Mhe. Zitto Zuberi Kabwe |
MWENYEKITI
wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhani Dau,
kutokuwa katibu wa kamati ya ukaguzi wa hesabu za ndani wa shirika hilo.
Zitto
alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salam wakati watendaji wa shirika hilo
walipokuwa katika mahojiano na kamati hiyo na kushauri kutafutwa mtu mwingine
awe katibu wa kamati hiyo.
“Nafikiri
yalikuwa yanafanyika makosa makubwa, mkurugenzi mkuu kuchukua nafasi ya katibu
wa kamati ya hesabu za ndani na kujikagua mwenyewe … sasa ninaagiza kwamba
aondoke ichukuliwe na mfanyakazi mwingine,” alisema Zitto.
Zitto
alisema hakuna sheria na si haki kwa kiongozi yeyote kutumia nafasi yake au
kuchaguliwa kujichunguza, bali kazi hiyo inapaswa kufanywa na wafanyakazi
wengine.
Katika
hatua nyingine, Zitto aliitaka NSSF kuielimisha jamii na kuboresha huduma ya
mafao ya bima ya afya ambayo yalianza miaka michache iliyopita.
Aliwataka
kuwatumia wasanii kuzunguka nchi nzima kutoa elimu ya namna ya kujiunga na
kueleza namna mafao ya afya yanavyotolewa.
Pia,
Zitto aliitaka NSSF kuangalia namna ya kutengeneza kadi za wanachama tegemezi
(watoto), ili kuondoa usumbufu unaojitokeza pale wanapotaka kupatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment