Rais
Jakaya Kikwete ameonya kwamba vitendo vya rushwa vinavyojitokeza katika chaguzi
za ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) visipodhibitiwa vitakitumbukiza
chama hicho kwenye shimo.
Rais Kikwete alitoa angalizo hilo ikiwa ni siku moja tu, baada ya Mkutano Mkuu
wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) kumchagua Sophia Simba kuwa Mwenyekiti
wake katika uchaguzi unaodaiwa kugubikwa na rushwa, vijembe na tambo.
Kikwete, amesema suala la kuuza na kununua kura lisiposhughulikiwa
litakitumbukiza chama kwenye shimo. Kikwete aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu Maalum wa
uchaguzi wa UWT uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Chuo cha
Mipango mjini hapa.
Rais Kikwete alisema kuwa wakati huu kuna mambo mengi ambayo baadhi yake
yanasikitisha na kwamba hata kuyasema yanatia aibu.
“Kuna mambo mengi, mengine yanasikitisha hata kuyasema ni aibu, na wakati wote
naendelea kukumbusha. Ndugu zangu haya tukiendelea nayo sura tunayoijenga kwa
wananchi ya chama chetu… tunaona sisi tunapata, lakini athari yake kwa wananchi
na ndani ya chama ni mbaya sana, tena sana, sina namna ya kutafuta maneno
mazuri ya kulieleza hilo ya kununua na kuuza kura ,” alisema Rais Kikwete
ambaye alionyesha kukerwa sana na jambo hilo na kuongeza:
“Nimeyasema haya ni lazima tufike mahali tutambue kuwa haya si mazuri na
yanapohusisha mpaka wanawake, maana zamani nilidhani haya mambo ni ya wanaume
tu, lakini sasa hadi wanawake ndio tena tumekwisha. Tunakoelekea sio kuzuri
sana na kama hatutafanya jitihada ya makusudi kubadiliks, tupo hapa mtakuja
kunieleza jinsi mtakavyoelekea kwenye shimo.”
Alisema kazi ya timu iliyochaguliwa katika uchaguzi huo ni kuziba nyufa za
mgawanyiko wa uchaguzi.
“Maana kuna watu wengine wanaondoka na mfundo, sina neno la kulielezea, lakini
anaondoka na kitu amekifunga, ana hasira ndio mfundo. Ukomavu na ustahimilivu
ni jambo linalohitajika sana,” alisema na kuongeza:
“Jambo hili lazima mtambue kuwa kugombea ni haki ya kila mwanachama, hakuna
ambaye ana haki zaidi ya mwenzake, maadam ulikuwa kiongozi miaka mitano haki
yako inaishia siku ile muda wako unapoisha baada ya hapo kila mwanachama anayo
haki ya kugombea nafasi ya uongozi uliyokuwa unashikilia.”
Rais Kikwete alisema pia mwanachama anayo haki ya kumuunga mkono mtu yoyote
ambaye anaona anafaa na kwamba kuna watu wanaweza kuchukiana kwa sababu ya
mwanachama kugombea nafasi aliyokuwa anashikilia.
“Kwa nini kagombea nafasi yangu? Yako kivipi? Katiba inasema utakuwa kiongozi
kwa muda wa miaka mitano, imeisha! Sasa unaomba upya, huyu Sophia ni Mwenyekiti
mpya alikuwepo huwezi kumchukia mwanachama anayegombea nafasi unayoiita yako si
yako,” alisema na kushangiliwa.
Alisema nafasi hiyo ni haki ya kila mwanachama na kuwataka kutowachukia wale
ambao hawakuwaunga mkono katika uchaguzi na badala yake kuwaunga wagombea
wengine.
“Mkiendekeza hilo hakutakuwa na demokrasia katika chama chetu, ukitoka hapo
kwanini aligombea nafasi yangu, mkitoka hapa mnanuniana kwanini yule alimuunga
mkono fulani, kama walikuwa wanataka wote wakuunge mkono wewe wasingewaruhusu
wengine waje,” alisema na kushangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.
Rais Kikwete alisema kumchukia ama kumnunia mtu ambaye ameamu kutumia haki yake
ya kidemokrasia katika uchaguzi ni kuonyesha kiwango cha juu cha udhaifu.
Alisema pia kiongozi wa namna hiyo atakuwa hatoshi, hajiamini na
ataendesha chama kimakundi.
“Hawa wangu, hawa si wangu, hakuna mtu wa mtu binafsi hawa wote ni wa chama,
lazima wote wapewe fursa ya kutumikia jumuiya yao kwa uwezo wao, sifa yao
isiwe hakuniunga mkono ama ameniunga mkono mtaiua jumuiya hii,” alisema.
NAFASI ZA UONGOZI
Alitolea mfano wa siku moja alipokuwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa
(Nec) kuwa wakati mwingine vineno vya kipuuuzi vilitoka. “Nikawaambia jamani baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, mwaka 2005, nimeunda
serikali akiwemo Mwandosya (Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri asiyekuwa
na Wizara Maalum).
Profesa Mwandosya alikuwa miongoni mwa makada 11 waliomba kuwania urais ndani
ya chama hicho katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005.
“Nimeunda serikali ambayo ina mawaziri ambao walikuwa wanawaunga mkono wagombea
wenzangu katika uchaguzi huo, na wengine walikuwa wananifanyia mambo ya ovyo
kweli, lakini yameshapita, sasa tuko katika hatua ya kujenga nchi yetu, nchi
haijengwi na marafiki zangu tu,” alisema.
“Hiyo nchi mnaweza kuifikisha hata shimoni kwa sababu ya urafiki, nina
mchanganyiko mle ndani, utakuta mle ndani kila mmoja katika wagombea wale 11
kila mmoja alikuwa na mtu wake,” aliongeza.
Alisema baada ya kuweka watu mchanganyiko katika serikali yake, alijenga
utulivu ndani ya chama, ingawa baadaye aligundua kuwa wanaogombana ni rafiki
zake.
“Wanagombana wao wananipa kazi kubwa, jamani tunagombea nini mbona katika
uchaguzi huo tulikuwa pamoja?” alihoji.
Alisema amelisisitiza hilo ili Simba na wenzake waepuke kulitenda na pia
akilifanya wanachama wa umoja huo wasiseme atakapowachagua waliompinga katika
uchaguzi huo.
Aliwataka kukusanya nguvu ili kuiwezesha jumuiya hiyo kujenga nguvu kwa ajili
ya ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015.
Aliwataka walioshinda kuanza kufanya kazi ya kuunganisha jumuiya hiyo na kuacha
kuwabeza wale walioshindwa.
“Lakini sisemi hivyo kwamba watu wa ovyo nao tuwakusanye hapana, majitu ya
ovyo, watoa rushwa, wezi, wenye muonekano mbaya katika jamii achaneni nao
hawatuongezei chochote, tunataka mtu ukimsimamisha mbele ya jamii, waseme yes
(ndiyo) huyu ni mtu safi,” alisema.
“Huyu anaweza kuwa kiongozi wa nchi, kiongozi wa wanawake na si kiongozi
ninayemtaka mie, uwe na mtu unayetaka wewe na mtu anayetakiwa na jamii.”
WANACHAMA WAPYA
Alisema wakiendelea na wanachama waanzilishi tu bila wapya jumuiya
itachosha na kwamba wakati alipopitia majina ya watu wanaogombea uongozi ndani
ya chama hicho, aliona uwepo wa idadi ndogo ya wasomi walioomba nafasi za
uongozi ndani ya jumuiya hiyo ikilinganisha na Jumiiya ya Vijana wa chama
hicho (UVCCM).
MALALAMIKO YA RUSHWA
Katika uchaguzi huo ambao Sophia Simba aliibuka kidedea kwa kupata kura 715,
Anne Kilango Malecela 310 na Mayrose Majinge kura saba, ulidaiwa kugubikwa na
rushwa.
Ilidaiwa kuwa wajumbe waligawiwa fedha katika nyumba za kulala wageni na kwenye
vyoo vya ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango.
Mmoja wa wagombea anadaiwa kuwasafirisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali na
kuwalipia gharama zote.
Malalamiko mengine kuhusu rushwa yametolewa na baadhi ya wagombea wa uenyekiti
wa mikoa. Waliolalamika ni Clement mabina (Mwanza), John Guninita (Dar es
Salaam), Thomas Ngawaiya (Kilimanjaro), Makongoro Nyerere (Mara) na William
Kusila (Dodoma).
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment