katika kupinga ufisadi baada ya kutajwa ya
kuwa aliendesha kampeni ya kumng'oa aliyekuwa waziri mkuu kwa wakati huo,
Lowassa, kwa kulazimishwa na Bunge kujuzulu kutokana na kashfa ya kampuni tata
ya kufufua umeme ya Richmond.
”Hapa
Sitta alikuwa hana jinsi ila kusalimu amri, na yakafanyika yaliyokusudiwa na
wabaya wake wanaounga mkono ufisadi. “Hii
plan B inaweza kutumika kabisa kwenye uchaguzi ujao 2015 kutokana na mikakati
yenye hila inayohusisha fedha nyingi inayoendelea ndani ya CCM,” kilisema
chanzo chetu.
Kwa
kadri muda unavyokwenda, kumekuwa na ongezeko la malalamiko kwenye chaguzi za
CCM katika ngazi mbalimbali kutokana na nguvu kubwa ya fedha kutumika kama njia
ya kujipanga kwenye kupitisha jina la mgombea kwenye nafasi ya urais.
Mfumo
ulioko sasa hivi wa kuwatumia wajumbe wa halmashauri kuu za wilaya/mikoa
kuchagua wawakilishi wa kwenda kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mkutano
Mkuu wa Taifa umeonesha kuwa na dosari kubwa sana kutokana na rushwa kubwa ya
fedha inayotumika kuwapata wawakilishi hawa.
Watu
wenye malengo ya kugombea urais na wapambe wao wamekuwa wanatoa fedha nyingi
kwa watu wanaowataka kwenye mikoa na wilaya ili pindi watakapochaguliwa
wakawapigie kura ya kuwapitisha kwenye NEC na mkutano mkuu wa taifa.
"Kwa
kweli rushwa za namna hii ni hatari sana na zinaweza kutupatia viongozi wa
ajabu na wapenda rushwa kutokana na mbegu waliyoiotesha tokea kwenye msingi.
Demokrasia nzuri ni ile ya kupanua wigo ili pawe na matokeo mazuri na yenye
maslahi mapana zaidi," alisema mstaafu mmoja wa CCM.
Baadhi
ya wastaafu na wana CCM wanaochukia rushwa wanapendekeza kuwapo kwa baraza
rasmi la mwisho la kupitisha jina la mgombea wa urais hata kama amepitishwa na
vikao vya NEC na mkutano mkuu.
"Pengine
baraza hili liwe na marais wastaafu, makatibu wakuu wastaafu, watu wenye weledi
mbalimbali kwenye jamii, na pia mawaziri wakuu wastaafu ambao hawagombei kwenye
nafasi hiyo ili mradi tu apatikane mtu makini kwenye nafasi nyeti kama hii ya
urais," alisema mstaafu mmoja aliyenukuliwa.
No comments:
Post a Comment