To Chat with me click here

Friday, October 5, 2012

MNYIKA AMVAA WAZIRI WA NISHATI

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini Mhe. John Mnyika
WAZIRI kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, kufuta taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.

Taarifa hiyo ilikuwa ikieleza lengo la agizo la kupitiwa kwa mikataba 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ili kuhakikisha mapungufu hayajirudii katika mikataba mipya ya baadaye kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za Taifa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo alisema kuwa ufafanuzi uliotolewa na Maswi unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati kuna madai waliyotoa mwaka 2011 wakidai baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi.

Aidha Mnyika alisema kuwa mwaka huu pia zimeibuka tuhuma za vigogo wa Serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti zao zilizopo nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi asili.

“Tafsiri ya ufafanuzi huo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni kwamba hata kama mikataba iliyopo ina upungufu usiozingatia maslahi ya taifa, matokeo ya mapitio hayo hayatarekebisha mikataba iliyopo bali mikataba ya baadaye,” alisema Mnyika.

Pia alisema kuwa taarifa ya Maswi ni ya kurudi nyuma tofauti na kauli za awali za Waziri Muhongo zilizokubaliana na madai ya kutaka mikataba yote ipitiwe upya, isiyozingatia maslahi ya Taifa ivunjwe au ifanyiwe marekebisho na mikataba mipya isiingiwe mpaka sera na sheria bora zenye kulinda uchumi na usalama wa nchi zitakapokuwepo.

Pia aliwataka kuzingatia kuwa, matatizo katika sekta za nishati na madini yanachangiwa na kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa serikali hali inayosababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.

No comments:

Post a Comment