NI ZAINABU VULLU WA VITI MAALUMU
MKOA WA PWANI, NAPE ASEMA UCHUNGUZI DHIDI YAKE BADO UNAENDELEA, ASISITIZA HATA AKISHINDA UCHAGUZI LEO, ANAWEZA
KUENGULIWA
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye. |
BAADA
ya Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Vullu (CCM) kukamatwa kwa tuhuma za rushwa
wiki iliyopita Mjini Kisarawe, Pwani, chama hicho kimesema mbunge huyo anaweza
kuporwa ushindi hata kama atafanikiwa kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Pwani.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa simu kuhusu tuhuma za rushwa dhidi ya mbunge huyo.
Pamoja na mambo mengine, MTANZANIA ilitaka kujua uchunguzi dhidi ya Vullu na wenzake wawili waliokamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kisarawe, umefikia wapi.
“CCM ni chama kinachojiendesha kisheria, hivyo madai yoyote yanayojitokeza ni lazima yafanyiwe uchunguzi. Ingawa kwa sasa nipo nje ya ofisi, lakini najua suala hilo tayari lilishaanza kufanyiwa kazi, kwa sasa sina majibu sahihi kwamba limefikia wapi, ila kwa sababu hiki ni chama kinachojiendesha kwa kanuni na sheria, lolote linalotokea linachunguzwa kwanza na baadaye tunatoa uamuzi.
“Kwa hiyo, kulingana na kanuni za chama, ni kwamba baada ya uchunguzi kukamilika na ikithibitika kwamba madai ya rushwa yaliyotolewa ni ya kweli, basi msimamo wa chama ni kufuta matokeo na uchaguzi utafanyika upya. Niseme tu kwamba, suala lile ni la kisheria, kwa hiyo, lazima lifuate taratibu za kisheria,” alisisitiza Nape.
Kwa mujibu wa Nape, tuhuma dhidi ya mbunge huyo na wenzake wawili siyo ndogo na kwamba uchunguzi wa kina lazima ufanyike ili kupata ukweli halisi wa kilichotokea, ikiwemo kuchukua hatua kwa watuhumiwa.
“Lile siyo suala dogo hata kidogo, kwa hiyo, naamini kabisa tangu liripotiwe, vyombo husika vimeshachukua hatua na hii itafanyika kwa madai yoyote yanayotolewa wakati huu wa uchaguzi ndani ya chama.
“Pia ninachotaka kusema ni kwamba, kwa vile upelelezi wa jambo hilo bado unaendelea, hakuna kanuni zinazozuia uchaguzi kutofanyika, uchaguzi utaendelea kama kawaida na watuhumiwa watashiriki, lakini uchunguzi ukikamilika na kuonyesha kuwa wamehusika na tuhuma za rushwa, chama kitafuta matokeo yao,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi huo wa UWT Mkoa wa Pwani unaotarajiwa kufanyika leo, Katibu wa UWT Mkoa wa Pwani, Sofia Masawe, alisema taratibu za uchaguzi huo zinaendelea vizuri na kwamba utafanyika kama ulivyopangwa.
“Maandalizi yanaendelea vizuri na tutafanya uchaguzi katika ukumbi wa Filbert Bay ulioko Kata ya Mkuza, Pwani, wagombea ni wale wale hakuna mabadiliko, hakuna aliyejitoa wala aliyetolewa.
“Hata hao akina Vullu wapo kwenye uchaguzi kwa sababu hatujapata maelekezo yoyote kutoka juu, sisi tunaendelea na uchaguzi na ikitokea chochote hata baada ya uchaguzi watatujulisha,” alisema Masawe.
Septemba 27 mwaka huu, TAKUKURU, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, ilimtia mbaroni Mbunge Vullu akiwa na wenzake wawili ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Asia Madima na Katibu wa UWT wa wilaya hiyo, Mwajuma Mombwe.
Mbunge huyo na wenzake hao, walikamatwa kwa tuhuma za kugawa fedha kwa wajumbe waliohudhuria kikao cha Baraza la UWT, Wilaya ya Kisarawe, kilichokuwa kikifanyika makao makuu ya CCM, Wilaya ya Kisarawe.
Wakati wa tukio hilo, Vullu, Asia na Mwajuma, walikamatwa na Kamanda wa TAKUKURU, Wilaya ya Kisarawe, aliyetajwa kwa jina moja la Noel.
Kutokana na tuhuma hizo, Vullu na Asia walizungumza na waandishi wa habari na kukiri kwamba walikamatwa na TAKUKURU, ingawa hawakujua ni kwa nini walikamatwa.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM, Wilaya ya Kisarawe, Mbunge Vullu alisema, “Ni kweli TAKUKURU walitukamata mimi na huyu mwenzagu Asia pamoja na Mwajuma.
“Mnajua katika vikao kuna posho zinazotolewa kihalali na ndiyo maana waliokuwa wakipokea hizo Sh 10,000 tulizokuwa tukiwapa, walikuwa wakisaini, jamani haikuwa rushwa hata kidogo, hizo siyo rushwa kwa sababu rushwa mtu hasaini.
“Pia mimi (Vullu) sikukamatwa na fedha zozote, aliyekuwa akigawa fedha ni huyu Asia, yeye ndiye anayejua alizitoa wapi, lakini bado nasema tulikuwa hatutoi rushwa na kwa kuzingatia hilo, hata tulipopelekwa pale ofisi za TAKUKURU tulikataa kujaza fomu alizotupatia yule Noel kwa sababu hatukuwa na kosa.
“Pamoja na hayo, naomba mkamuulize huyo Noel ni kwa nini alikuja kutukamata na ‘gate keeper’ (mlinzi wa getini) anaitwa Kingu, hivi huyo Kingu ni nani hapo, mkamuulize,” alisema Vullu.
Kwa upande wake, Asia alisema wakati anakamatwa alikuwa na burungutu la noti zenye thamani ya Sh 550,000 kwa kuwa baadhi ya wajumbe alikuwa ameshawasainisha kiasi fulani cha fedha.
“Kikao kilikuwa na wajumbe 49 na mhudumu mmoja, kwa hiyo hao TAKUKURU walipofika hapa, walitukamata na wakachukua fedha zangu ambazo baadaye nitazifuatilia ili wanirudishie maana hizo hazikuwa rushwa bali ni posho za kawaida ambazo nimezipata kwa njia halali.
Kwa mujibu wa Asia, maofisa hao wa TAKUKURU, mbali na kuchukua fedha hizo, walichukua pia Katiba ya UWT, walichukua nyaraka za vikao, orodha ya wajumbe waliokuwa wakitakiwa kusaini posho na kitabu cha Kanuni.
Kutokana na tuhuma hizo, siku moja baada ya tukio hilo, Nape aliiambia MTANZANIA kwa simu, kwamba watuhumiwa hao watachunguzwa na Kamati ya Maadili ya chama ili kujua ukweli wa tuhuma dhidi yao.
CHANZO: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment