To Chat with me click here

Tuesday, October 2, 2012

SUMAYE KUPASUA JIPU DAR

BAADA ya kushindwa katika nafasi ya kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupita Wilaya ya Hanang’, Mkoa wa Manyara, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema atazungumza na waandishi wa habari kueleza mchakato wa uchaguzi huo ulivyokuwa.

Sumaye alitoa taarifa hiyo jana kupitia ujumbe wa simu ya mkononi, baada ya kutakiwa na MTANZANIA, aeleze jinsi Mbunge wa Hanang’, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alivyomgaragaza katika uchaguzi huo uliofanyika juzi.

Kabla Sumaye hajasema kwamba atazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, awali mwandishi wetu alimwandikia ujumbe wa simu ya mkononi uliosema hivi.

“Mheshimiwa Sumaye, habari za mchana, mimi ni Mwandishi wa Gazeti la MTANZANIA, nimekupigia simu mara kadhaa lakini haikupokewa, shida yangu ni kutaka kujua hali halisi ilivyokuwa Hanang pamoja na msimamo wako baada ya Dk. Nagu kukushinda”.

Baada ya kuandikiwa ujumbe huo, Sumaye naye aliujibu baada ya muda mfupi akisema hivi. “Nimewaeleza waandishi wenzako wengi, kuwa nitawaita kwa pamoja mara nikirudi Dar es Salaam ndani ya siku tatu kuanzia leo,” alisema Sumaye kwa kifupi.

Kitendo cha Sumaye kupigwa mweleka katika uchaguzi wa kuwania nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kupitia Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara, kiliwashangaza wengi, kwa kuwa alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda.

Uchaguzi huo uliokuwa ukifuatiliwa na wengi kutokana na kuibua makundi na mivutano ya wapambe, ulihitimishwa kwa wapiga kura 1,150 kushiriki uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, Dk. Nagu aliibuka mshindi kwa kupata kura 648, huku Sumaye akiambulia kura 481. Kura 41 ziliharibika.

Hata hivyo, mgombea mwingine katika nafasi hiyo ya NEC kupitia Wilaya ya Hanang, Leons Marmo, aliamua kujitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa hiari yake.

Uchaguzi huo ulikuwa ukisimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo.

Baada ya Mbwiro kumtangaza Dk. Nagu kuwa ndiye mshindi, wafuasi wa Sumaye walijikuta wakiondoka eneo la tukio kwa hasira, wakionyesha kutoamini kilichotokea huku wakitishia kuihama CCM kwa madai kwamba, Dk. Nagu alitumia fedha nyingi kufanikisha ushindi huo.

Pamoja na wafuasi hao wa Sumaye kuonyesha kutoridhishwa na matokeo, pia Sumaye alipoona kuna kila dalili za yeye kugaragazwa, aliondoka ukumbini kimya kimya hata kabla ya matokeo kutangazwa.
Toa Maoni yako kwa habari hii

No comments:

Post a Comment