WAZIRI
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameeleza kusikitishwa na kauli za
viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini
(TANESCO) kuhusu hali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini
sanjari na uboreshaji wa utendaji TANESCO.
Amesema
kauli hizo zinatoa matumaini potofu kwa wananchi na kuwasihi kuzipokea kwa
tahadhari kwa kuwa hazielezi ukweli kuhusu tatizo la umeme nchini.
Mnyika
ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake kwa
vyombo vya habari na kusema kulingana na nyaraka alizonazo za ndani ya wizara
hiyo na TANESCO kuanzia Septemba hadi Oktoba mwaka huu, hali ya uzalishaji na
usafirishaji na usambazaji wa umeme imekuwa tete kwa sababu mbalimbali ikiwemo
upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi asili kwa ajili ya uendeshaji wa
mitambo ya kufua umeme na kasi ndogo ya uwekezaji kwa ajili ya kupata ufumbuzi
wa kudumu.
Mnyika
pia alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, ili Wizara ya
Nishati na Madini iwajibike kueleza hali halisi katika mikutano ya kamati za
Bunge inayoendelea.
“Katika
barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la kupokea na kujadili
taarifa ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na utekelezaji wa mpango
wa uboreshaji wa utendaji wa TANESCO lishughulikiwe na kamati nyingine kwa
haraka kwa kuzingatia maelezo na maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati
wa kuahirisha mkutano wa nane wa Bunge,” alisema.
Aidha
alisema mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa shirika
hilo yahusishe kamati ya kudumu ya Bunge na itakayoeleza hatua iliyofikiwa
katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi kwa kuzingatia kuwa siku 60 za uchunguzi
zimepita.
No comments:
Post a Comment