ULINZI MKALI WATANDA, APELEKWA RUMANDE
KIONGOZI
wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kislamu, Sheikh Faridi Hadi Ahmed, na
wenzake sita jana walipandishwa katika Mahakama ya Wilaya Manakwerekwe visiwani
hapa, wakikabiliawa na tuhuma za kufanya uchochezi na kusababisha vurugu.
Mwendesha
Mashtaka wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Maulid Ame,
aliwataja viongozi wengine kuwa ni Sheikh Mselem Ali Mselem (Kwamtipua), Sheikh
Musa Juma Issa (Makadara) na Sheikh Azani Khalid Hamdani (Mfenesini).
Wengine
ni Sheikh Suleiman Juma Suleiman (Makadara), Sheikh Khamis Ali Suleiman
(Mwanakwerekwe) na Hasan Bakari Suleiman mkazi wa Tomondo.
Wote
kwa pamoja walidaiwa kuwa Agosti 17, mwaka huu, majira ya saa 11 jioni huko
kiwanja cha Magogoni Msumbiji katika Wilaya ya Magharibi Unguja wakiwa
wahadhiri kutoka Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya Kiislamu walitoa matamko ya
uchochezi.
Kwamba
maneno hayo yaliashiria uvunjifu wa amani na kusababisha fujo na maafa
mbalimbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Hata
hivyo wakili wa washtakiwa hao, Abdalla Juma, alisema kuwa makosa ya wateja
wake si miongoni mwa yale yanayopaswa kunyimwa dhamana, hivyo aliomba mahakama
kuwapatia dhamana kwa masharti mepesi.
Alisema
kuwa kitendo cha kutaka barua ya sheha na wadhamini ambao ni watumishi wa
serikali kwa ajili ya dhamana ni kuwakwamisha wateja wake kwani watu hao ni
vigumu kuwapata.
Hata
hivyo, mwendesha mashtaka wa serikali hakuwa na pingamizi na ombi la dhamana
hiyo na kusema anaiachia mahakama itoe uamuzi. Naye
hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Ame Msaraka Pinja, alisema wa kuwa dhamana ni
haki yao haitakuwa busara kwa mahakama yake kutoa uamuzi wa haraka wala kuchelewesha
dhamana za washtakiwa hao.
Aliiahirisha
kesi hiyo hadi Oktoba 25 mwaka huu ambapo itakuja kusikizwa uamuzi wa dhamana
zao, na hivyo watuhumiwa wote walirudishwa rumande.
Hata
hivyo, wakati wote kesi hiyo ikiendelea, ulinzi mkali wa polisi ulitanda
kuzunguka mahakama hiyo, huku watu wakizuiwa kuingia ndani.
Sheikh
Faridi na wenzake walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 5:00 asubuhi chini
ya ulinzi mkali wa polisi wenye magari saba aina ya Landrover.
No comments:
Post a Comment