Mbunge
wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amesema kuwa mgogoro kuhusu eneo la ujenzi wa
Shule ya Sekondari Mburahati umeelekea kupatiwa ufumbuzi ambapo sasa mapendekezo
ni kujenga shule hiyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 katika eneo la wazi
jirani na kituo cha polisi katika kata hiyo hivyo wakazi wanapaswa kutoa maoni
yao iwapo pendekezo hilo ni muafaka.
Aidha,
amewataka wananchi kama ambavyo waliungana pamoja bila kujali vyama vyao katika
kufuatilia suala hilo waelekeze nguvu katika kufuatilia kuhakikisha kwamba
ujenzi wa barabara ya Mburahati mpaka Mabibo NIT iliyoanza kujengwa kwa kiwango
cha lami kwa kusuasua ikiwa imetengewa kiasi cha shilingi milioni 504 kwenye
mwaka wa fedha 2011/2012 unaendelea na kukamilika kwa haraka zaidi kwa
kuongezewa fedha katika mwaka 2012/2013.
Mnyika
aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mburahati
hivi karibuni na kusisitiza kuwa barabara hiyo ina umuhimu wa pekee wakati huu
ambapo barabara ya Morogoro iko katika ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo
Haraka (DART) hivyo barabara hiyo ikikamilika kwa kiwango cha lami ikikamilika
itaweza kuchangia katika kupunguza foleni ikiwa njia mbadala.
Mnyika
alisisitiza kuwa pamoja na wananchi kuchagua wabunge na madiwani bado
wanawajibu wa kutimiza wajibu wa kiraia wa kufuatilia masuala ya msingi ya
maendeleo ili kuhakikisha uwajibikaji.
Alisema
kuwa katika kufanya hivyo, vyama vya siasa navyo vina wajibu wa pekee ndio
maana Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba chama legelege huzaa serikali
legelege hivyo pamoja na ziara za kiserikali anazozifanya jimboni kwa nyakati
mbalimbali amejiunga pia katika ziara ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) jimboni Ubungo ili kukiwezesha chama nacho kutimiza wajibu wake.
Awali
Mnyika alieleza shule ya sekondari ya Mburahati ilianzishwa mwaka 2010 na
kupewa usajili ikitumia madarasa ya kuazima ya shule ya msingi Muungano.
Amesema ulizuka mvutano wa kundi moja likitaka wanafunzi wa shule ya
msingi wasambazwe katika shule jirani za Barafu, Bryson na Mburahati ili shule
hiyo igeuzwe kuwa sekondari huku kundi lingine wananchi wakitaka shule ya
sekondari ijengwe kwenye eneo la wazi lillovamiwa na CCM katika mtaa wa Barafu
au eneo la karibu na kituo cha polisi cha Mburahati.
Mnyika
alisema kuwa kufuatia hali hiyo na baada ya wananchi kumtaka kuingilia katika
katika mkutano alioufanya kata ya Mburahati tarehe 26 Februari 2012 alifanya
hivyo kupitia mikutano ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na hatimaye
akaihoji bungeni kwenye mkutano wa bunge la bajeti uliomalizika mwezi Agosti
2012. Kufuatia kuingilia kati amepewa majibu kuwa sasa ujenzi huo utafanyika
katika eneo la wazi jirani na Kituo cha Polisi Mburahati.
No comments:
Post a Comment