To Chat with me click here

Thursday, October 18, 2012

RUSHWA YAVUNJA UCHAGUZI CCM PWANI


TUHUMA za kushamiri kwa vitendo vya rushwa katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM mkoani Pwani, jana vilimlazimisha mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Mwinshehe Mlao kuvunja mkutano huo.

Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike kwenye Jengo la Mkuu wa Mkoa wa Pwani, uliahirishwa saa chache, kabla ya upigaji kura kuanza kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba baadhi ya wajumbe walikuwa wakitoa na kupokea rushwa ili kushawishi ushindi wa baadhi ya wagombea.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza aliwaeleza wajumbe hao kuwa amepata taarifa kutoka vyombo vya usalama kuwa uchaguzi huo umegubikwa na vitendo vinavyoashiria kuwapo na rushwa.

Akiahirisha mkutano huo jana, Mlao alisema amelazimika kusitisha uchaguzi huo hadi utakapotangazwa tena, kutokana na baadhi ya wajumbe kukidhalilisha chama kwa kujihusisha na rushwa.

“Kwa haya yaliyotokea lazima tuwasiliane na wenzetu makao makuu. Baada ya kusema haya natangaza kuahirisha kikao hadi tarehe ya uchaguzi itakapotangazwa tena,” alisema Mlao.

Akizungumza katika mkutano huo, Mahiza alilaani kitendo hicho akisema kuwa kimeidhalilisha CCM na ofisi yake.

Awali Mahiza alisema kuwa alipata taarifa kutoka kwa maofisa wa Takukuru kuhusu kuwapo kwa mazingira ya rushwa yanayofanywa na wajumbe wa mkutano huo na baadaye alifika katika ukumbi wa mkutano.

“Baada ya kupata taarifa kuhusu mazingira ya rushwa, nilitoka nje na kweli ukumbini sikukuta watu. Niliposhuka chini niliwakuta wajumbe wengi wakiwa wamesimama makundi. Sikujua na wala sikushuhudia nani aliyekuwa anatoa rushwa ila maofisa wangu wameliona hilo," alisema Mahiza.

Mkuu huyo wa mkoa aliendelea kusema, "Najua nitabeba lawama kubwa sana, nitatukanwa sana na baadhi yao, lakini hili sitalivumilia.”

Nafasi iliyodaiwa kuwa ndiyo iliyokuwa ina wagombea waliokuwa wakichuana vikali zaidi ni katibu wa uchumi ambayo wagombea wake ni, Imani Madega na Haji Abuu Jumaa.

Baada ya kuahirishwa kikao hicho,  Mahiza alifanya kikao cha ndani na wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa (NEC) wa mkoa huo, Ridhiwan Kikwete na Rugemalila Lutatina.

Alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, " Waseme wenyewe wa Pwani. Kama imetokea leo siwezi kupata taarifa leo."

Aliendelea kusema," Kama imetokea wataleta taarifa, zikifika tutakuwa na cha kuzungumza, lakini leo waache waseme wao kwanza."

Msindai naye juu
Mbunge wa zamani wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida.

Msindai maarufu kwa jina la ‘CRDB benki’, ameshinda kiti hicho baada ya kupata kura 673 dhidi ya 41 za mpinzani wake, Amari Rai.

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Joramu Allute aliangukia pua mapema baada ya kupata kura 194 kwenye duru ya kwanza kwa  kupata kura ambazo hazikutosha na kuondoka wakati mkutano huo ikiwa unaendelea.

Mabima akata rufaa
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina amekata rufaa kutokubaliana na matokeo yaliyompa ushindi  Anthony Diallo katika uchaguzi uliofanyika juzi.

Katika uchaguzi huo ambao msimamizi wake alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvu, Diallo alishinda kwa kura 611 na mpinzani wake Mabina aliambulia kura 328.

Hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Joyce Masunga alisema kulingana na kanuni za uchaguzi wa chama, rufaa hiyo inapaswa kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa CCM na kwamba yeye hayuko tayari kuipokea.

Alisema kwa kuwa Mabina ametangaza nia ya kukata rufaa basi ni imani yake kwamba atazingatia kanuni husika.

Akizungumzia kupinga ushindi wa Diallo, Mabina alisema mpinzani wake huyo alikiuka misingi na kanuni za uchaguzi kwa kuzungukia wajumbe ikiwa ni pamoja na kudaiwa kuwapa rushwa.

No comments:

Post a Comment