To Chat with me click here

Wednesday, October 24, 2012

NDEGE YA JESHI YAANGUKA, RUBANI AFARIKI DUNIA


ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kapteni Deogratius Magushi amefariki dunia na mwenzake Kapteni Feruz Kwibika kujeruhiwa vibaya wakati wakijaribu kujiokoa baada ya ndege waliyokuwa wakifanyia mafunzo kupata hitilafu ikiwa angani na kuanguka.

Ndege hiyo ilipata hitilafu jana saa 4.28 asubuhi katika Kambi ya Jeshi la Anga (Air Wing) Ukonga, Dar es Salaam. Mashuhuda waliokuwepo katika eneo la tukio, walisema ajali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya ndege hiyo kupaa na kupoteza mwelekeo kabla ya kuanguka.

Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi, Lugalo. Kanali Mgawe alisema Kapteni Kwibika aliumia vibaya kichwani na amelazwa katika Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), hospitalini hapo.

Alisema kabla ya tukio hilo, marubani hao walikuwa wakijiandaa kurusha ndege hiyo mpya ya mafunzo lakini ikapata hitilafu wakati ikianza kushika kasi.

“Ilishindwa kuruka na ilitakiwa kuanguka katika hanga dogo ambalo lilikuwa na ndege nyingine. Ingekuwa ni hatari zaidi na pengine ingeleta maafa zaidi.”

Kanali Mgawe alisema baada ya marubani hao kuona hatari hiyo, waliamua kuirusha ndege hiyo umbali wa mita 100   hivyo wakapata wasaa wa kutumia parachuti.

Alisema baada ya kutoka katika parachuti hizo Kapteni Mangushi alianguka katika hanga dogo na kufariki papo hapo wakati Kapteni Kwibika aliangukia paa la nyumba na baadaye kuporomoka katika kambi na kuumia kichwa.

“Parachuti la Kapteni Kwibika lilikosa kizuizi na hiyo ndiyo ikawa sababu kubwa ya kuumia kwake,” alisema.

Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange alikuwa mmoja wa viongozi waliofika kushuhudia tukio hilo muda mfupi baada ya kutokea kwake. Hata hivyo, Jenerali Mwamunyange hakuzungumza lolote kuhusiana na ajali hiyo.
Habari zilizopatikana jana jioni zinasema kuwa, ndege hiyo ilipangiwa safari ya kwenda katika Kambi ya Ngerengere Mkoa wa Morogoro na kurudi ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa askari hao.

Itakumbukwa kuwa, Juni 30, 2010 ndege nyingine ya JWTZ ya Kambi ya Ngerengere ilianguka katika eneo la Manga -Kabuku Mkoa wa Tanga. Ndege hiyo iliyokuwa katika mazoezi ya vitendo, ilipata hitilafu hivyo kutua kwa dharura barabarani na kugongana uso kwa uso na basi lililokuwa limebeba watalii.

Ilielezwa kuwa, ndege hiyo ilikuwa imebeba watu watatu, wawili kati yao wakiwa ni marubani na mmoja wao alifariki dunia papo hapo.
Iliripotiwa kuwa hakuna abiria yeyote katika basi hilo la utalii aliyepoteza uhai. Hata hivyo, ndege hiyo ilisababisha kukwama kwa usafiri kwa abiria waliokuwa wanatoka na kuingia kwa kutumia barabara hiyo inayounganisha Mikoa ya Kaskazini na ile ya Pwani na nchi jirani.

No comments:

Post a Comment