MGOMBEA udiwani kata ya Daraja Mbili
kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Prosper Msofe,
amelazwa kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru akisumbuliwa na maumivu ya uti
wa mgongo baada ya kuzuiliwa kwenye kituo cha polisi cha kati, Arusha usiku wa
juzi kuamkia jana.
Katibu wa wilaya ya Arusha wa CHADEMA,
Martin Sarungi, na aliyekuwa mbunge wa Arusha, Godbless Lema, waliwaeleza
waandishi wa habari mbele ya kituo cha polisi kuwa mgombea wao alikamatwa
majira ya saa mbili usiku eneo la Friends Corner baada ya kuhoji sababu
wamachinga kunyang’anywa bidhaa zao na Ramadhan Kalamba (56) anayedai kuwa
halmashauri ya jiji imempa jukumu la kuwaondoa machinga katikati ya jiji.
“Msofe alihoji sababu za Ramadhan
kuchukua mali za wamachinga majira ya usiku wakati ambao halmashauri haifanyi
kazi; alikuwa akizipeleka wapi na ni nani aliyempa mamlaka ya kuchukua vitu
hivyo ndipo gari la polisi likafika na kumchukua,” alisema Lema.
Walisema kuwa baada ya kupata taarifa
za mgombea wao huyo kukamatwa, baadhi ya wanachama na viongozi walimfuatilia
mpaka kituo cha polisi kwa lengo la kumwekea dhamana jambo ambalo
lilishindikana ndipo majira ya saa nne usiku wakaamua kuondoka.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani hapa
(RPC), Liberatus Sabas, alikanusha madai hayo kwa kile alichoeleza kuwa mgombea
huyo hakunyimwa bali alikataa dhamana mwenyewe ambapo alidai kuwa alikamatwa na
askari wa doria na kufikishwa polisi kwa tuhuma za kumpiga ngumi ya kifuani
Kalamba.
Alisema kuwa jeshi la polisi lilipata
taarifa kuwa Kalamba anashambuliwa ndipo askari wa doria walipofika na
kumchukua Msofe ambapo alisema kuwa mzozo baina ya wawili hao ulitokana na
hatua ya Msofe kuhoji sababu za Kalamba kutaka wamichinga hao waondoke eneo hilo
huku akijaribu kumzuia asiendelee kutangaza.
Awali jana majira ya saa nne asubuhi
mgombea huyo wa CHADEMA alienda kupatiwa matibabu kwenye zahanati ya polisi
akiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi ambapo daktari wa zahanati hiyo
alishauri apelekwe hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi lakini polisi waliamua
kumpeleka mahakama ya mwanzo ya Maromboso.
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwa
mahakamani hapo walikwenda kuuona uongozi wa mahakama na kuwaonyesha cheti
alichopatiwa mtuhumiwa huyo kinachomtaka apelekwe hospitali ya mkoa kwa
uchunguzi zaidi jambo ambalo linadaiwa pengine ndilo lililopelekea mtuhumiwa
huyo kutofikishwa mbele ya hakimu.
Mgombea huyo ambaye alikuwa amepakiwa
kwenye gari ya polisi yenye namba za usajili PT 1844 ambayo ubavuni imeandikwa
OCD Arusha alikaa rumande ya mahakama hiyo kwa zaidi ya saa moja ambapo gari
hilo lilirudi likiwa limeongeza idadi ya askari wenye silaha wakiongozwa na
Mkuu wa Polisi wa wilaya hii (OCD), G. A Muroto na kumchukua ambapo walimpeleka
moja kwa moja hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Wagombea wengine katika kinyang’anyiro
hicho na vyama vyao kwenye mabano ni Philip Philip (CCM), Mohamed Msuya
(NCCR-Mageuzi), William Laizer (TLP) na Zani Zakaria (CUF).
No comments:
Post a Comment