VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Wilaya ya Mbeya
Mjini juzi waliingia katika malumbano ya kung`ang`ania msiba baada ya kila
chama kudai msiba huo unakihusu.
Katika msiba huo ulikuwa
wa mama mmoja aliyefahamika kuwa ni RoseMary Mbwete wa eneo la
Mwanjelwa, jijini Mbeya.Katika tukio hilo viongozi na wanachama wa vyama hivyo
walitoa magari kwa ajili ya matangazo na muziki.
Chadema ndiyo walikuwa wa kwanza
kuwasili na gari lao mapema saa 3:00 asubuhi na kutaka kuhodhi msiba
huo.Mvutano huo ulikuja baada ya Chadema kuwazuia viongozi wa CCM waliotaka
kulitumia gari lililotolewa na chama hicho kwa ajili ya shughuli za matangazo.
Kitendo hicho kiliwalazimisha
CCM kwenda kuleta gari la kwao na kusababisha eneo hilo kuwa na
magari mawili ya matangazo.
Hali hiyo ilisababisha kutokuwapo kwa
maelewano kwa kuwa magari yote yalikuwa yanatumika kupiga muziki na
matangazo kwa wakati mmoja.
Hali hiyo ilimlazimisha Mtendaji wa
Kata ya Ruanda, Elizabeth Kalinga kuingilia kati na kwamba hayuko tayari
kuona amani inavunjika katika eneo hilo.
Alikitaka kila chama kufuata
taratibu, hatua iliyosaidia kurejesha amani na utulivu.Akizungumzia tukio hilo,
Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija alisema wao
walikwenda msibani na kuweka bendera ya Chadema kwa ajili ya kumfariji mwenzao
aliyefiwa na dada yake.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, marehemu
alikuwa kada wa CCM."Unajua sisi Chadema tupo karibu na jamii na
michango tunayotoa ni mikubwa hali inayowatisha CCM ndiyo maana waliamua
kutufanyia vurugu," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja
wa Wanawake CCM wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Shija Mwakatundu alisema
kitendo cha Chadema kwenda kwenye msiba wa CCM na kuweka bendera zao
kinaashiria vurugu na uchonganishi.
No comments:
Post a Comment