Mhe. Zitto Z. Kabwe |
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na mwenzake wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(CHADEMA), wamewaonya viongozi na madiwani wa chama hicho wilayani Karatu kuwa
hawatavumiliwa endapo watashindwa kutatua tatizo la maji wilayani humo.
Vigogo
hao walitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wakiwahutubia wakazi
wa mji wa Karatu wakiwa wameongozana na Mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Israel
Natse, katika mkutano wa kuhamasisha maendeleo pamoja na ushiriki wa wananchi
katika utoaji wa maoni ya Katiba mpya.
Zitto
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, alisema akiwa kama kiongozi wa
chama pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Lissu, wametoa
maagizo kwa viongozi wao wa wilaya chini ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,
Lazaro Maasai, kwenda kuzungumza na wananchi kwenye vijiji ambavyo mradi wa
maji wa Kaviwasu unapita.
Alifafanua
kuwa lengo la kwenda kuzungumza na wananchi hao ni kujua matatizo yaliyopo
ambayo yanasababisha mradi huo kutotoa huduma kwa kiwango kilichokusudiwa na
kuyapatia ufumbuzi mara moja ili watu waendelee kupata maji safi na ya kutosha.
“Naomba
niwambie wazi kama hawatatekeleza maagizo haya tutawafukuza wote kwa kuwa
hatutakubali kuona mradi huo wa maji ulioasisiwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Willibrod Slaa, wakati akiwa mbunge wa jimbo hili unaharibiwa na watu wachache
wenye tamaa ya fedha,’’ alisema.
Aliongeza
kuwa wametembelea maeneo hayo na kukutana na malalamiko mengi juu ya viongozi
kushindwa kusimamia vema majukumu yao na kuwataka wananchi wawaambie viongozi
hao kuwa katika miradi ya maendeleo hakuna siasa na ikibidi wawawajibishe kama
watashindwa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumzia
kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa
serikali, Zitto alisema tayari wana orodha ya Watanzania 27 ambao wanamiliki
mamilioni ya dola nje ya nchi ambayo waliyapata kwa njia zinazotia shaka.
Zitto
alitaja kuwa miongoni watuhumiwa hao yumo ofisa mmoja wa jeshi mstaafu ambaye
hata hivyo hakumtaja jina, akisema anamiliki akaunti nje ya nchi ikiwa na kiasi
cha dola milioni 56.
Aliitaka
serikali iwataje wote wanaomiliki fedha nje na kuchukua hatua haraka,
vinginevyo wao watawaweka hadharani kwa umma ili nguvu ya wananchi ichukue
mkondo.
Naye
Lissu akizungumza katika mkutano huo, aliwaonya wananchi wa Karatu wasikubali
kuanza kurubuniwa kwa kuchukua visenti vidogo vidogo na kuharibu historia yao
nzuri ya mfano kwa nchi hii.
Alisema
vitendo vya kuendekeza njaa katika masuala ya utendaji si desturi na mfumo wa
chama hicho, hivyo kuwatahadharisha wananchi kuwa kama kunatokea kiongozi ama
mwanachama ana matatizo hayo basi hakuna kufichaficha waelezane hadharani.
Kuhusu
utoaji maoni kwenye tume ya Katiba, Lissu aliwaomba wananchi kujitokeza kwa
wingi kama wanavyojitokeza kwenye mikutano ya chama hicho ili kutoa maoni yao.
“Naomba
niwaambie wananchi nyie mna historia kubwa toka nchi inapata uhuru mliishawahi
kuchagua kiongozi bila kupitia chama chochote, Chifu Sarwatt na mkambwaga
mgombea wa TANU lakini leo miaka 50 ya uhuru tunaambiwa bado hatujakomaa kuwa
na wagombea binafsi, kwa kutumia uandikwaji wa Katiba mpya jitokezeni mtoe
maoni yenu,” alisema Lissu.
Alifafanua
kuwa wasipojitokeza kutoa maoni kwa tume hiyo watakuwa wamechangia kuruhusu
watu wachache kuwaandikia Katiba ama vipengele vingi vya Katiba ya zamani
inayolalamikiwa vitabaki vilevile.
No comments:
Post a Comment