To Chat with me click here

Wednesday, October 24, 2012

CCM IFANYE NINI ZAIDI TUJUE HAIFAI?

ALIYEPATA kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hayati Horace Kolimba, mwaka 1997 alipata kusema chama hicho kimepoteza dira na mwelekeo.

Kolimba kama walivyo wakosoaji wengine alifanya jinai kwa wasiopenda ukweli kwa kuanika udhaifu huo wakati ambapo chama hicho na wakereketwa wake walikuwa wakiadhimisha miaka 20 tangu kizaliwe.

Kauli ya Kolimba naiita jinai kwa masikio ya wasiopenda ukweli, lakini kwa Mungu alitimiza wajibu wa kusema kile alichokiamini japo wenzake hawakupenda.

Hivyo aliitwa kwenye vikao vikuu ya chama mjini Dodoma kuhojiwa na kwa bahati mbaya akafa akihojiwa.

Wale wachache wanaopenda kukosolewa kwa kusikiliza maneno ya wapinzani wao hata kama hayafurahishi, leo wanamkumbuka Kolimba kama shujaa aliyeandika historia ya kisiasa kufa akitetea kile alichokiamini.

Lakini kwa wapenda sifa kwa mambo yasiyo na tija sasa wanajuta na kutamani laiti wangemsikiliza katibu wao wakayafanyia kazi makosa aliyoyaona, CCM isingefikia hatua hii ya umahututi iliyonao.

Ila kama wasemavyo wahenga: ‘Asiyesikia la mkuu huvunjika guu ama ‘Majuto ni mjukuu’, ndivyo CCM inajuta sasa hivi, dira na mwelekeo alivyosema Kolimba wakamdharau, viongozi wake wanahaha bila mafanikio kuvirejesha.

CCM imekuwa kwenye uchaguzi wake wa ndani na sasa inaelekea kuhitimisha ngazi ya Taifa, huku vituko vya rushwa, makundi ya udini, ukabila na ushirikina yakitawala kila kona.

Swali ambalo mimi na wewe hatuwezi kulijibu ni je kwa vitendo hivi vya rushwa vinavyokithiri ndani ya CCM, uhalali wa chama hichi kuendelea kuiongoza nchi unatoka wapi?

Nani yuko tayari kuongozwa na viongozi wanaonunua kura ili wachaguliwe hata kama hawana sifa. Hawa wakiwa madarakani watatekeleza majukumu gani zaidi ya kutumia muda mwingi kurejesha fedha walizotumia kwenye uchaguzi.

CCM inapisha majina ya watuhumiwa wa rushwa kugombea uongozi ndani ya chama na wakati huo huo wanaendelea kugawa rushwa kuimarisha mitandano yao na hatimaye kuchaguliwa kuwa viongozi, hapa nani wa kumfunga paka kengele?

Laiti wangemsikiliza hayati Kolimba wakati huo, wakajitathimini na kujivua gamaba wakati huo, yasingewakuta haya wanayowakuta wakati wakielekea uzeeni na kupoteza chachu ya ushabiki kwa wafuasi wao.

Sijui tunataka CCM ifanye miujiza gani tujue haifai kuongoza tena nchi zaidi ya kutumia mabavu ya fedha badala ya demokrasia huru ya sanduku la kura?
Nani jasiri leo ndani ya CCM anaweza kuthubutu kukemea rushwa kwa dhati na akasikilizwa.

Wengi tunaowasikia wakijitokeza wanalalamika kuangushwa kwa mazingira ya rushwa wakati hata wao walihonga.

Wana-CCM wakongwe wenye heshima ndani ya chama na wasiopenda rushwa, hawawezi kuthubutu kukemea vitendo hivyo, wanaogopa kuandamwa yasije kuwakuta yaliyomkuta Kolimba endapo watasema ukweli.
Uchaguzi umemalizika na viongozi wamepatikana kwa kishindo, je wana uadilifu kiasi gani mbele ya umma kukabiliana na wapinzani kukitetea chama chao kuwa kimeondokana na rushwa?

Kama hilo ni gumu, tutarajie mwelekeo gani na dira mpya viongozi CCM walioshinda. Je, uchaguzi wao utakuwa na maana yoyote endapo watazidi kuparaganyika kwa makundi ya washindi na washindwa.

Safari ya CCM ni ndefu, wanaoutamani urais 2015 wamekimega chama vipande vipande na kujiwekea mizizi ya makundi ambayo hata mwenyekiti wa sasa hana ubavu ya kuyavunja kirahisi.

Kwenye chama chochote cha siasa hakuna mtu aliye maarufu zaidi ya chama, lakini kwa CCM, Katibu Mkuu aliyepita, Yusuf Makamba, aliwahi kusema zaidi ya mara moja kuwa Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete ni zaidi ya chama.

Kumbe kinachoitesa CCM ya sasa ni umaarufu wa mweyekiti wao, viongozi wengine nao ili waweze kupata wadhifa wa urais wanapaswa wawe maarufu kuliko chama, ndiyo maana tunashuhudia vikumbo visivyokwisha.

Kinachopiganiwa si umakini na udhabiti wa chama bali umaarufu wa mtu na kundi lake. Hicho ni chama cha aina gani, dira yake ni ipi, mwelekeo wake upo wapi. 

Je, alichokisema Kolimba kilikuwa sahihi, mbona hakusikilizwa?
Natamani hayati Kolimba angefufuka kwa muda kidogo akarudia kauli ile ya mwaka 1997 kuwa CCM imepoteza dira na mwelekeo, tuone kama kuna kiongozi atathubutu kubisha.

Wito wangu kwa wanasiasa wa vyama vyote, ni vyema wakajijengea utamaduni wa kusikiliza ushauri wa mzuri wa watu hata wasiyowapenda japo unaweza kuwa mchungu lakini utakuwa na faida baadaye.

Kama CCM wangemsikiliza Kolimba wakati ule, wakaanzisha oparesheni ya kujivua gamba mapema kwa kuziba nyufa na kurejesha misingi yao bila shaka hata vyama vya upinzani visingefurukuta na kuwababaisha kiwango cha sasa. Vinginevyo tuelezwe tunataka CCM ifanye nini tujue haifai. Tafakari!

No comments:

Post a Comment