To Chat with me click here

Friday, October 12, 2012

NGUVU YA LOWASSA YAMTESA KATIBU CCM

AKUMBWA NA ZOMEAZOMEA, AOMBA RADHI

Mhe. Edward Lowassa
Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, ameendelea kuchafua hali ya hewa katika uchaguzi wa chama hicho baada ya kujkuta akizomewa na wajumbe wa mkutano Mkuu wa Uchaguzi ngazi ya Mkoa.

Chatanda alikutwa na masahibu hayo baada ya kuacha kumtambulisha Mjumbe wa Halamshauri Kuu ya Taifa (Nec) wilaya ya Monduli alikuwa amekaa meza kuu, Edward Lowasa, kama alivyofanya kwa wengine hivyo kujikuta akizomewa na wajumbe.

Tafrani hiyo ilitokea jana majira  ya saa nne, asubuhi kwenye Hoteli ya Naura Spring, ambako CCM waliamua kufanyia uchaguzi wao.

Chatanda katika mkutano huo, alikuwa Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi, akimsaidia Msimamizi Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Jumanne Maghembe.

Baada ya kutambulisha wajumbe wote waliokuwa wamekaa meza kuu, alimruka Lowasa na kujikuta akizomewa na wajumbe wa mkutano huo, ambao walipaza sauti wakitaka mjumbe huyo atambulishwe.

Kutokana na zomea zomea hiyo, Chatanda alilazimika kuomba msamaha na kumtambulisha Mjumbe huyo, hali iliyosababisha ukumbi wote kulipuka kwa shangwe, huku wakiimba “CCM, CCM, CCM” na wengine wakipiga vigelegele na shangwe za Kimasai.

“Wajumbe samahani naomba nimtambulishe Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Lowasa, naomba msamaha jamani,” alisema huku akiirudia rudia kauli hiyo, kwa madai wajumbe wengi wapya hawafahamu majina yao.

Baadhi ya wajumbe walisikika wakisema alifanya hilo kwa makusudi, kutokana na kuangushwa kwa mtandao wake na kujigamba watashinda hata ngazi ya mkoa.

Naye Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo Prof. Maghembe akizungumza katika mkutano huo, aliwaasa wajumbe kuacha kushangilia watu hata kama wanawapenda au kuzomea, ili uchaguzi uwe wa amani.

Alisema hakuna haja ya kuzomea au kupigiana kelele, kwa sababu wote ni wanachama wa chama kimoja na hakuna mpinzani, hivyo lengo ni moja.

“Jamani wajumbe hapa wote ni CCM lengo letu moja, tusizomeane, wala tusipigiane kelele, kwa sababu hapa hakuna wapinzani,” alisema Maghembe.

Maghembe alisema kuwa lengo la uchaguzi ni kuwa kitu kimoja kwa kupata viongozi watakaojenga chama kwa kuvunja makundi na kuunganisha watu pamoja, ili kurudisha viti vya udiwani na ubunge vilivyopotea.

“Msichague viongozi watakaobweteka na kutugawa, hawa hawatufai, tuepuke viongozi wa aina hii, tuchaguwe kiongozi atakayetuunganisha," alisema.

Alisema katika kuhakikisha uchaguzi unaenda kwa amani na kumalizika kwa salama, alilazimika kuomba ulinzi wa kutosha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye alimpatia askari wa kutosha wengine walivalia sare na wengine wakiwa hawana sare.

“Nawaomba wajumbe, Karatu, Ngorongoro, Monduli, Arumeru, Longido na Arusha, tusizomeane humu ndani tu wamoja,” alisisitiza.

Baada ya kueleza hayo waliingia katika hatua ya uchaguzi, ambao  alisema wajumbe wa kupiga kura katika uchaguzi huo wapo 897, lakini waliokuwapo hadi muda wa kupiga kura walikuwa 855.

Lakini kabla ya kwenda katika hatua ya kunadi wagombea, wajumbe walimchagua Lowasa, kuwa Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo na kushangiliwa kwa kishindo.

Wajumbe walianza kwa kuwaruhusu wagombea nafasi ya Mwenyekiti Mkoa, kujinadi ambayo inagombaniwa na wajumbe watatu, ambao ni Onesmo Nangole anayetetea nafasi yake, Dk. Salash Toure na Adamu Chora.

Akijieleza mbele ya wajumbe Nangole alisema kuwa anaomba kura, ili asimamie dosari zilizopo na kushughulika na watu wote wanaoleta makundi ndani ya chama.

“Mimi najua matatizo ya kila mmoja na nitaweza kutatua, naomba mnirudishe jamani, sisi tumegawanyika sana ukianglia kamati zote wilaya hadi mkoa tumegawanyika, nirudisheni niwaunganishe kwa kuwashughulikia wanaotutenganisha,” alisema.

Baada ya kujieleza aliulizwa swali na mjumbe mmoja, kuwa atawezaje kuwarejeshea amani waliyokuwa nayo kama chama tawala kwa kuvaa nguo na kutembea kwa uhuru Arusha, sababu kwa sasa hawana amani.

Naye Dk.Slash Toure akijinadi alisema akichaguliwa atamaliza makundi yaliopo ambayo yameigawa CCM kila ngazi na kuwaomba kuwabwaga waliotumia fedha kuomba uchaguzi huo.

Mgombea wa tatu wa nafasi hiyo, Adamu Chora, alisomba ridhaa kwa kusema yeye peke yake ataweza kuyamaliza makundi yanayoangamiza chama hicho, hadi kikapoteza majimbo.

Mbali na nafasi hizo kugombewa, pia kuna nafasi za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, ambao watatoka wawili kila Wilaya.

Lowasa baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo, aliwashukuru wajumbe wote kwa kuwa na imani naye.

“Wajumbe nimewaelewa na sitawaangusha, nimewaelewa ndugu zangu sitawaangusha, nawashukuru kwa kunishangilia, ila sasa tusishangilie tusije kuharibu utaratibu,” alisema Lowasa.

LOWASSA APIGA VIJEMBE

Lowassa naye kwa upande wake, alimrushia kijembe Katibu wa CCM Mkoa, Chatanda, kuwa hakuridhika na baadhi ya matokeo ya uchaguzi wa chama hicho uliomalizika jana.

Katika vijembe hivyo pia alisema wapinzani wamekuwa wakipata kichwa wanapopita mijini na kupata maandamano lakini alisema CCM ni chama chenye nguvu ya umma.

Alisema hayo baada ya msimamizi wa uchaguzi Profesa Jumanne Maghembe, kumkaribisha kuzungumza akiwa kama mwenyekiti aliyeongoza uchaguzi huo.

“Wapinzani waelewe hapa Arusha hapawezekani, ni pagumu kwao na hiki chama (CCM) kina nguvu ndicho peke yake chenye nguvu ya umma,” alisema.

Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita, CCM mkoani hapa kilipoteza Jimbo la Arusha Mjini, lakini alisema anataka kuwapelekea ujumbe wapinzani kwamba kama uchaguzi utarudiwa sasa, watalichukua jimbo hilo.

“Tumejipanga kuwakabili kama mahakama itaamua uchaguzi urudiwe…nataka niwapelekee ujumbe, walichukua Jimbo la Arusha kutokana na udhaifu uliokuwepo katika mkoa na wilaya, lakini kama utarudiwa tutalichukua jimbo letu,” alisema.

Alisema kwamba wakazi wa Arusha wamechoka na maandamano ya kila wakati yanayosababisha fujo, chokochoko na msongamano wa magari.

“Heshima ya Arusha sasa imekwisha, umekuwa ni mji wa vurugu na chokochoko,” alisema.

Akimpiga dongo Chatanda, Lowassa kwanza alianza kwa kumsifia kuwa ni kada mzuri na amesimamia chaguzi ndani ya mkoa wake vizuri.

Hata hivyo, alizungumzia kitendo cha Chatanda kutomtambulisha kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo jana asubuhi kwamba hakuwa amekielewa iwapo alikifanya kwa makusudi au la.

“Namshukuru Mary kuwa ni kada mzuri, lakini asubuhi alipoacha kunitambulisha nikajiuliza kafanya makusudi au kasahau,” alihoji na wajumbe wakadakia kwa sauti kuwa alifanya kusudi.

Lowassa aliendelea: “Mary ni kada mzuri na amepitia chaguzi nyingi, lakini zipo nyingine ambazo hakuzifurahia sana,” alisema na kufanya wajumbe kulipuka kwa shangwe.

Aliwapongeza wagombea wote kwa ujumla lakini alimtaja kwa jina mgombea wa nafasi ya uenyekiti aliyeshindwa, Adam Chora pamoja na Onesmo Nangole kwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti.

Hata hivyo, hakumtaka mgombea mwingine Dk. Salash Toure ambaye alikuwa akiwania nafasi ya uenyekiti.

Alimtaka mwenyekiti huyo mteule kuwa jasiri na kuacha woga na ikidi achukue maamuzi magumu.

MATOKEO YA UCHAGUZI:

Msimamizi wa Uchaguzi huo, Profesa Maghembe, alimtangaza Onesmo Nangole kuwa amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa mkoa baada ya kupata kura 604 dhidi ya wapinzani wake Adam Chora aliyepata kura 213 na Dk.Toure kwa kupata kura 13.

Alisema kura zote zilizopigwa ni 833 na kura tatu ziliharibika, hivyo kura halali ni 830.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Chora aliahidi kuendelea kushirikiana na mwenyekiti mpya katika shughuli za utekelezaji wa kazi za chama.

Nangole kwa upande wake aliwashukuru wajumbe kwa imani kubwa waliyonayo kwake na akaahidi kufanya vizuri zaidi.

“Hotuba ya Lowassa aliyoitoa sasa hivi nitaifanyia kazi na imenitia moyo sana,” alisema.

Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi Profesa Maghembe alipomwita Dk Toure kuzungumza na wajumbe hao kwa dakika tatu kama walivyofanya wenzake, alikuwa amekwishaondoka ukumbini humo.

No comments:

Post a Comment