To Chat with me click here

Friday, October 12, 2012

MAGUFULI ATAJA MABINGWA WA RUSHWA WIZARANI KWAKE


Mhe. John Pombe Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema kati ya Idara zote za wizara yake, Idara ya Mizani imekuwa ikimtia kichefuchefu kwa sababu watumishi wake wengi akiwamo ndugu za vigogo ni wala rushwa.

Dk. Magufuli aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la ghorofa tano liloko kwenye mtaa wa Moshi, linalomilikiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA).

“Nawapongeza wafanyakazi wenzangu wa TBA na Tamesa kwa majukumu makubwa wanayoyafanya... ninajua ni wafanyakazi wachache waadilifu, kwenye mizani ni wala rushwa kweli kweli, na kwenye hili naomba uongozi wa mkoa utusaidie,“  alisema na kuongeza:

“Kwa sababu hata tulipowapeleka watu wa kuwahakiki hawawahakiki kwa hiyo nao wamejidhihirisha kuwa wanakuwa  sehemu ya wao, Mkuu wa Mkoa na mikoa yote watusaidie wafanyakazi walioko katika mizani na wengine inawezekana wako hapa hapa wananiangalia tu, ni wachache sana ambao si wala rushwa.”

Dk. Magufuli alisema watumishi hao wamekuwa wakitumia simu kuwasiliana na wasafirishaji, lengo likiwa ni kutafuta rushwa.

“Mara nyingi hawa ni ndugu wa wakubwa, siyo watoto wa watu wadogo wadogo, kila mtu anaomba mtoto wake aende kwenye mizani ….Endelea kuwasimamia, nakushukuru (Meneja wa Dodoma), umeanza kuwafukuza fukuza tu waende mahakamani waende wapi . Kwa sababu una mamlaka ya kuwafukuza ama kuwachukua,” alisema.

Alisema ametoa agizo kwa mameneja mikoani kuhakikisha kuwa hakuna mfanyakazi wa Mizani ambaye anaingia kazini na simu ya mkononi na kwamba atakayebainika kukiuka agizo hilo afukuzwe kazi.

Pia Dk. Magufuli alisema hivi sasa nafasi za kazi za maofisa wa mizani zitatangazwa ili kupata watu ambao watakuwa na sifa ili watakapokwenda kinyume washtakiwe mahakamani.

Alisema masharti ya kupata ajira hizo yatakuwa makali.

“Unashangaa utakuta magari mengi yamekamatwa katika mizani, lakini kesho yake hayapo,” alisema Dk. Magufuli na kuwafanya baadhi ya watumishi wa wizara hiyo waliokuwepo katika eneo hilo kuguna kwa sauti.

Alisema mapato yanayokusanywa na mizani kutokana na faini ya makosa ya kuzidisha uzito ni Sh. bilioni tatu huku kiasi kama hicho kikitolewa kwa ajili ya kuhudumia vituo hivyo vya mizani.

Aidha, alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga,  kuhakikisha kuwa wahandisi wa mikoa yote nchini wanajenga majengo kwa ajili ya ofisi na nyumba za kuishi.

Dk. Magufuli alimtaka Mwakalinga kuwatimua kazi wahandisi wa mikoa ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao huo.

“Umewapeleka kule kulala? wenzao wa Arusha wameshajenga majengo mawili, wa Dodoma wanajenga, kila injinia wa mkoa aonekane anachofanya hakuna sababu ya kumpeleka kusoma wakati hana anachokifanya…Lazima wajitume katika kazi zao,”alisema Dk. Magufuli.

Alisema kwa kuwafukuza watumishi wabadhirifu kutasaidia kuwapunguza.


MALALAMIKO YA UUZWAJI WA NYUMBA ZA SERIKALI

Dk. Magufuli alisema suala hilo halikuanza nyakati za uongozi wa awamu ya tatu bali hata wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambapo nyumba mbalimbali zinazomilikiwa na serikali ziliuzwa kwa wananchi.

Alisema mwaka 1963 wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi,  nyumba za serikali ziliuzwa kwa wananchi na kwamba suala la kuuza nyumba mwaka 1995 halikuwa jipya kwa sababu lilishafanyika.

“Kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni kuendelea kujenga nyumba nyingi na kuziuza kwa wananchi…mbona wanalalamikia kuuzwa kwa nyumba, mbona viwanda vilipouzwa kwa Wahindi hawakulalamika ama kwa sababu anayeuziwa ni Mtanzania?” alihoji Dk. Magufuli.

MADENI YA  TAASISI ZA UMMA

Dk. Magufuli alisema TBA ina haki ya kuwashtaki wadeni sugu wote na ikiwezekana kuwafukuza katika majengo yao kwa kufuata taratibu za kisheria.

“Orodhesha wote mnaowadai na waliopanga katika nyumba za serikali walipe madeni yao…mnahaki ya kuwashtaki wadeni sugu bila kujali vyeo wala taasisi zao na ikiwezekana kuwafukuza kwenye nyumba za serikali,” alisema.
 

ANZISHENI KAMPUNI YA UJENZI

Dk. Magufuli aliipa TBA miezi mitatu kuanzisha kampuni ya ujenzi ambayo itakuwa na uwezo wa kujenga majengo yake bila kutafuta wakandarasi kutoka nje ya wizara.

“Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za ujenzi, mtaajiri Watanzania wengi na fedha zitabaki hapa hapa nchini badala ya kwenda nje ya nchi,” alisema.

Aliongeza kuwa hata kama watalazimika kuwaajiri wataalamu wachache kutoka nje ya nchi basi wafanye hivyo.

MKUU WA MKOA WA DODOMA


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, alisema kuanzia sasa kiongozi ambaye eneo lake litafanyika bomoa bomoa atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwekwa rumande.

Alisema hatua hiyo imefuatia viongozi wengi hasa wa kuchaguliwa na wananchi kupita na kuwadanganya wananchi kujenga katika maeneo yasiyopimwa pamoja na kwamba wanajua wanavunja sheria.

“Viongozi wengi hasa wanaoingia madarakani kwa njia ya kuchaguliwa wamekuwa wakiwapotosha wananchi kwa kuwataka kujenga katika maeneo yasiyopimwa hii ni dhambi kubwa,” alisema na kuongeza kuwa:

“Kiongozi yeyote tutakayeingia kubomoa nyumba, tutahakikisha naye tunambomoa…hata kuwakamata kuwaweka ndani ili wakasemee wakiwa huko huko ndani.”

No comments:

Post a Comment