To Chat with me click here

Thursday, October 4, 2012

‘NI NDOTO KATIBA MPYA KUPATIKANA 2014’

Mwenyekiti wa Jukwaa la katiba Tanzania Bw.Deus Kibamba (katikati)akizungumza na waandishi wahabari Dar es Salaam jana,(hawapo pichani) kuhusu mchakato wa kukusanya maoni kwa ajili ya uundaji wa katiba mpya Tanzania katika mikoa mbalimbali ya tanzania kushoto ni Mratibu jukwaa hilo Bi.Diana Kidala na kulia ni Mjumbe Bw.Israel Ilunde.

******************************************
 
JUKWAA la Katiba Tanzania limesema ni ndoto kwa Katiba Mpya kukamilika Aprili 12, mwaka 2014, kama ilivyoahidiwa na Serikali. Tathmini hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kibamba alisema, kutokana na utafiti uliofanywa katika mikoa mbalimbali, jukwaa hilo limebaini ni vigumu, Katiba hiyo kupatikana kwa wakati kutokana na utaratibu mbovu uliopo.

Alisema muundo uliopo hivi sasa, unawanyima haki baadhi ya wananchi kutoa maoni na kusema kuwa, ni vigumu kukamilika haraka ukusanyaji wa maoni ya muundo wa Katiba mpya.

“Tume ya kukusanya maoni ya muundo wa Katiba mpya, imeonesha wazi haiwezi kukidhi matakwa ya baadhi ya wananchi kutokana na muundo uliopo.

Alisema utaratibu wa sasa haujawapa uwezo wa kutoa maoni walemavu wa masikio, macho na wale wa ngozi, hivyo kundi hilo limenyimwa uhuru wao wa kutoa maoni kwa ajili ya Katiba mpya.

“Naomba kusisitiza hili, tume lazima ifanye kazi kwa umakini, kwani inaonesha makundi haya maalum yametengwa na yanatakiwa kupewa uhuru wao.

“Ni muda mwafaka kwa tume kutafuta wataalam wa alama kama ambavyo walishauriwa, ili kuwapa haki ya msingi walemavu wa kutokusikia kutoa mawazo yao,” alisema Kibamba.

Aliongeza katika mikoa 15 ambayo hadi sasa tume hiyo imepita kukusanya maoni, yapo maeneo mengi ambayo tume hiyo haijakutana na wananchi, hivyo muda zaidi unahitajika.

“Ninachofikiria hapa tume hii inasukumwa na baadhi ya wanasiasa ambao wana maslahi ya kukamilisha ripoti ya ukusanyaji maoni ya muundo wa Katiba mpya, kwa maslahi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema.

No comments:

Post a Comment