TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI VIONGOZI AINA YA MCHUNGAJI GETRUDE LWAKATARE NI AIBU KWA TAIFA
Hivi karibuni Waziri wa
Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Terezya Huvisa walitoa tamko kwamba
nyumba zote zilizojengwa kando kando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa,
bila wamiliki kulipwa fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za
mwaka 1992, 1995 na 2004.
Kauli hiyo ilitokana na
ukweli kwamba imekuwa ni jambo la kawaida kwa watu wenye nguvu ya fedha
kuharibu mazingira kwa makusudi pasipo kujali athari ambazo zinaweza kutokea
sasa na baadae kwa wakazi wa maeneo husika, jamii inayowazunguka na taifa kwa
ujumla! Kwa watu wengi, kauli ya mawaziri hao ilionekana kama ni hatua muhimu
sana katika kulinda mazingira ya fukwe zetu na jamii nzima hasa kutokana na
umuhimu wa kulinda mazingira katika wakati huu wa athari za mabadiliko ya
tabianchi.
Lakini baadhi yetu
tuliona kama ni mwendelezo wa kauli za Serikali ambazo utekelezaji wake ama
huwa ni wa mashaka au ukitekelezwa basi utekelezaji wake hutawaliwa na
upendeleo wa hali ya juu kwa watu wenye fedha na nafasi kubwa serikalini
(vigogo). Moja kati ya nyumba iliyotakiwa kubomolewa imejengwa kwenye viwanja
namba 2019-2020 Kawe Beach, katika fukwe za Bahari ya Hindi.
Viwanja ambavyo
vilipatikana kwa ushirikiano wa Mchungaji Lwakatare na tapeli maarufu wa Ardhi
jijini Dar es salaam, anayejulikana kwa jina la Frank Mushi. Ikumbukwe kwamba
katikati ya mwezi Julai, 2012 wananchi waliojenga nyumba katika maeneo
yanayosemekana ni tengefu ya Jangwani Beach, Mto Ndumbwi na Mto Mbezi
walivunjiwa nyumba katika operesheni iliyoendeshwa na Baraza la Mazingira la
Taifa (NEMC). Operesheni ambayo ilihusisha takriban nyumba 15 na kuta ( fences)
8. Katika nyumba hizo, mojawapo iliyotakiwa kuvunjwa ni ya Mchungaji Getruda
Lwakatare.
Lakini kwa sababu
ambazo wahusika, akiwemo yeye mwenyewe na serikali, wanazifahamu, nyumba yake
haikuguswa! Wakati wananchi wanaofahamu ukweli wa mambo, wakiwa bado wanahoji
chinichini juu ya upendeleo wa kitabaka ulio wazi, hivi karibuni wameshuhudia
kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, ikiripotiwa kuwa Mchungaji
Lwakatare (Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God na Mbunge wa Bunge la
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ) amehamia kwenye nyumba yake mpya.
Nyumba ambayo ilipaswa
kuwa imebomolewa kwa sababu imejengwa kwenye viwanja ambavyo ni kinyume cha
sheria kujenga katika maeneo hayo. Kuvunja sheria kwa uwazi namna hii, huku wengine
wakichukuliwa hatua kwa kuvunja sheria hiyo hiyo, si tu ni ’double standards’,
bali kunaweza kutafsiriwa ni kuitia serikali mfukoni.
Kitu kibaya zaidi ni
kwamba kiongozi huyo alishataarifiwa tangu mapema juu ya ubatili wa kujenga
katika eneo hilo, kupitia kwa huyo Frank Mushi kabla hata ujenzi wa nyumba hiyo
haujaanza. Ikumbukwe pia kuwa viwanja hivyo vilipatikana na ujenzi huo
kuwezekana baada ya eneo la bahari na mto kujazwa kifusi na mawe! Kwa kutambua
kuwa kuendelea na ujenzi katika eneo hilo ni kuvunja sheria za nchi zinazohusu
utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya jamii nzima, Mchungaji Lwakatare
aliendelea kwa kujiificha nyuma ya mgongo wa huyo Mushi, akijifanya hahusiki
kabisa na kilichokuwa kikiendelea katika eneo husika.
Kupitia barua hiyo,
wizara ilimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuchukua hatua za kubomoa/kuondoa
uendelezaji batili uliokuwa ukifanyika katika viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi
Kawe. Barua hiyo ilisainiwa na Bwana Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu
Mkuu wa Wizara. 2) Uthibitisho mwingine ni barua ya tarehe 30/9/2011 kutoka
NEMC kwenda kwa Bwana Frank Mushi. Barua husika, ilitoa maelekezo kwa Mushi
kuvirudisha katika hali yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa mujibu wa
vifungu 55(2) (a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,(4) (b) na (f) vya
Sheria ya Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004.
Barua husika
inabainisha kwamba timu ya wataalam toka Baraza la Mazingira (NEMC), Wizara ya
Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na Manispaa ya Kinondoni
ilitembelea eneo husika kufuatia malalamiko kutoka kwa viongozi na wakazi wa
Kawe Beach.
Timu hiyo ilibaini
kwamba eneo la Mto Ndumbwi, pamoja na bahari lilikuwa linajazwa mawe na vifusi
hali iliyosababisha kupatikana kwa viwanja na 2019 na 2020. Ambapo ndani ya
viwanja hivyo lilikuwa linajengwa jumba kubwa kinyume kabisa na vifungu
55(2)(a) , 55(2) (b) , 55(2)(d) na 55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira. Ilibainika
pia kuwa mikoko ilikatwa kinyume na s.63(1) ya Sheria ya Mazingira. Kwa mujibu
wa nyaraka nilizonazo, yafuatayo yalijitokeza i) Timu ya wataalam ilibaini
kwamba, tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilishatoa zuio la ujenzi katika
eneo husika. ii) Manispaa ya Kinondoni, mara kadhaa iliweka zuio la uendelezaji
na kutoa amri kwa ’mmiliki’ wa eneo husika kubomoa, lakini mmiliki huyo
alipuuza amri hiyo na kuendelea na ujenzi! iii) Ilitolewa amri ya Mahakama,
tarehe 5/4/2011 kumtaka Bwana Mushi asiendelee na ujenzi. Amri hiyo ilipuuzwa
na ujenzi ukaendelea.
Baraza la Mazingira
lilimwagiza tena, Bwana Mushi:- 2) Kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja
vyenye mgogoro. 3) Ndani ya siku saba, tokea amri husika kutolewa (amri
ilitolewa 30/9/2011) awe ametoa mawe na vifusi vyote vilivyoharibu mkondo wa
maji na bahari na kuurudisha mto na bahari katika hali yake ya kawaida. 4)
Ndani ya siku 30 chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
kuhakikisha kwamba mikoko yote iliyokatwa imerudishwa katika hali iliyokuwa
awali. Kwa gharama za Bwana Mushi.
Licha ya amri zote
hizo, mazuio yote hayo, matamko ya mawaziri yaliyotawaliwa na mbwembwe nyingi,
ujenzi uliendelea, nyumba imekamilika. Sasa inatumika. Wakati kigogo huyo
amehamia kwenye nyumba yake kwa matangazo na mbwembwe, Mto Ndumbwi, bahari na
mazingira kwa ujumla yameharibiwa vibaya! Bila kusahau kuwa wananchi wengine
wamebomolewa nyumba zao kwa kutumia sheria hizo hizo. Kwa mujibu wa Sheria ya
Mazingira, Sura 191 ya mwaka 2004, Fungu 57(1) hairuhusiwi kufanya shughuli
zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60 ambazo kwa asili yake zinaweza
kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi na utunzaji wa mazingira, utunzaji wa
bahari, kingo za mto, bwawa au mwambao wa asili wa ziwa.
Halikadhalika, Sheria
ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 ( Sura 113) Fungu 7 (1) (d) inabainisha kwamba
eneo lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto na bahari linatakiwa
kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa. Na pale inapotokea kuwa masharti
ya sheria moja yanapingana na masharti ya Sheria ya Mazingira, kuhusu mambo
yanayohusu usimamizi wa mazingira, Sheria ya Mazingira ndiyo hutumika, kwa
mujibu wa Fungu 232 la sheria ya mazingira sura Kutokana na hali hii serikali
inatakiwa kujinasua katika mwendelezo wa tafsiri wanayoipata wananchi kuwa
imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu wachache wenye uwezo.
Maana wanaona kuwa huu
ni mwendelezo wa serikali kuwa na kigugumizi pale sheria zinapovunjwa na vigogo
serikalini au watu wenye fedha wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi wa
serikali na chama tawala kufanya ufisadi. Wameona mambo ya namna hii mara
kadhaa, ikiwemo serikali kushindwa kuwachukulia hatua waliohusika na kashfa
kubwa za ufisadi kama ’akina’ Kagoda na wenzake (EPA), Richmond na kashfa
nyingine nyingi. Kwamba sasa inazidi kuonekana dhahiri kuwa kuna watu wako juu
ya sheria za nchi, huku wanyonge wakishughulikiwa.
Ni wakati mwafaka sasa
kwa mawaziri wanaohusika na masuala ya ardhi na mazingira kuwaeleza Watanzania
kulikoni wananchi wa hali ya chini kuvunjiwa nyumba zao kwa kigezo cha kuvunja
sheria wakati huo huo Mchungaji Lwakatare (kigogo) ambaye uharibifu wake ni wa
hatari kuliko hata hao waliovunjiwa akitamba mtaani kwamba yeye yuko juu ya
sheria na hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kumzuia kufanya alichofanya! Ni
aibu kwa Taifa kuwa na viongozi wa aina hii! Viongozi ambao wako tayari kutumia
fedha, hila, mamlaka na dhamana za uongozi walizopewa, kuhalalisha haramu, ni
janga kwa mstakabali wa taifa letu! Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na
Maendeleo ya Makazi
Imetolewa Dar es Salaam na;
Halima Mdee (MB)
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Imetolewa Dar es Salaam na;
Halima Mdee (MB)
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi
No comments:
Post a Comment