Mhe. Mnyika akifafanunua jambo mjengoni |
WAZIRI
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Spika wa Bunge, Anna
Makinda, kutumia madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya
kudumu ya Bunge itakayoshughulikia masuala ya gesi asili kabla na wakati wa
mkutano wa Bunge ujao mwishoni mwa mwezi huu.
Mnyika
ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo kupitia CHADEMA, alisema hatua hiyo ni kutokana
na hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia
umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema pamoja na mambo
mengine, Spika Makinda aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa ya
utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu sekta ndogo ya gesi asili
ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi.
Madai
mengine ni ya mapunjo ya fedha za mauzo ya gesi asili na hatua iliyofikiwa
katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi asili.
“Hatua
hii ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo kuhusu kauli yangu ya Oktoba 4, 2012 ya kutaka taarifa ya ufafanuzi
kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini iliyotolewa na wizara hiyo
Septemba 21 mwaka huu ifutwe,” alisema.
Alisema
kuwa taarifa hiyo ya wizara ilieleza kuwa maandalizi ya sera ya gesi asili yapo
katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati mbalimbali za kudumu za Bunge
hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu pamoja na kuwa mamlaka ya kutunga
sera kwa mfumo wa sasa ni ya Baraza la Mawaziri.
“Kwa
unyeti na upekee wake sera ya gesi, Spika wa Bunge anapaswa kuwezesha Kamati za
Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo mashauriano na maridhiano kwa mapana na
marefu,” alisema.
Mnyika
alisema izingatiwe kwamba katika mkutano wa nane wa Bunge, Spika alitangaza
kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa na kwamba
majukumu iliyokuwa ikishughulikiwa yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa
mujibu wa madaraka na mamlaka ya spika.
No comments:
Post a Comment