WAJIBODOA KUIPIKU CCM UCHAGUZI WA MADIWANI
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinatarajiwa kufanya mikutano mikubwa ya
hadhara mkoani Arusha itakayohutubiwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa,
yakiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Oktoba 28
mwaka huu katika kata 29.
Dk.
Slaa atahutubia mkutano wa kwanza kesho mjini Arusha katika viwanja vya Ndarvoi
Kata ya Daraja Mbili na kuzindua rasmi kampeni za udiwani, ukiwa ni mkakati wa
kuinyakua kata hiyo iliyokuwa ikiongozwa na CCM.
Akizungumza
na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mweyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha,
Samson Mwigamba, alisema kuwa tayari maandalizi yote yamekamilika na kwamba wanataka
kutumia uchaguzi huo kuidhihirishia CCM na wapambe wake kuwa kanda hiyo ni
ngome ya CHADEMA.
Mwigamba
alifafanua kuwa Jumapili, Dk. Slaa atahutubia mkutano mwingine katika kata ya
Bangata jimboni Arumeru Magharibi, ambayo nayo ilikuwa ikiongozwa na diwani wa
CCM aliyefariki.
“Tutafanya
kampeni kwa kishindo kikubwa na kwa jinsi hali ilivyo hapa Arusha hakuna kata
ambayo CHADEMA tutashindwa kuichukua. Na CCM katika kuogopa hili wameanza
kutembeza fedha kununua shahada za kupigia kura kwa dau kubwa wakidhani watu wa
hapa wanadanganyika,” alisema.
Hata
hivyo, uchaguzi huo mdogo mjini humo, hautazihusisha kata nne ambazo madiwani
wake walifukuzwa uanachama na CHADEMA na ile moja ya Sombetini ambayo aliyekuwa
diwani wake kupitia CCM, Alphonce Mawazo, alihamia CHADEMA.
Madiwani
hao waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Charles Mpanda (Karoleni), Estomi
Mallah (Kimandolu), John Bayo (Elarai) na Ruben Ngowi (Themi).
“Kata
hizi hazitafanya uchaguzi kwa sasa kwani utakumbuka baada ya madiwani hawa
kufukuzwa walifungua kesi kupinga lakini wameshindwa na taarifa hizo zilikwenda
Tume ya Uchaguzi wakati tarehe ya uchaguzi ikiwa imeshapangwa,” aliongeza
Mwigamba.
Kuhusu
mwenendo mzima wa uchaguzi, mwenyekiti huyo alisema wamejipanga vya kutosha,
hivyo kuwa na matumaini makubwa ya kunyakua kata zote kutoka mikononi mwa CCM.
Alipoulizwa
juu ya operesheni ya Chama cha Wananchi (CUF) maarufu kama Dira ya Mabadiliko
(V4C) iliyofanyika hivi karibuni jijini humo imewaathiri kiasi gani, Mwigamba
alitamba kuwa hawakuathirika kwa lolote kwa vile ilikufa kabla haijaanza.
“Niliwaambia
CUF mapema kwamba ngome yao iko Pemba, hivyo V4C ilipaswa ianzie huko ndipo
waisambaze huku Arusha lakini hawakufanya badala yake wameleta wafuasi kutoka
Dar es Salaam, Tanga na Kilimanjaro ili kuvuta umati wa watu mkutanoni bila
mafanikio,” alisema.
No comments:
Post a Comment