To Chat with me click here

Monday, October 8, 2012

FREDERICK SUMAYE AIVUA NGUO CCM

Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye akizungumza na waandishi jana.
Baada ya kuangushwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Hanang’, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameibuka na kueleza kuwa sasa chama hicho kinaandamwa na rushwa mpya aliyodai imetoka kwa mtu kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na sasa kuna rushwa za kimtandao.

Rushwa za kimtandao alisema ni zile ambazo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji katika safari za ndoto zake za kuwania uongozi ndani ya chama hicho.

Alizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam aliouitisha mahususi kueleza yaliyojiri katika uchaguzi huo uliofanyika Septemba 29, mwaka huu.

Mwaka huu, alisema rushwa hiyo ndiyo iliyotumika katika uchaguzi Nec Hanang', mkoani Manyara, ambako aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika kinyang’anyiro hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu alimwangusha.

Alisema mambo yaliyotokea katika uchaguzi huo, yalitokea pia katika chaguzi nyingine za CCM zilizofanyika katika maeneo mengi nchini, tofauti ikiwa ni viwango vya yaliyotokea na sura za watu waliohusika na matukio hayo.

Alisema katika sura ya kitaifa, uchaguzi wa CCM unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini umegubikwa sana na matumizi makubwa ya fedha za rushwa.

“Suala la rushwa katika nchi yetu na katika chama chetu siyo geni, lakini sasa nahisi tatizo hili sasa limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa. Mimi binafsi nilizungumza tatizo hili mara kadhaa,” alisema Sumaye.

Alisema mapambano dhidi ya rushwa ni agenda ya kudumu kwake na kwa hiyo ataendelea nayo popote atakapokuwapo.

“Hivi leo tunavyoongea hali ya rushwa wakati huu wa uchaguzi imekuwa mbaya zaidi. Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapigakura humchagua mwakilishi wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake, yaani humchagua mwakilishi wao kwa ajili yao.

Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachagulia watu mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapigakura ni wapiga mihuri tu,” alisema Sumaye na kuongeza: "zamani kulikuwa na rushwa ya mtu kuwahonga watu fedha wa eneo fulani ili achaguliwe, lakini leo hii kuna rushwa ya kimtandao."

Alisema watu wanaochaguliwa kwa utaratibu huo, utumishi na uaminifu wao siyo kwa wale waliopiga muhuri kuidhinisha zile kura alizopata, bali ni kwa fedha zilizonunua zile kura na hasa kwa aliyetoa au waliotoa fedha, hivyo Watanzania kuwa na wawakilishi wa mtu au watu na siyo wa umma.

Kutokana na hilo, aliwaomba Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa wanavyotoka, kupiga vita hali mbaya aliyosema kuwa inadhihaki na kudhalilisha demokrasia na pia inayodhalilisha utu wa wananchi wanaopiga kura.

RUSHWA UCHAGUZI WA NEC WILAYA YA HANANG’


Alisema uchaguzi wa Nec Wilaya ya Hanang, uligubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho vingi, uharamia wa kuhamisha wapigakura usiku na maovu mengine mengi, ambayo hakuyataja.

Akijibu swali aina gani ya rushwa iliyotumika katika uchaguzi huo, alisema: “Ni ya mtandao” na kusema fedha hizo pamoja na mtu aliyezipeleka hamjui.

Alisema mtandao uliopo siyo mmoja, bali wenye mitandao wapo wengi.

Pia akijibu swali kuhusu madai kwamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alishiriki katika mtandao huo, Sumaye alimtaka mwandishi kwenda kumuuliza Lowassa suala hilo.

Hata hivyo, alisema hajakata tamaa na wala hatakata rufaa ya kupinga matokeo wala kupeleka malalamiko katika chama kwa sababu yaliyokuwa yanatendeka yalikuwa yanafahamika na kwamba hata vyombo vya habari vilitolea taarifa mara kadhaa.
“Narudia tena mimi nitabaki mwanachama mwaminifu wa CCM,” alisema.

Alisema Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alipokuja na kaulimbiu ya kuleta mageuzi katika chama, maarufu kama “kujivua gamba” yeye (Sumaye) ni miongoni mwa watu waliofurahishwa na pia alimpongeza kwa hilo.

Alisema kama kuna mtu atathibitika kuhusika na kashfa ya ufisadi ndani ya chama anatakiwa aadhibiwe na kuwapisha wanachama wengine, kwani anaharibu sifa nzuri ya chama.

Pia akijibu swali kwamba, kwa nini asimtafute Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kumlalamikia kuhusu yaliyotokea katika uchaguzi wa Hanang, alisema hawezi kufanya hivyo, kwa sababu yeye siyo katika aina ya watu wanaopenda kukimbilia Ikulu kwenda kulalamika kwa Rais na kwamba, siyo kila kitu lazima mtu akimbilie huko (Ikulu).

Alisema kuangushwa katika uchaguzi huo hakujadhoofisha ndoto zake za kisiasa, badala yake kumempa nguvu zaidi, kwani kugombea urais akiwa nje ya chama ni vizuri zaidi kuliko kuwa ndani ya chama.

KUPASUA JIPU, BOMU

Awali, akinukuu vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti vilivyosema: “Sumaye kupasua jipu Dar es Salaam na “Sumaye: Nitalipua bomu jipya”, alisema hana jipu wala bomu la kupasua.

Alisema kama kulikuwa na bomu au jipu limeshapasuka na waandishi wa habari wanalijua.

KUMTANGAZIA VITA LOWASSA


Kuhusu habari za baadhi ya magazeti kwamba: “Sumaye amtangazia vita Edward Lowassa” na “ikiwa Lowassa atawania urais, Sumaye ataingia katika mpambano huo kukabiliana naye kwa njia yoyote ile. Hataki kusema ataingia kwa CCM au chama gani au mgombea binafsi”, alisema ni hisia za chanzo cha habari hizo kama kipo, ambacho alisema hakifahamu.

“Mimi sijaongea na mtu yeyote mambo hayo wala nisingeweza kuyasema hayo kwa sababu kwanza sina uhasama na Mheshimiwa Lowassa na pili nikiamua kugombea urais sitagombea kwa sababu ya mtu fulani bali nitagombea kwa sababu ya nchi na wananchi wa Tanzania,” alisema Sumaye.

KUTETA NA CHADEMA


Kuhusu madai kwamba aliteta na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) siku chache baada ya kuangushwa katika uchaguzi huo wa NEC Wilaya ya Hanang, Sumaye alisema tatizo hapo siyo mtu kukutana na viongozi wa chama hicho.

Bali alisema habari hiyo siyo ya kweli, kwani hajakutana na kiongozi yeyote wa Chadema wala wa chama chochote cha upinzani.

Hata hivyo, alisema kuna haja ya Watanzania kufikia kwenye ustaarabu kwamba, vyama vya upinzani siyo maadui wala viongozi wao siyo maadui wa viongozi wa CCM.

“Mimi ningekuwa nimekutana nao ningesema tu mbona hata hao wengine wanaotafuta urais kwa udi na uvumba huwa wanakutana nao?” alihoji Sumaye na kuongeza:

“Nasikitika sana kusema kuwa habari hii iliyotengenezwa kwa kusudi maalum, na picha yangu kuwekwa pamoja na Mheshimiwa Mbowe kana kwamba, kweli tulikuwa kwenye mazungumzo, imebeba uvumi mzito kuwa kama nitaingia Chadema ikibidi nitashughulikiwa itakavyoonekana inafaa ili nisivuruge mipango ya watu fulani kuingia Ikulu.

“Dawa siyo kushughulika na wanaokihama chama bali tushughulikie yale yanayowahamisha kwenye chama chetu. Mimi namwomba Mwenyezi Mungu kuwa huu uwe ni uvumi usio na msingi tusije tukaiingiza nchi katika matatizo makubwa kuliko tunavyofikiri.”

Alisema yeye ni mwanachama mwaminifu wa CCM na kwamba, alishawahi kusema yeye hayuko CCM kwa ajili ya cheo na wala kukosa kwake Nec na hasa kwa njia iliyotumika hakunyimi usingizi wala hakumzuii kugombea urais kwa tiketi ya CCM endapo ataamu kufanya hivyo.

“Lakini nataka kukumbusha kuwa hata Baba wa Taifa na mwanzilishi wa chama hiki aliwahi kusema kama chama kikiacha misingi yake atakiacha. Chama si mama yake. Kilichomuudhi Mwalimu wakati huo, pamoja na mambo mengine, ni hali ya rushwa katika chaguzi zetu. Hivyo, tusiandame watu bali tuandame maovu,” alisema Sumaye.

Alisema Septemba 6, mwaka huu alipokuwa akifunga mafunzo ya waandishi wa habari viongozi, alitahadharisha sana juu ya waandishi kutumika vibaya hasa nyakati za uchaguzi kwa maslahi ya watu binafsi badala ya maslahi ya umma au ya taaluma yenyewe.

Hivyo, akasema hana uhakika kama ‘gonjwa’ hilo halijaanza kuwakumba baadhi ya waandishi hapa nchini.

Hata hivyo, alisema angependa kuamini kwa sasa kuwa labda hayo yaliyotokea ni utaratibu wa kawaida wa wanahabari kuchokonoa habari, lakini akawataka wasivuke mipaka wakajioteshea ndoto za uchokozi.

Alisema nchi nyingi hasa zenye demokrasia changa kama Tanzania zimeingia katika vurugu na kuhatarisha amani na utulivu nyakati za chaguzi.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba Watanzania wasichafue historia yao nzuri ya amani na utulivu kwa ajili ya uroho wa madaraka.

“Madaraka yatakuja kama wananchi wapigakura wanaona wewe ndiye utakayewafaa na wala tusiwarubuni kwa fedha au jambo lolote kwa kutumia vibaya nafasi ya umaskini wao,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Napenda nitambue kuwa haya ninayoyasema siyo matamu masikioni mwa baadhi yetu, lakini ni vema tukayasikiliza kwa makini na kuchukua hatua chanya ili yasilete madhara zaidi katika jamii na wala tusidiriki kuwanyamazisha wanaoyazungumzia kwa uwazi. Hawa wanatuonyesha tahadhari iliyoko mbele yetu kama taifa,” alisema Sumaye.

Akijibu swali kama bado ana imani na uongozi wa CCM hasa baada ya kubaini chama hicho kimegubikwa na rushwa, alisema bado ana imani na chama hicho kwani kama chama hakina matatizo.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuwa bado ana imani na viongozi wa CCM, bado hawajaweza kujisimamia vya kutosha kupambana na uovu, ambao alisema kina uwezo wa kubadilika licha ya kwamba, hajui lini mabadiliko hayo yatapatikana.

Alisema umma mpana wa Watanzania hautaki rushwa na unaumia sana na rushwa, hivyo akavishauri vyama vya siasa kujirekebisha kabla wananchi hawajasema sasa inatosha, kwani wakisema hivyo itakuwa ni hatari.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 na Mbunge wa Hanang' kwa miaka 20 (1985-2005).
 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment