To Chat with me click here

Monday, October 15, 2012

JERRY SILAA: WANANCHI TIMIZENI WAJIBU


Meya wa Manispaa ya Ilala - Jerry Slaa

MEYA wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, amesema wananchi wanatakiwa kutimiza wajibu wao, ili nchi ipate maendeleo kwa haraka.

Amesema kama kila mmoja atatimiza wajibu wake na kuondokana na tabia ya kuitegemea serikali ifanye kila kitu, nchi itapata maendeleo haraka tofauti na inavyotarajiwa.

Silaa alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga maonesho ya kifedha na uwekezaji yaliyokuwa yakizishirikisha taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za kifedha.

“Maonesho haya yamefanyika kwa mara ya kwanza nchini, lakini naamini washiriki wote wamefika hapa kama sehemu ya kila mmoja kutimiza wajibu wake.

“Kila mmoja akitimiza wajibu wake naamini nchi itasonga mbele, kwa hiyo, tuondokane na tabia ya kuitegemea serikali katika kila jambo kwa sababu serikali ina mambo mengi,” alisema Silaa.

Naye Meneja Matukio wa Kampuni ya Neubrand iliyoandaa maonesho hayo, Geofrey Kivamba, alisema waliamua kuandaa maonesho hayo, ili wananchi waweze kujua namna huduma za kifedha zinavyotolewa na kampuni mbalimbali.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetahadharisha wananchi kuhusu uwepo wa simu feki madukani.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala, katika maonesho hayo na kuwataka wananchi kuwa makini pindi wanaponunua simu.

No comments:

Post a Comment