Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinasikitishwa sana na mauaji yanayoendelea
kufanywa na vyombo vya dola hususan vyombo vya ulinzi na usalama bila hatua za
kisheria kuchukuliwa kwa watuhumiwa wa ukiukwaji huo wa haki ya kuishi.
Tangu
mwaka 2001 hadi sasa, LHRC tumekuwa tukifuatilia matukio mbalimbali ya kuuawa
kwa raia yanayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama. Hivi karibuni, mnamo
tarehe 2 Septemba, 2012 tulishuhudia mauaji ya kinyama kule Iringa yaliyofanywa
na polisi kwa kutumia kile tunachosadiki kuwa ni ‘bomu la machozi’ kwa kumuua
mwandishi wa habari ndugu Daudi Mwangosi.
Leo
hii, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetoa taarifa baada ya uchunguzi na
kufuatilia mwenendo wa matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu,
hususan ukiukwaji wa haki ya kuishi (waathirika wakiwa mikononi mwa vyombo vya
dola).
Taarifa
rasmi imeambatanishwa. Kwa mfano kwa mwaka huu tu hadi mwishoni mwa mwezi wa
tisa takwimu za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu zinaonyesha kuwa tayari
watu 24 walikwisha uawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama. Baadhi ya
sababu ni kushindwa kuhimili siasa za vyama vingi na ukosekanaji wa uvumilivu
wa kisiasa.
Pia,
kushindwa kuwa na mipango shirikishi ya kiusalama katika maeneo ya uwekezaji
hususan kwenye migodi na kwenye hifadhi za taifa. Baada ya kutafakari na
kuangalia uwajibikaji wa viongozi wa nchi hii, Kituo kimechukua hatua
zifuatazo, baina ya nyingine: ·
Kupeleka
malalamiko kwa Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya mauaji ya
raia yanayofanywa na vyombo vya dola (UN-Special Rapporteur on etra-judicial
killings). Kumtaka mjumbe huyu kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa
serikali ya Tanzania. Taarifa ilipelekwa tarehe 28 Septemba 2012. Na tayari
ameshaanza kupitia malalamiko ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu; ·
Kupeleka
malalamiko kwa Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa (ICC Prosecutor) na
kumtaka kufanya uchunguzi na kuona hatua anazoweza kuchukua, Tarehe 28
September 2012; · Kupeleka suala hili kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu
na Haki za Watu katika kikao chake cha mwezi wa Oktoba 2012, kule Ivory Coast
na kuitaka Tume kuchunguza na kuchukua hatua ikiwemo kulipeleka suala hili
Mahakama ya Afrika; ·
Taarifa
hii pia imepelekwa kwa wadau wengine mbalimbali wa haki za binadamu kama
Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH) na Ofisi za umoja wa mataifa
Tanzania kwa hatua mbalimbali.
Nchi
hii inaheshimu utawala wa sheria na katiba. Katika haki zilizoainishwa kwenye
katiba ibara ya 18 ni haki ya kutoa maoni na uhuru wa mtu kushirikiana na
wengine ibara ya 20. Matumizi ya mikutano ya hadhara na maandamano yenye
kufuata taratibu za kisheria ni njia mojawapo ya demokrasia.
Hivyo ipo
haja kwa serikali kutoa taarifa na habari kwa umma kuhusu juhudi
zinazochukuliwa na serikali katika kuwalinda wao na mali zao, kuwaletea
maendeleo na kupunguza ugumu wa maisha.
No comments:
Post a Comment