Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Ndg. Eliakimu Maswi |
Dar es Salaam. Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amemsimamisha kazi kwa muda, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma
kuhusu ushiriki wake katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Badala
yake, Sefue amemteua Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi
Mwihava kukaimu nafasi ya Maswi hadi uchunguzi husika utakapokamilika.
Maswi
(pichani), anakuwa kiongozi wa tatu kukumbwa na dhoruba inayotokana na sakata
la Escrow baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick
Werema na kung’olewa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka juzi.
Hatua
ya Balozi Sefue inafanana na ile iliyowahi kuchukuliwa na mtangulizi wake,
Philemon Luhanjo Julai 21, 2011 pale alipomsimamisha kazi kwa muda aliyekuwa
Katibu Mkuu katika wizara hiyo, David Jairo na kukaimisha nafasi yake kwa Maswi
ili kupisha uchunguzi.
Baadaye
Jairo alirejeshwa kazini lakini siku moja baadaye Rais Kikwete alimrejesha
nyumbani kutokana na shinikizo la wabunge na tangu hapo hakuwahi kurudi katika
utumishi wa umma na badala yake Maswi alithibitishwa kuwa katibu mkuu hadi
jana.
Hatua
ya kusimamishwa kwa Maswi imekuja siku moja tangu Rais Jakaya Kikwete
alipoelekeza mamlaka za utumishi kuchukua hatua dhidi ya Maswi baada ya kufanya
uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
“Kuhusu
katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma,
anatawaliwa na sheria na kanuni za utumishi wa umma, hivyo nimeshaelekeza
mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za
kinidhamu zitachukuliwa,” alisema Rais Kikwete wakati akilihutubia Taifa
kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam juzi.
Taarifa
iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, ilisema Balozi Sefue
amechukua hatua hiyo kwa kutumia madaraka aliyonayo kama mamlaka ya nidhamu kwa
watumishi wa umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwamo makatibu wakuu.
Amechukua
hatua hiyo kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Namba
8 ya 2002 (kama ilivyorekebishwa). Maswi
na watumishi wengine wa umma ambao wametajwa watashughulikiwa na Tume ya
Maadili, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) pamoja na Jeshi la
Polisi na ikithibitika kuwa walikiuka maadili yao ya kazi, sheria stahiki
zitachukuliwa.
Taratibu za uchunguzi
Kwa
mujibu wa taratibu, Maswi analazimika kwenda likizo kuanzia leo ili kupisha
uchunguzi wa awali ambao unalenga kubaini iwapo ametenda kosa la kinidhamu kwa
mujibu wa sheria zinazoongoza utumishi wa umma. Kwa kawaida likizo yake ni ya
malipo.
Ikiwa
uchunguzi wa awali utabaini kwamba ana makosa ya kinidhamu, atapewa taarifa za
tuhuma husika ambayo itaambatana na hati ya mashtaka, ambayo itaeleza kwa
kifupi makosa hayo na jinsi yalivyotendekea.
Matokeo
ya mchakato huo wa kinidhamu unaweza kuwa kushushwa cheo, kupunguzwa mshahara,
kufukuzwa kazi, kuachishwa kazi au kurejeshwa kazini kutegemea matokeo ya
taratibu zitakazofuatwa. Kwa
mujibu wa taratibu hizo, taarifa ya tuhuma itatoa maelezo kuhusu lini mtuhumiwa
anapaswa awe amezijibu.
Baada
ya kupelekewa atalazimika kujibu kwa kuzikubali au kuzikataa na ikiwa
atazikubali mamlaka ya nidhamu inaweza kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria na
kanuni za utumishi wa umma.
Kama
atakana au kukataa tuhuma husika, mamlaka ya nidhamu inapaswa kuunda kamati ya
uchunguzi ambayo itapewa muda maalumu wa uchunguzi wa kuwasilisha tarifa yake
kwa mamlaka ya nidhamu ikiwa ni mapedekezo na Katibu Mkuu Kiongozi anaweza
kutoa adhabu kwa kuzingatia mapendekezo hayo.
Mamlaka
ya nidhamu baada ya kupitia mapendekezo husika inawajibika kuendelea na
mchakato wa kutoa adhabu kwa mujibu wa Sheria ya Umma na kanuni zake na iwapo
adhabu ni kuvuliwa madaraka, mamlaka ya nidhamu italazimika kuwasiliana na
mamlaka ya uteuzi ambaye ni Rais.
Ikiwa
mtuhumiwa hataridhika na adhabu aliyopewa, taratibu zinampa fursa ya kukata
rufaa kwa Rais.
No comments:
Post a Comment