MBOWE ASEMA UJENGWE
MFUMO MPYA KUSAIDIA CCM KUKABIDHI MADARAKA BILA VURUGU
Mhe. Freeman Mbowe |
SERIKALI
imetakiwa kuandaa mfumo wa kikatiba utakaowezesha chama cha upinzani kuongoza
iwapo kile kinachotawala kitaondolewa madarakani.Kauli hiyo ilitolewa jana na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipokuwa akihutubia mikutano ya kampeni
ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata za Mpapa, wilayani Momba na Myovizi,
Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya.
Alisema
kutokana na vuguvugu la siasa za mabadiliko zinazoendelea nchini, ni wakati
mwafaka nchi ikawa na mfumo wa kikatiba na sheria kwa ajili ya kusimamia
mabadiliko ya uongozi kufanyika kwa amani ili kuepusha nchi kuingia katika
vurugu na mkanganyiko wa kisiasa.
Mbowe
alisema ingawa hiyo inaweza kuonekana kuwa ni dhana mpya, kutokana na umuhimu
wake kwa ajili ya mustakabali mwema wa Taifa, ni vyema Watanzania wakaanza
kuitafakari.
Alitola mifano
wa Ghana ilivyopitia misukosuko kutoka utawala wa Jerry Rawlings kwenda chama
cha upinzani cha Rais John Kufour.
Akiwanadi
wagombea wa Chadema katika maeneo hayo, Mbowe alisema ni hatari kwa nchi kama
Tanzania ambayo sasa inapitia kwenye wimbi kubwa la mabadiliko, kukosa mfumo
huo wa kuhakikisha mabadiliko ya mpito kutoka utawala wa Serikali moja kwenda
nyingine yanafanyika kwa amani na kulinda masilahi ya nchi bila vurugu.
“Ni muhimu sana kuwa na sheria itakayohakikisha 'transition' (kipindi cha mpito) kutoka Serikali ya chama fulani kwenda chama kingine au Serikali moja kwenda Serikali nyingine, kufanyika kwa amani na kwa kuhakikisha masilahi ya umma na nchi yanazingatiwa,” alisema na kuongeza:
“Lazima
tuepuke hali kama hiyo. Wenzetu wale (Ghana) walijifunza, walipoingia
madarakani wakaamua kutunga sheria ya kusimamia ‘transition period’ kutoka
uongozi wa Serikali moja kwenda nyingine.”
“Watanzania
wanaweza kujiuliza kwa nini Marekani inachukua siku 72 kwa Rais kuapishwa na
kukabidhiwa rasmi mamlaka ya kuongoza nchi tangu achaguliwe? Ni kwa sababu kuna
vitu vya muhimu sana vya kusimamiwa na kufanyiwa kazi kabla utawala mpya
haujakabidhiwa Ikulu.”
Mwenyekiti
huyo wa Chadema alisema wakati Marekani inachukua takriban siku 72 tangu
uchaguzi na uongozi mpya kukabidhiwa madaraka ya kuongoza nchi, Tanzania
inachukua wastani wa saa 48 pekee, akisema hali hiyo ni hatari kwa nchi kwani,
kuna masuala ya msingi ambayo yanahitaji muda wa kutosha katika kufanya
makabidhiano kutoka Serikali moja kwenda nyingine.
“Ni
wakati mwafaka kuanza kufikiria kuwa na mfumo huu wa kikatiba na kisheria.
Huwezi kutumia saa 48 tangu uchaguzi kufanyika kumkabidhi Rais mpya madaraka.
Kwanza kwa muda huo nani anasimamia kikamilifu rasilimali za umma, nini hatma
ya watumishi wa umma. Kuna masuala ya majeshi, nyaraka za siri na kila kitu,
vitu ni vingi. Wenzetu walio makini na nchi zao wanajua umuhimu wa masuala kama
haya. Wanapata muda wa kufanya 'orientation' (uelewa wa mazingira), alisema
Mbowe na kuongeza:
“Ndiyo maana hapa kuna wakati watumishi wa Serikali wakaamua tu kuikumbatia CCM hata kama nao wameichoka, kwa sababu wanakuwa hawajui hatma yao ni nini kwenye Serikali au uongozi mpya, baada ya uchaguzi.
“Ghana
katika kipindi hicho cha mpito kutoka Serikali moja hadi nyingine wameweka
utaratibu wa mamlaka inayoongozwa na mtu ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa
anasimamia rasilimali zote, nyaraka zote, zinakuwa zimeandikishwa, zinajulikana
zikoje.”
Alisema
lazima hatari hiyo izuiliwe kwa kuwa wakati Serikali mpya ilivyoingia Ghana,
waliokuwepo madarakani walichoma moto nyaraka muhimu na kuharibu vitu, kitendo
kilichosababisha Serikali iliyoingia madarakani kuhangaika kuanza upya.
Alisema
kutokana na hali kama hiyo ni lazima wananchi waanze kudai mfumo huo kwani hivi
sasa Katiba na sheria ziko kimya kitu kinachoweza kusababisha siku moja mtu
akakabidhi ukuta wa Ikulu tu kukiwa hamna kitu ndani.
“Mfumo huo utahakikisha 'smooth exit' yaani wanaoondoka au anayeondoka aondoke kwa amani. Kwa sasa hakuna 'mechanism' (mfumo) yoyote ile, hakuna utaratibu, hakuna sheria, Katiba iko kimya. Tunataka 'smooth exit', 'smooth entry' (Kutoka kwa amani, kuongia kwa amani).”
“Watumishi
wa umma wawe na uhakika wa kuwepo kwa Serikali, bila hivyo nchi inaweza kuingia
kwenye machafuko kwa sababu tu watawala waliokuwepo hawataki kuondoka.”
Mwenyekiti
huyo yuko kwenye ziara ya kuwanadi wagombea udiwani wa chama hicho katika kata
mbalimbali za Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa, katika uchaguzi mdogo
unaohusisha kata 29 nchini ambao umepangwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment