To Chat with me click here

Monday, October 15, 2012

BABA AMWUMBUA MTOTO WAKE ANAYEGOMBEA UDIWANI



AMTANGAZA HADHARANI KUWA NI MWIZI, HANA SIFA

MGOMBEA udiwani wa Kata ya Mwawaza Manispaa ya Shinyanga, Anthony Peter (CHADEMA), juzi aliumbuka baada ya baba yake mzazi kumtangaza katika mkutano wa hadhara, kuwa hana sifa za kuwania nafasi hiyo kwa madai kuwa ni mwizi.

Hali hiyo ilijitokeza katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo, ambao umeitishwa baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo Charles Magina, kufariki dunia kwa ajali ya pikipiki.

Katika mkutano huo, mzazi wa mgombea huyo mzee Peter Molla (62), aliwaacha hoi wafuasi wa CCM na wananchi wengine pale alipomshambulia kijana wake akisema kuwa, hafai kuwa kiongozi.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa, Molla alisema pamoja na kuwa mwanaye huyo hapendi kufanyakazi, licha ya kuwa na umri mkubwa na kwamba muda mwingi amekuwa akizurura kwa ndugu zake kijijini bila ya mafanikio.

Molla alisema, hivi karibuni aliuza ng’ombe zake kwa ajili ya kwenda kumuokoa mgombea huyo, baada ya kukamatwa na polisi usiku kwa kosa la kukutwa na bunduki kinyume cha sheria.

“Mimi sikujua nilidhani nimezaa mtoto wa kiume ambaye atakuja kunilea na kunitunza uzeeni, kumbe hakuna kitu, amenitelekeza hapa mnaniona na umri huu nimebaki napata shida.

“Siyo siri mwanangu amekuwa mwizi, hawezi kukaa sehemu moja anatangatanga ovyo na makundi ya vijana wenzake anaozunguka nao huku wakimshauri mambo machafu, hao jamaa zake nao ni wezi,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa Shinyanga, Khamis Mgeja ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika uziduzi wa kampeni hizo, aliwasihi na kuwaomba wakazi wa kata ya Mwawaza, kumchagua mgombea wa CCM Juma Nkwabi, kwa maendeleo ya kata yao.

“Chagueni Chama cha Mapinduzi, chagueni mgombea wa CCM kwa vile chama chake kina majibu ya kero zenu na lengo la chama chetu ni kuhakikisha wakazi wa Ndala na Manispaa ya Shinyanga, wanapata maendeleo ya dhati,” alisema.

Mgeja aliwaeleza na kuwashawishi wapiga kura wa kata hiyo, kutowachagua wagombea wa vyama vya upinzani kwa madai kuwa sera za vyama hivyo hazina dira.

No comments:

Post a Comment