To Chat with me click here

Tuesday, October 16, 2012

MANUMBA: POLISI LIPIZENI KISASI

ASEMA WALIOMUUA KAMANDA BARLOW LAZIMA WAKAMATWE, KUAGWA DAR LEO

Askari wakiwa wamebeba mwili wa marehemu ACP Barlow
MKURUGENZI wa Upelelezi wa  Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba amewataka Polisi kuhakikisha wanalipa kisasi dhidi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (53).

Akitoa salamu za polisi, wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Marehemu Barlow, DCI Manumba alisema polisi wamefundishwa kuwa watulivu wakati wa hatari, lakini kwa kifo cha kamanda huyo “wanatakiwa kulipiza kisasi” kwa kuwakamata waliohusika.

 “Wakati wa hatari, askari tunafundishwa kutulia, ninawashukuru askari mlitulia, lakini katika hili ninawataka kuhakikisha mnalipa kisasi kwa waliohusika, kwa kuwakamata wote walioshiriki mauaji haya,” alisema Manumba.

Mwili kwa Kamanda Barlow aliyeuawa na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba 13, mwaka huu, uliagwa na maelfu ya wakazi wa Mwanza wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi katika ibada iliyofanyika katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo na viongozi mbalimbali, wakiwamo makamanda wa polisi wa mikoa ya Tabora, Shinyanga, Geita, Mara, Kagera na Simiyu.DCI Manumba alisema ulipizaji huo wa kisasi lazima ulenge kuwakamata washiriki wa matukio mengine ya mauaji kama yale ya albino pamoja na wazee vikongwe kwa sababu za imani za kishirikina.

Kuhusu upelelezi wa tukio hilo, Manumba alisema ushirikiano walioupata kutoka kwa wananchi umefanikisha kazi hiyo kufikia hatua nzuri kwani tayari wamewabaini baadhi ya watuhumiwa.“Taarifa mlizotupa zimetusaidia na muda si mrefu tutakuwa tumemaliza kazi na wale wote waliotusaidia watakuwa wadau wetu,” alisema DCI Manumba na kuongeza:

“Tabia mbovu za kutekeleza mauaji kwa kujichukulia hatua mikononi, yakiwamo yale ya vikongwe na albino bila ya kujali uwepo wa Mahakama ni changamoto, Watanzania wanatakiwa kutafakari wapi wanalipeleka taifa hili.”

Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na uhalifu wa namna hiyo kwa sababu wahalifu hawana dini wala kabila na kuwataka wananchi kuimarisha ulinzi shirikishi kutokana na uchache wa askari katika jeshi hilo.

Ibada ya kuaga
Ibada ya kuaga mwili wa kamanda huyo iliongozwa na Padri Raymond Manyanga wa Parokia ya Nyakahoja.
Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri Lukuvi aliwataka wananchi wa Mwanza kuwa na imani na Serikali yao akisema ipo kwa ajili ya kuwalinda pamoja na mali zao.

Lukuvi alisema kuuawa kwa Barlow hakuwezi kusababisha kuvurugika kwa amani katika mkoa huo kwa kuwa Serikali ipo makini kulinda usalama wa nchi.

Katika salamu zake za Mkoa wa Mwanza, Ndikilo alisema katika kipindi hiki, polisi hawataweka silaha chini na watasonga mbele mpaka hapo ushindi wa kuwakamata wauaji utakapopatikana.Alisema vyombo vya usalama vimepanga kuhakikisha vinawawajibisha wahusika wa mauaji hayo ambayo aliyaita ya kinyama.

Alisema mkoa umepata pigo kwa kuwa Kamanda Barlow alikuwa mtu mwenye ushirikiano akimsifia kwa ushirikiano wake wa kuhakikisha Mkoa wa Mwanza unakuwa salama.

“Tangu Kamanda Barlow alipoteuliwa kuja katika mkoa huu, amefanya kazi nzuri ya kuhakikisha usalama wa Wana - Mwanza pamoja na mali zao na kukomesha mauaji ya albino, vikongwe pamoja na ujambazi wa majini na barabarani,” alisema Ndikilo.

Padri Manyanga alimwombea msamaha marehemu kwa wale wote ambao aliwakosea na kuwataka wamwombee ili apumzike kwa amani.

Alisema hategemei katika kazi aliyokuwa akifanya marehemu asiwe na maadui kwa sababu yeye ni binadamu kama walivyo wengine... “Marehemu alijitahidi kuwatumikia Watanzania kwa kuhakikisha kuwa haki inatendeka. Kama alikuwa na upungufu, basi alikuwa kama watu wengine ila kwa uwezo wake Mungu alimjalia kufanya kazi yake. Maisha ya mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mungu, hakuna mtu ambaye ana haki ya kutoa uhai wa mtu yeyote.”

Salaam za Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linachukua hatua za lazima kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria watu wote wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji ya Kamanda Barlow.Katika salamu za rambirambi alizompelekea Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, Rais Kikwete amesema ameshtushwa na kuhuzunishwa na mauaji hayo.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ACP Barlow kilichotokea usiku wa Ijumaa katika jiji la Mwanza ambako watu wasiojulikana walimpiga risasi na kumuua ofisa huyo mwandamizi wa Jeshi letu la Polisi,” alisema na kuongeza:

“Historia ya ACP Barlow ni ya mfano katika utumishi wa umma na hususan katika Jeshi la Polisi. Kwa hakika, Jeshi la Polisi limempoteza kamanda hodari na wananchi wa Tanzania, hususan wale wa Mkoa wa Mwanza, wamempoteza mlinzi shupavu wa usalama wao na mali zao.”

Mwili wa Barlow uliwasili Dar es Salaam jana na leo utaagwa nyumbani kwake Ukonga kuanzia saa 6:00 mchana kabla ya kupelekwa katika Kanisa Katoliki Majumba Sita kwa ajili ya misa na watu mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho.

Wasifu wa Barlow
Marehemu Barlow alizaliwa Desemba 26, 1959 mkoani Kilimanjaro na kusoma katika Shule ya Msingi Lombeta Moshi Vijijini na kuhitimu mwaka 1974.Mwaka 1979 alimaliza elimu ya sekondari katika Shule ya Seminari Maua na mwaka 1981 alijiunga na Shule ya Sekondari Mirambo, Tabora katika mchepuo wa Lugha.

Mwaka 1982 aliajiriwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Iringa na mwaka huohuo alijiunga na Chuo cha Polisi Moshi kusoma sheria ya uhamiaji. Baada ya kuhitimu, mwaka 1984 aliajiriwa katika Idara ya Uhamiaji na kupelekwa katika ofisi zake za Mkoa wa Mtwara.

1984 alitunukiwa shahada ya kwanza ya utawala mafunzo,  Chuo cha Polisi Dar es Salaam na baadaye kupata mafunzo ya ukaguzi mnamo mwaka 1987.
Mwaka huohuo wa 1987 alihamishiwa Polisi na kuanza kazi katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi.

Katika uhai wake, aliwahi kufanya kazi katika Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Kigoma kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi na kufanya kazi ya kuongoza jeshi hilo katika mikoa ya Mara na Tabora kabla ya kuhamishiwa Mwanza.

No comments:

Post a Comment