MWENYEKITI
wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe,
amelionya Jeshi la Polisi akisema haliwezi kuzima vuguvugu la mabadiliko (M4C)
nchini kwa kutumia risasi kutisha na kuua wananchi.
Badala
yake, amelitaka kufanya shughuli zake kwa utaalamu kwa kuzingatia sheria na
kanuni zinazolisimamia na kuepuka kutumiwa kutekeleza matakwa ya watawala
wanaowaagiza kuwanyanyasa wapinzani.
Mbowe
alitoa onyo hilo juzi wakati akimnadi mgombea wa udiwani wa Kata ya Daraja
mbili, Prosper Msofe katika Mtaa wa Jamhuri, ambaye hata hivyo hakuweza kuhudhuria
mkutano huo kutokana na kulazwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru akipatiwa
matibabu ya uti wa mgongo baada ya kushikiliwa na polisi.
Licha
ya mgombea huyo kutokuwepo mkutanoni, Mbowe alimtaka kutotishika na tukio
lililompata badala yake iwe changamoto ya kuzidi kudai na kupigania haki kwa
maslahi ya umma.
“Kama
sababu ya CHADEMA kuitwa chama cha vurugu ni kwa kutokana na hatua yetu ya
kuwahamasisha watu kudai na kupigania haki zao, basi acha tuendelee kutambulika
hivyo,” alisema.
Mbowe
alieleza kushangazwa na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa
kutangaza uchaguzi katika kata nne za Jiji la Arusha ambazo zilikuwa
zinaongozwa na madiwani waliotimuliwa CHADEMA tangu mwaka jana licha ya juhudi
walizofanya kuikumbusha kwa maandishi.
Kata
hizo ni Elerai, Kimandolu, Kaloleni, Themi na Sombetini iliyokuwa ikishikiliwa
na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo,
ambaye alijivua gamba kwa kujiunga na CHADEMA.
“Woga
wao wanajua nguvu ya CHADEMA kwa sasa, wanaogopa kuona tukishinda viti hivi na
kuingiza madiwani sita pamoja na wa viti maalum, idadi ya madiwani wetu itakuwa
kubwa, hivyo tutaongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha,” alisema.
Akizungumzia
utaratibu wa CHADEMA kuwachangisha wanachama wake fedha kwenye mikutano yao kwa
ajili ya kuchangia gharama za uendeshaji, alisema kuwa chama kinajengwa na watu
wenye fedha safi kama hizo.
Naye
Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa wa CHADEMA, Godbless Lema, aliwataka polisi wadogo
kutokubali kutumiwa kutekeleza amri za kikandamizaji za viongozi wao kuumiza
wananchi kwani mwisho wa siku watakaohukumiwa ni wao.
Alisema
kuwa kwenye vurugu za Arusha za Januari 5 mwaka jana, walikufa watu watatu
ambapo polisi wa vyeo vya juu ndio walioongezewa vyeo huku wale wa chini
wakiambulia patupu.
No comments:
Post a Comment