Japokuwa nchi yetu ya Tanzania inaongozwa na Rais na Makamu wa Rais
walio waislamu na ina Katiba ambayo siyo ya kidini bado kuna madai kuwa tupo
chini ya 'Mfumo Kristo'. Ukiichambua kwa mapana dhana ya 'Mfumo Kristo' utaona
inamaanisha 'Mfumo wa Kimagharibi' kwa kuwa kwa kiasi kikubwa taasisi, elimu,
taratibu na sheria zetu zinatokana na 'Ustaarabu wa Kimagharibi' (Western
Civilization) ambao unasemekana ni zao la 'Ustaarabu wa Kikristo' (Christian
Civilization) ulioletwa 'kwanza' kwetu na wamishionari na wakoloni waliotoka
katika 'nchi za kikristo na kimagharibi'. Ndio maana kama hivyo ndivyo watoa
madai wanavyoamini basi kushambulia watu au/na vitu ambavyo hatuoni uhusiano wa
moja kwa moja na madai yao mengine, ni sehemu ya kupambana na huo wauitao 'Mfumo
Kristo'.
Hoja hii haipingani na hoja jadidi ya Mwanasosholojia wa Dini kuwa nchi
yetu iko katika ombwe la dira na matatizo ya ajira na ujira hasa kwa vijana
hivyo kufanya iwe kazi rahisi kuwafanya waone tatizo ni huo 'Mfumo Kristo'
ambao wanauona ndio, kihistoria, umewanyima elimu na ajira. Kwa mfano, mjomba
wangu ambaye ni muislamu anadai kuwa tunakosea tunapomsifu Mwalimu Nyerere kwa
kuchukua shule za wamishonari/makanisa na hivyo eti kuwasaidia waislamu wasome.
Kwa mujibu wa tafsiri yake ya historia ya Tanzania, moja ya sababu ya
waislamu kuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru ni ili waweze kujenga
shule zao wenyewe zitakazotoa elimu bila kulazimika kufuata misingi ya wakoloni
na wamishionari ambao walikuwa ni wakristo. Hivyo kwa tafsiri yake, Nyerere
alichofanya baada ya uhuru ni kuwazuia waislamu wasiweze kujenga shule zao na
hivyo kuwafanya, kwa ujumla, waendelee kuwa nyuma kuliko wakristo. Inawezekana
kabisa kuna ukweli katika hilo.
Ni vigumu kuelewa hoja hizo bila kuvua lensi za Kikristo na kuutafiti
kwa kina ukweli wake. Tunapaswa kuelewa watoa madai wanamaanisha nini hasa
wanaposema kuwa tatizo ni 'Mfumo Kristo' kujikita katika nyanja ya maisha na
taasisi zetu. Inabidi tuwaelewe na tujielewe kwa undani kwanza. Na kama
alivyosema mpagani fulani, kudhani kutofikiria dini ni kutokuwa na udini ni
sawa sawa tu na kudhani kutofikiria rangi (color blindness) ni kutokuwa na
ubaguzi wa rangi.
No comments:
Post a Comment