AMTUMIA MWANDOSYA
KUJISAFISHA
Rais Kikwete |
HATUA
ya Rais Jakaya Kikwete kueleza mshangao wake kuhusu vitendo vya rushwa kupenya
katika chaguzi zinazohusisha wanawake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
imepokewa kwa hisia tofauti na makada wa chama hicho na wadadisi wa masuala ya
siasa.
Kikubwa
kinachoonekana kuwashtua wafuatiliaji wa siasa ndani ya CCM ni hatua ya Rais
Kikwete kutoa kauli ya mshangao pasipo kuonekana akichukua hatua zozote za
kukabiliana na vitendo vya rushwa ambavyo yeye mwenyewe anakiri kwamba
vinahatarisha uhai wa chama hicho.
Mmoja
wa makada wa muda mrefu serikalini na ofisa wa juu mstaafu wa moja ya taasisi
nyeti za dola, amelieleza kwamba, kauli ya Kikwete imeonyesha namna kiongozi
huyo anavyojitanabahisha kwa namna tofauti na ilivyopata kufanywa na
watangulizi wake watatu.
Ofisa
huyo ambaye kama walivyo wengine wanne waliozungumza na waandishi wa gazeti
hili kwa masharti ya kutotajwa kwa majina yao, alisema Rais Kikwete ambaye
ndiye mwenyekiti wa taifa wa CCM alipaswa kutoa kauli ya kukemea, karipio na
yenye mamlaka dhidi ya wagombea wanaotoa rushwa katika chaguzi zinazoendelea
ndani ya chama hicho.
Kwa
mujibu wa ofisa mwingine mstaafu, kitendo cha rais kutoa kauli zinazobadilika
badilika kuhusu rushwa huku akiwa na mamlaka ya kuwachukulia hatua watuhumiwa
wa vitendo hivyo hususan ndani ya serikali na katika vikao vya chama
anavyoviongoza, ni dalili za woga wa kuchukua maamuzi sahihi.
“Rais wangu ni
mtu wa kushangaza na mwoga. Amepata kusema anawafahamu wala rushwa kwa majina.
Ni huyu huyu aliyewahi kutamka kuwa siku za wala rushwa zinahesabiwa na leo
anasema eti anashangaa kusikia hata wanawake wanajihusisha na rushwa katika
uchaguzi,” alisema kada mwingine mwandamizi ndani ya CCM.
Tangu
kuanza kwa uchaguzi huo wa chama hicho ngazi ya shina hadi taifa, kumekuwa na
malalamiko kila kona ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa, huku watuhumiwa hao
wakipitishwa na vikao vya juu na kuibuka na ushindi.
Tayari
baadhi ya vigogo walioanguka katika uchaguzi wa ndani ya CCM katika ngazi
tofauti, wamekuwa wakizungumza chini kwa chini kwamba kuongezeka kwa kasi ya
vitendo vya rushwa ndani ya chama imetokana na udhaifu wa Rais Kikwete
kushindwa kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo.
Akihutubia
Mkutano Mkuu wa Nane wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) wa CCM juzi, Rais Kikwete
aliishia kuonya juu ya vitendo vya rushwa vinavyozidi kushamiri ndani ya chama
hicho, akisema kuwa visipochukuliwa hatua mapema, kuna hatari ya kukifikisha
chama katika hatua mbaya.
Hakuishia
hapo, alikwenda mbele zaidi na kusema, imekuwa ni hulka sasa hasa baada ya
kumalizika chaguzi kwa wanachama kuendeleza na kuwekeana uhasama kama
uliokuwepo wakati wa kampeni na wengine kuwaadhibu ambao hawakuwachagua hali
ambayo ni mbaya sana kwa mustakabali wa chama.
Rais
Kikwete aliwaasa wagombea wa nafasi mbalimbali wa UWT walioshindwa kutoweka
visasi na walioshinda kutowapiga vijembe walioshindwa kwani kazi iliyo mbele ni
kubwa kutokana na CCM hivi sasa kukabiliwa na hali ngumu ya ushindani wa
kisiasa.
“Kweli
tusipokemea vitendo hivi na kuviacha vikiendelea, tutakipeleka chama mahali
pabaya, ninasikitika sana kusikia hata wanawake sasa wanajihusisha na utoaji
rushwa ili kununua nafasi za uongozi kitu ambacho ni hatari sana,” alisema
Kikwete.
Alifafanua
kuwa chama kinapoelekea si kuzuri ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko. Katika
hatua nyingine, Rais Kikwete ameonyesha kutishwa na nguvu na kasi kubwa ya
vyama vya upinzani.
Alisema
wakati CCM ikichafuka kwa rushwa, vyama vya upinzani vimekuwa vikijiimarisha
kisiasa hali ambayo inakifanya chama chao kiwe katika wakati mgumu.
Kutokana
na hali hiyo, Rais Kikwete alizihimiza jumuiya za chama hicho kuongeza juhudi
na kujipanga kupambana na hali hiyo kwa lengo la kuiwezesha CCM kushinda
uchaguzi wa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment