To Chat with me click here

Tuesday, October 23, 2012

DK. SLAA AMKABA JK

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuvunja ukimya wake na kuchukua hatua sahihi kumaliza chokochoko za udini zinazolielemea taifa.

Dk. Slaa alisema kuwa yanayoendelea ndani ya nchi yametengenezwa na watawala wenyewe, hivyo amemtaka Rais Kikwete kujifunza kwa Rais mstaafu Alli Hassan Mwinyi.

Alisema kuwa kiongozi huyo aliweza kuchukua hatua za kitaasisi kumaliza mizozo iliyoanzishwa na makundi ya Wakristo wenye imani kali na Waislamu miaka ya 90, ambayo yalikuwa yakishambuliana kwa mahubiri na hotuba kalikali.

Akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Bugarama, Kahama juzi, Dk. Slaa alisema kuwa hatua hiyo ni moja ya vitu vinavyomfanya Rais Mwinyi akumbukwe na Watanzania.

“Hali ya sasa hivi ni tofauti kwani matatizo yanayoendelea nchini yamezalishwa na viongozi wenyewe, wanaotafuta visingizio vya kuvuruga nchi baada ya kushindwa kuongoza na kuweka fursa za wananchi kujipatia maendeleo,” alisema.

Dk. Slaa aliongeza kuwa yanayoendelea sasa ni kama vile nchi haina kiongozi, haina serikali na hakuna chama kinachoongoza serikali, kwani wote wanaowajibika kukemea na kuchukua hatua sahihi kumaliza tatizo wamekaa kimya.

Alisema kuwa Watanzania wote wema, bila kujali itikadi zao za dini wala siasa, wanaoipenda nchi yao, wanapaswa kupaza sauti zao kabla nchi haijatumbukia katika matatizo.

Kwamba hali hii imetokana na watawala walioko madarakani kuwatumia viongozi wa dini kuwagawanya Watanzania ili wasiwe na muda wa kuhoji masuala ya msingi.

“Sasa tunamtaka Kikwete kama nchi imemshinda atangaze kuwa ameshindwa ili asaidiwe. Na CCM yao hawana tena uwezo wa kuhubiri amani, maana nilishawaambia amani haihubiriwi majukwaani,” alisema.

No comments:

Post a Comment