KUNA
taarifa za kutatanisha kuhusu afya ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambapo
inadaiwa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Habari
tulizopata toka nchini India kwa watu wake wa karibu, zimeeleza kuwa Spika
amelazwa tangu wiki iliyopita katika hospitali hiyo.
Vyanzo
vyetu hivyo vilisema, Spika Makinda ameongozana na watu watano ambao wamekuwa
wakionekana naye hospitalini hapo.
Hata
hivyo, hatukuweza kufahamu mara moja ugonjwa unaomsumbua kutokana na jambo hilo
kuwa siri kati ya mgonjwa na madaktari wake.
Taarifa
za ndani zinasema kuwa baadhi ya watu waliofika kumuona waliambiwa kwamba
anasumbuliwa na macho.
Alipoulizwa
kuhusu taarifa hizo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alikiri kuwa Spika
alikwenda nchini humo kwa shughuli mbili ikiwamo ya kufanya uchunguzi wa afya
wa kawaida.
Alisema
Makinda alikwenda nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu kwenye mkutano wa Maspika
Wanawake (IPU) na baada ya kumaliza shughuli hiyo ndipo akaenda kufanya
uangalizi wa afya yake.
Kashilila
ambaye hata hivyo alikwepa kuzungumzia kama Spika amelazwa, aliishia kusema tu
kwamba alipitia kufanya uangalizi wa kawaida wa afya yake na amekuwa akifanya
hivyo kila mwaka.
Kwa
mujibu wa Kashilila, Spika atarejea wiki ijayo baada ya kumaliza taratibu zote
za kuangalia afya yake.
Wakati
Dk. Kashilila akisema hivyo, mitandao mbalimbali ya intaneti, ilionyesha kuwa
mkutano huo wa maspika wanawake ulifanyika kati ya Oktoba 3 hadi 4 mjini New
Delhi, nchini humo.
Hivyo,
endapo Spika alitoka kwenye mkutano na kupitia moja kwa moja kuangalia afya
yake, atakuwa ametumia takriban siku 11 hadi kufikia leo.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya intaneti, katika mkutano huo
ambao mada kubwa iliyokuwa ikijadiliwa ni masuala ya jinsia, Spika Anne
Makinda, alichangia kuhusu suala hilo akisema wanawake maspika wana jukumu
kubwa la kuhakikisha kwamba mabunge yanazingatia ujinsia.
Akichukulia mfano hatua
ambazo Tanzania imechukua katika kufanikisha masuala ya kijinsia katika Bunge,
Makinda alielezea umuhimu wa maspika wanawake kuhakikisha suala hilo
linafanyika kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kuanzisha kamati ya usawa wa
kijinsia pamoja na suala zima la bajeti sanjari na kuimarisha muundo wa
mabunge.
No comments:
Post a Comment