To Chat with me click here

Thursday, October 18, 2012

DR. ULIMBOKA AILIPUA IKULU

BAADA ya kuahidi kufichua siri ya kile kilichompata usiku wa Juni 26 mwaka huu, hatimaye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, amewataja wabaya wake, aliodai walihusika kumteka, kumtesa na kumuumiza vibaya.

Tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, lilitokea ikiwa ni siku chache baada ya mgomo wa madaktari kuanza nchini nzima na hivyo kuibua hisia kali kwa wananchi ambapo wengine walidai serikali ilihusika ikiwa ni hatua ya kuwanyamazisha wanataaluma hao, tuhuma ambazo hata hivyo zilikanushwa.

Baada ya kuokotwa akiwa ameumizwa vibaya katika msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Ulimboka alilazwa kwa muda katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (MOI) kisha akahamishiwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Tangu arejee nchini toka kwenye matibabu, mwenyekiti huyo amekuwa akiahidi kuanika ukweli wa kile kilichompata na hata baada ya kukaa kimya, baadhi ya watu walianza kumshutumu kuwa amewasaliti wenzake kwa kuzibwa mdomo.

Akizungumza jana kupitia kwa wakili wake Nyaronyo Kicheere, Dk. Ulimboka alifichua mambo mazito katika taarifa yake hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Taarifa kwa Watanzania na wapenda haki”.

Kicheere aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ameteuliwa na Dk. Ulimboka kusoma taarifa hiyo ambayo iliandaliwa Oktoba 7 mwaka huu na kushuhudiwa mbele ya wakili na Kamishna wa viapo, Rugemeleza Nshala.

Taarifa hiyo ilisomeka kuwa, “mimi Dk. Ulimboka Stephen, ambaye kila mmoja anafahamu matatizo yaliyonipata usiku wa Juni 26 mwaka huu, jijini Dar es Salaam; ninathibitisha maelezo yangu kuwa ni sahihi na kwamba nimeyatoa nikiwa na akili timamu.”

Ifuatayo ni taarifa yeke kamili
Leo ikiwa ni takribani miezi mitatu imepita, huku nikiwa najiandaa kuelekea nje ya nchi kwa matibabu zaidi, nimekaa na kutafakari kwa makini na kugundua kuwa nitakuwa sijawatendea haki Watanzania ambao waliniombea kwa sala, dua na wengine kufunga, iwapo nitaondoka nchini bila kueleza au kuthibitisha japo kwa uchache, baadhi ya yale yalioandikwa na vyombo vya habari, hasa gazeti lililofungiwa na serikali kwa kuripoti tukio la kutekwa kwangu la MwanaHalisi.

Kabla ya kutoa andishi hili, nimejiuliza pia mambo mengi; kwa mfano, ni jukumu la nani kuhakikisha haki inatendeka katika nchi yetu? Ni jukumu la vyombo vya habari ambavyo hutajwa kuwa ni mhimili wa nne wa dola? Je, ni jukumu la Bunge? Je, ni jukumu la serikali ambayo imepewa nguvu za dola na wananchi?

Je, ni jukumu la asasi zisizo za kiserikali (Civil Society) ambazo wengine huita mhimili wa tano? Au ni jukumu la mhusika mwenyewe kuelezea kinagaubaga kilichompata na kwamba ni yeye pekee anayepaswa kupigania upatikanaji wa haki yake? Binafsi sikupata jibu.

Kutokana na kushindwa huko kupata majibu, ndipo kwa ustawi wa taifa langu nimeamua kueleza yafuatayo:

Kwamba tukio la kutekwa kwangu, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno; na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande, Wilaya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, lilitokea wakati nikiwa na kikao na afisa aliyetambulishwa kwetu kuwa ni afisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid Ighondu.

Nathibitisha kwamba Ramadhani Ighondu alitambulishwa kwetu kwa jina la Abeid. Binafsi ninamfahamu sana bwana huyu kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile.

Nakumbuka kuwa Abeid alitambulishwa kwetu na kigogo mmoja, nikiwa pamoja na wawakilishi wengine wa madaktari kuwa yeye (Ramadhani Ighondu) ndiye atakayehusika katika kuchukua madai na hoja za madaktari katika mgogoro kati ya madaktari na serikali.

Nathibitisha kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu na kuniita kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye nilitekwa. Katika mawasiliano hayo, Abeid alikuwa anatumia simu Na. 0713 760473.

Kwamba hakuna mashaka kwamba namtambua Abeid kwa sura na namba aliyokuwa anatumia kuwasiliana nami mpaka siku ya kutekwa kwangu. Ni namba hiyo hiyo iliyoandikwa na gazeti tajwa hapo juu.

Katika mawasiliano hayo, mimi nilikuwa natumia simu 0713 731610 na kwamba mimi naamini kwa dhati kuwa afisa huyo wa Ikulu bado yuko hai na mimi na wenzangu tuko tayari kutoa ushirikiano kwa chombo huru kuhakikisha haki inatendeka.

Aidha, kwa nyakati tofauti Abeid alitumwa kwangu kukagua/kuchukua nyaraka zangu mbalimbali ikiwa pamoja na vyeti kwa ajili ya uthibitisho wa taaluma na masomo yangu.

Siku ya kwanza ya utambulisho akiwa pamoja na afisa mwenzake wa Ikulu, Ramadhani alichukua maelezo mafupi ya mtiririko wa mgogoro na akaendelea kufanya hivyo kwa nyakati tofauti.

Ninaendelea kuthibitisha kuwa maelezo niliyotoa ambayo yamerekodiwa kwenye mitandao mbalimbali pamoja na kwenye mtandao wa intaneti wa YouTube kuwa ni maelezo ya kweli.

Wakati natoa maelezo hayo nilikuwa nipo na kumbukumbu nzuri bila athari yoyote pamoja na maumivu makali ya mwili na kupungukiwa damu.

Uthibitisho wa kumbukumbu nzuri niliyokuwa nayo, ni pale nilipokutana na Juma Mganza katika msitu wa Mabwepande asubuhi ya siku ya tukio. Pamoja na maumivu makali niliyokuwa nayo kutoka kila sehemu ya mwili wangu, niliweza kumshawishi Mganza kunifungua kamba za mikono nilizokuwa nimefungwa.

Na pia kukumbuka namba ya simu ya rafiki yangu Dk. Deogratias ambapo Mganza aliweza kuitumia kuwasiliana naye kumpa taarifa juu ya tukio hilo. Ni kupitia taarifa hiyo, ndipo suala la mimi kufikishwa hospitali ya mifupa MOI lilipofanikiwa.

Najua wapo watu ambao wamekuwa wakihaha kupindisha ukweli. Lakini wanaotaka kupindisha ukweli wanasahau kuwa, kama niliweza kushawishi Juma Mganza hadi akashawishika kunikaribia na kunisikiliza pamoja na hofu aliyokuwa nayo ya kukutana na mtu aliyekuwa kwenye hali kama yangu.

Na kama niliweza pia kukumbuka namba ya rafiki yangu, mambo hayo yanatosha kuthibitisha kuwa nilichokisema ni ukweli na kuwa utimamu na kumbukumbu zangu ni sahihi.

Hivyo basi, nathibitisha kuwa maelezo yote niliyotoa na kurekodiwa kabla sijafika na kwamba Watanzania wawapuuze wale wote wanaotaka kupotosha ukweli juu ya jambo hili.

Ninaendelea kuthibitisha kuwa Abeid ninamfahamu na hata akikamatwa leo hii, nitakwenda kufanya utambuzi. Inasikitisha kukumbusha kuwa hatujasikia popote kuwa Abeid pamoja na washiriki wake wamehojiwa pamoja na jamaa wengine waliotajwa mpaka sasa.

Ninafahamu kuwa ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa kinga kwa uhai wa kila mtu anayeishi katika nchi yetu. Tena inaitaka jamii kulinda uhai wa kila mtu.

Mimi Ulimboka Stephen ni raia wa Tanzania ambaye ninafahamu kuwa nina haki ya kuishi na kuwa serikali yangu na wananchi wenzangu wana jukumu la kuulinda uhai wangu.

Kilicho na kinachonisikitisha sana ni kuona jinsi serikali ya nchi yangu ilivyopuuza kuhatarishwa kwa uhai wangu na kutoa kauli za rejareja juu ya unyama huo. Wale wote waliotuhumiwa na ninaowatuhumu kunitendea unyama huu wako huru na hakuna aliyewagusa.

Je, uhai na maisha yangu yana thamani ndogo kama ya mnyama anayekwenda machinjioni? Je, serikali ya nchi yangu itakubali lini kuundwa kwa tume huru kuchunguza unyama huu na kuhakikisha kuwa haki inatendeka?

Je, kuna watu ambao katika nchi yetu ambao wana haki ya kutenda unyama kwa kuwa wao wako juu ya sheria? Hiyo siyo Tanzania ninayoifahamu au ambayo Watanzania wenzangu wanaipenda na kuwa tayari kuifia.

Ninapenda kusema kuwa mimi niko tayari kuhojiwa na kutoa ushirikiano wangu kwa vyombo huru na makini vya uchunguzi ambavyo vitaundwa ili kuweza kuubaini ukweli.

Kwa madaktari wenzangu ninapenda kusema kuwa niko pamoja nao na kuwa madai yetu ni ya haki na ya msingi. Nitaendelea kuwa nao katika kupigania masilahi yetu na kuwa tusikubali kugawanywa na watu wasiotutakia mema na wanaoishi kwa vitisho na si hoja.

Sisi kama madaktari tunastahili kufanya kazi katika mazingira mazuri na kupata ujira wa haki kutokana na kazi na huduma yetu tukufu.

Namaliza kwa kusema wapo watu ambao hawatapenda kusikia siri iliyojificha katika tukio lile. Lakini nimetafakari sana, nimeona hakuna njia nyingine iliyonyooka zaidi ya kueleza ukweli na kama ilivyoandikwa katika vitabu vitakatifu “ukweli utawaweka huru”.

No comments:

Post a Comment