MTOTO
wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere, ameangushwa katika kinyang’anyiro cha
kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara,
ambayo sasa imechukuliwa na Christopher Sanya.
Makongoro
ambaye amekuwa mwenyekiti wa mkoa huo kwa miaka mitano, alishindwa katika
uchaguzi huo uliofanyika juzi chini ya usimamizi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu
(NEC) Taifa kutoka Mkoa wa Kagera, Nasir Karamagi.
Akitangaza
matokeo ya awali, Karamagi alisema kuwa kati ya kura 1,012 zilizopigwa, Sanya
alipata 469 na Makongoro alijikusanyia 402 huku Enock Chambili akiambulia 144.
Lakini
kwa mujibu wa Katiba ya CCM mshindi hakuwa amevuka nusu ya kura, na hivyo
ilibidi Sanya na Makongoro, kuingia katika duru ya pili ambapo mwenyekiti huyo anayemaliza
muda wake alipitwa kwa kura 59.
Akizungumza
baada ya matokeo kutangazwa, Makongoro alimuasa Sanya kufanya kazi kwa mujibu
wa katiba ya chama na kuvunja makundi yaliyoshamiri ndani ya CCM huku akiahidi
kutoa ushirikiano wake.
“Naomba
uwe muadilifu, mkoa huu wa Mara ni mgumu sana kuufanyia kazi, kwani kazi ya
uenyekiti si lelemama, hii ndiyo nafasi kubwa ambayo itatusaidia katika
uchaguzi wa 2014/2015,” alisema.
Makongoro
aliwataka pia wajumbe kuachana na mambo ya kambi, akisema uchaguzi umekwisha
kilichopo ni kushikamana na kuwapa ushirikiano viongozi wapya wakiongoze chama
vizuri.
Katika
nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM mkoa - kila wilaya nafasi mbili,
waliopenya ni Josephat Seronga na Ester Nyarobi (Serengeti), Zuhura Makongoro
na Jackson Waryoba (Bunda), Josehat Kisusi na Felister Nyambaya (Rorya).
Wengine
ni Grace Bunyinyiga na Thabita Idd (Butiama), Abdalah Jumapili na Kananda
Kananda (Musoma Mjini) na Mariam Mkono na Samson Gesase (Tarime).
Mbunge
wa Busega, Dk. Titus Kamani, amepata ushindi wa kishindo katika kinyanganyiro
cha uenyekiti Mkoa mpya wa Simiyu baada ya kujizolea kura 415.
Waliobwagwa
ni aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, George Nangale na Mwenyekiti mstaafu
wa CCM Wilaya ya Meatu, Enock Yacob.
Msimamizi
wa uchaguzi huo, Jackson Msome, alisema kuwa kati ya kura 714 zilizopigwa,
mbali na Dk. Kamani, Nangale alipata 234 huku Enock akiambulia 91.
Wakasuvi arejea Tabora
Mwenyekiti
CCM Mkoa wa Tabora aliyemaliza muda wake, Hassan Wakasuvi, amefanikiwa kutetea
kiti hicho kwa ushindi wa kishindo.
Wakasuvi
aliwamwaga wenzake watatu ambao ni Zuberi Mwamba, Juma Nkumba na Haji Bagio
ambao walijitoa muda mfupi kabla ya uchaguzi kuanza.
Akitangaza
matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Mwigulu Mchemba, alisema kati ya kura
996 zilizopigwa, Wakasuvi alipata 921, akifuatiwa na Zuberi Mwamba kura 75 na
16 ziliharibika.
Katika
nasaha zake, Wakasuvi aliwataka wajumbe wavunje makundi na wamsaidie kukijenga
chama, huku akiahidi kushirikiana na kila mmoja bila kujali makovu ya uchaguzi.
Alionya
kuwa wapo watu ambao wanadhani kwamba bila wao CCM Tabora haipo, akisema
atawachukulia hatua maana ndani ya chama wamekuwa wakiketi vikao vya kukibomoa.
Msukuma apeta Geita
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Joseph Msukuma, aliyeng’olewa
madarakani na Baraza la Madiwani kwa tuhuma za ufisadi, amechaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa kwanza wa CCM Mkoa mpya wa Geita.
Katika
uchaguzi huo, Msukuma alipata kura 565 kati ya 698 zilizopigwa na wajumbe wa
wilaya tano za Nyang'hwale, Geita, Chato, Mbogwe na Bukombe zinazounda mkoa
huo.
Msukuma
aliwabwaga Jeremiah Ikangala, aliyepata kura 130 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya
hiyo aliyemaliza muda wake, John Luhemeja aliyeambulia kura tano.
Mlao arudi Pwani
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Pwani, aliyemaliza muda wake, Mwinshehe Mlao, amefanikiwa
kutetea kiti chake baada ya kuibuka na ushindi wa kura 528 dhidi ya Kapteni
Mpembenue Seif Ally aliyepata kura 196 na Mziwanda Yahaya aliyeambulia 13.
Washindi
wa ujumbe wa NEC kutoka wilayani ni Halfan Mavala, Asia Madima (Kibaha
Vijijini), Fatma Ngozi, Mwajuma Denge (Bagamoyo), Hafsa Kilingo, Imani Madega
(Kibaha Mjini) na Bakari Mbonde, Hawa Mtopa (Rufiji).
Kingunge anena
Kada
mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema kuwa vitendo vya rushwa ndani
ya chama hicho, vimeshamiri kutokana na ubinafsi wa baadhi ya wanachama kuweka
mbele maslahi binafsi.
Mzee
Kingunge, alitoa kauli hiyo juzi mkoani Pwani, wakati akifungua mkutano wa
uchaguzi wa mkoa wa chama hicho, akisema kuwa ubinafsi huo umefanya vyama kuwa
mali ya mtu na ushindani unakuwa si wa kindugu bali uhasama.
Alisema
wakati wa Afro- Shiraz na TANU, nchi iliwekwa mbele tofauti na sasa ambapo
ubinafsi ndio unawekwa mbele na nchi inabaki peke yake.
“Kwa
kuwa suala ni ubinafsi ndiyo maana sasa watu wanafikia hatua ya kununua vyeo
kutoka kwa wapiga kura, jambo linalomdhalilisha mtoaji na mpokeaji wa
rushwa,”alisema.
JK ashauriwa
Mmoja
wa wagombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya CCM kupitia Wilaya ya
Bunda, Cyprian Musiba, amemshauri Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete,
kuwafutia matokeo baadhi ya wagombea waliopita kwa rushwa.
Musiba
ambaye ni mwanahabari kitaaluma na Mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano ya
I&RH, alitaja nafasi ambazo Rais Kikwete anapaswa kutengua matokeo yake
kuwa ni ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara na Morogoro.
Pia
Musiba alitaja washindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC katika wilaya za Monduli,
Bunda na Musoma Mjini pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Musiba alifafanua kuwa wenye fedha
wameifanya CCM kuwa sehemu ya kufichia madhambi yao, hivyo hawaoni hatari
kutumia gharama yoyote kupata uongozi.
“Penye
rushwa hakuna haki, hakuna kuwatumikia wananchi, mimi ni miongoni mwa wagombea
nilioshuhudia hali hii, watu kutoa fedha kwa ajili ya kununua uongozi ni jambo
la kawaida kwa CCM. Mkoani mara zimetumika zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya
kumwangusha Makongoro,” alisema Musiba.
Kada
huyo ambaye wiki iliyopita aliwasilisha malalamiko yake ndani ya chama kupinga
uchaguzi aliyoshiriki wilayani Bunda, alishauri kuwa rufaa hizo hazipaswi
kusikilizwa na kamati za siasa na maadili za wilaya kwa vile wajumbe wake ndio
watuhumiwa.
Alisisitiza
kuwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara, fedha zilikuwa zikigawiwa
wazi wazi kwa wajumbe na baadhi ya vigogo na wafanyabiashara wakubwa
kuhakikisha watu wao wanashinda.
“Viongozi
wanaotumia fedha ndani ya CCM hawawezi kuwa watetezi wa wanyonge. Na kwa rushwa
hii hata uchaguzi wa Bunda kanuni zilikiukwa kwa kuruhusu mfanyakazi wa
serikali kugombea,” alisema.
Musiba
alisema kuwa anaungana na kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, ya kutaka wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya CCM
wawajibishwe kwa kutoswa.
No comments:
Post a Comment