VYAMA
vya upinzani vimepinga teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR),
itakayotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga kura vikidai mfumo huo umetumika Zanzibar, lakini
bado una changamoto nyingi.
Hatua
hiyo ilijitokeza jijini Dar es Salaam jana, wakati NEC ilipokutana na viongozi
wa vyama vyote vya siasa, kikiwemo CCM, ili kupeana taarifa kuhusu maandalizi
ya uboreshaji huo utakaoanza Septemba.
Pia,
mkutano huo ulikuwa kwa ajili ya NEC kuwaonyesha viongozi hao jinsi mtambo mpya
utakavyofanya kazi. Lakini ulipofika wakati wa kuonyeshwa mtambo huo, viongozi
wa NEC walidai wako nyuma ya muda.
Uamuzi
huo ulionekana kumkera Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), na
hivyo kuhoji kwanini waliahidi kuwaonyesha mtambo halafu waseme wako
nyuma na muda.
“Mmetuambia
kuwa mtatuonyesha jinsi mtambo huo utakavyofanya kazi, lakini sasa hivi mnasema
muda umeenda, hivyo mtatuonyesha ulivyo tu bila ya kuona utendaji wake wa kazi,
haina maana yoyote, kama hilo limeshindikana ni bora tuendelee na ratiba
zingine,” alisema Lissu na kuungwa mkono na viongozi wengine.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Lissu alisema kuwa bado anaona kuna tatizo na kwamba
kuna maswali mengi ambayo wanajiuliza na hawajapata majibu, hivyo bado
hawajaelewa jinsi mfumo huo utakavyoleta mabadiliko na kuondoa changamoto
zilizopo.
“Wamesema
kitambulisho kitakuwa kina mfano wa kadi ya benki, kama ukikipoteza haupigi
kura? Tume inaandikisha wapiga kura wengi sana na utaratibu wa sasa kama una
kadi unaenda kujiandikisha na ukijiandikisha kwa sababu una kadi, kumbukumbu
zako wanazo.
“Je,
kama ulijiandikisha huna kadi, unaenda kujiandikisha kama mpiga kura mpya
ambaye kumbukumbu zako haziko kwenye tume au unaenda kujiandikisha kama mpiga
kura ambaye kumbukumbu zako ziko kwenye tume, lakini huna ushahidi wa kuwa na
kadi?” alihoji.
Aliongeza
kuwa kitu muhimu kinachohitajika kwanza ni mabadiliko ya sheria, kwamba tatizo
kubwa lililopo mtu hata kama alijiandikisha akapoteza kitambulisho haruhusiwi
kupiga kura, hivyo utaratibu huo hauwezi kuondoa tatizo.
“Namna
ya kuliondoa ni sheria iseme wazi kwamba kama umejiandikisha, picha yako iko
kwenye tume na ipo siku ya uchaguzi kwenye orodha ya kupiga kura, una haki ya
kupiga kura kwani watu wanakufahamu na picha yako ipo,” alisema.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema tume imeeleza
kuhusu mashine hiyo, lakini hawajaambiwa kampuni ambayo imehusika na jinsi gani
inaweza kusimamia ikiwa na uzoefu gani.
Alisema
Zanzibar wanatumia mtambo kama huo, lakini bado kuna matatizo mengi, hivyo
tatizo sio mtambo ila ni utendaji.
Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema bado nchi iko nyuma kiteknolojia,
kwani mtambo huo unatumiwa na nchi za Afrika tu, na kama ungekuwa na ubora
ungetumika pia katika nchi zilizoendelea.
“Bado
sijaona kama matatizo yataisha, nenda nchi zote za Ulaya, mfumo ni mmoja tu,
wanatumia kitambulisho kwa kila kitu, lakini nchi yetu kila kitu kina mfumo wake,”
alisema.
Mapema
katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva,
alisema mfumo wa BVR ni wa kuchukua au kupima taarifa za mtu kibaiolojia au
tabia ya mwanadamu na kuzihifadhi katika kanzi data (Database), kwa ajili ya utambuzi.
Alisema
kwa kutumia mfumo huo, wananchi wote wenye sifa za kuwa wapiga kura na wale
walio na kadi za mpiga kura, watatakiwa kuandikishwa upya.
“Mtakumbuka
kuwa vituo vya uandikishwaji uliopita vimekuwa katika ngazi ya kata, kwa
utaratibu huu vituo vya kujiandikisha vimeongezeka kutoka 24,919 hadi kufikia
40,015 ambavyo vimewekwa katika ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa ili
kuwezesha kuwa karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Kwa
mujibu wa Jaji Lubuva, uchaguzi mkuu wa mwakani kwa mujibu wa Sensa ya 2012,
utakuwa na wapiga kura 23,917,467 baada ya kutoa watu watakaokadiriwa watakuwa
wamefariki.
No comments:
Post a Comment