SASA UCHAGUZI MDOGO
WANUKIA SUMBAWANGA
Aeshi Hilaly Khalfan |
KWA
mara nyingine tena, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimegonga mwamba baada ya
Mahakama ya Rufaa Tanzania, kuitupilia mbali rufaa ya aliyekuwa Mbunge wake wa
Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly, aliyevuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya
Sumbawanga Aprili 30, mwaka huu.
Uamuzi
wa kuitupilia mbali rufaa hiyo, umetolewa na jopo la majaji watatu, Januari
Msoffe, Edward Rutakangwa na Engela Kileo, baada ya kubaini kasoro za kisheria.
Hilaly
alivuliwa ubunge na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Sumbawanga, Bethuel Mmila, kutokana na kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea
ubunge kupitia CHADEMA, Nobert Yamsebo.
Hata
hivyo, Mei 28 mwaka huu, Hilaly alikata rufaa namba 55 ya mwaka 2012, dhidi ya
Yamsebo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Justus Kalama na Vitus Kapufi,
akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Rufaa
hiyo imebainika kuwa na dosari kadhaa ambazo zimeishawishi Mahakama ya Rufaa
Tanzania chini ya jopo la majaji hao kuitupilia mbali jana katika uamuzi
uliotolewa jijini Dar es Salaam.
Dosari
hiyo ni kutokuwepo kwa mwenendo wa maombi ya mlalamikaji katika kesi ya msingi
ya kuomba mahakama impangie kiwango cha fedha ambacho alipaswa kulipa kama
amana ya kufungua kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 111 (3) cha Sheria ya
Uchaguzi ya mwaka 2010.
Katika
uamuzi wake uliosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma,
mahakama hiyo ilirejea kifungu cha 111 (3) cha Sheria hiyo ya Uchaguzi.
Kwa
mujibu wa kifungu hicho, Mahakama ilisema kwamba mtu anayefungua kesi ya
uchaguzi, ni lazima awasilishe maombi ili mahakama impangie kiwango cha amana
anachopaswa kulipa ndani ya siku 14 tangu kufungua kesi na kwamba ndani ya siku
14 nyingine tangu siku ya maombi hayo, mahakama hiyo iwe imeshapanga kiwango
hicho.
Majaji
hao waliongeza kuwa, ni muhimu kwa sababu kuu mbili, moja ni kuipa nafasi
mahakama kuona kama maombi yaliwasilishwa ndani ya muda baada ya kesi
kufunguliwa na pili kuona kama maombi hayo yaliamuliwa ndani ya muda tangu
kuwasilishwa.
Kwamba
kwa mujibu wa Kanuni ya 96 (1) na (3) za Kanuni za Mahakama ya Rufani, si
jukumu la upande katika kesi kuamua kuwa nyaraka fulani ni muhimu au si muhimu
katika rufaa, kama wakili wa Hilaly, Rweyongeza alivyodai.
Mbali
ya kanuni hiyo, Mahakama hiyo pia ilirejea katika uamuzi wake katika rufaa
namba 8 ya mwaka 2008, Fedha Fund Limited na wenzake wawili, dhdi ya George
T.Varghese, pamoja na tafsiri ya Kanuni ya 85 (3) ya Kanuni za Mahakama ya
Rufani ya Kenya za mwaka 1979.
"Kutokana
na sababu hizo tulizokwisha kuzieleza hapo juu, tanarudia kusema kwamba
kumbukumbu zinazohusiana na mwenendo wa maombi ya kupangiwa kiwango cha kulipa
kama amana ni nyaraka muhimu katika rufaa.
Kutokuwepo
kwa nyaraka hizo, rufaa haina nguvu chini ya Kanuni ya 96 (1) (k) ya Kanuni za
Mahakama ya Rufani, hivyo rufaa inatupiliwa mbali," lilisema jopo hilo.
Hata
hivyo, mahakama hiyo ilisema kuwa haiwezi kuamua upande wa warufani ulipe
gharama za rufaa hiyo kwa kuwa kasoro zilizosababisha kutupiliwa mbali kwa
rufaa hiyo ziliibuliwa na mahakama yenyewe.
Julai
3, 2012, AG na Kalama, nao walikata rufaa namba 65 ya mwaka 2012 dhidi ya
Yamsebo wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.
Kutokana
na rufaa hizo dhidi yake, Yamsebo kupitia kwa Wakili wake Victor Mkumbe,
aliweka pingamizi la awali (PO) pamoja na mambo mengine akidai kuwa Hilaly
hakuwa amelipia ada ya kufungua rufaa hiyo ya Sh 2000.
Hata
hivyo, siku ambayo Mahakama ya Rufani ilipanga kusikiliza rufaa hiyo, iliamua
kuziunganisha rufaa hizo mbili, ambapo Hilaly aliunganishwa na AG pamoja na
Kalama wakawa waomba rufaa dhidi ya Yamsebo.
Kabla
ya kuanza kusikiliza pingamizi la Yamsebo dhidi ya rufaa ya Hilaly, mahakama
hiyo ilibaini kutokuwepo kwa mwenendo huo wa maombi ya Yamsebo kupangiwa
gharama za kufungulia kesi hiyo ya msingi.
Kutokana
na kasoro hiyo, mahakama ilihoji na kutaka maoni ya mawakili wa pande zote
kuhusiana na kasoro hizo.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Mwema Punzi alijibu kuwa wao walimwandikia barua
Msajili wa Mahakama ya Rufani Kanda ya Sumbawanga kumuomba mwenendo wa kesi
hiyo pamoja na vielelezo vingine na kwamba walipopewa, mwenendo wa maombi ya
gharama za kesi haukuwemo.
Wakili
wa Yamsebo, Mkumbe, alidai kuwa kutokana na kutokuwepo kwa mwenendo huo,
kunaifanya rufaa hiyo iwe batili, na akaiomba mahkama hiyo iitupilie mbali.
Hata
hivyo Wakili wa Hilaly, Richard Rweyongeza, alidai kuwa kukosekana kwa mwenendo
huo hakuwezi kuifanya rufaa hiyo iwe ni batili, badala yake aliiomba mahakama
hiyo itumie mamlaka yake chini ya Kanuni ya 2 ya Kanuni za Mahakama ya Rufani,
ili iweze kuendelea.
Wakili
Rweyongeza aliongeza kwamba hata ikibainika kuwa hizo gharama za kufunulia kesi
hazikulipwa, anayeathirika ni mjibu rufaa, hoja ambayo iliungwa mkono na Wakili
wa Serikali, Punzi.
Katika
kesi hiyo ya msingi namba 01 ya mwaka 2010, Yamsebo alikuwa akipinga ushindi wa
Hilaly, akidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi na
hivyo kusababisha uchaguzi huo kutofanyika kwa haki na uhuru.
Pia,
alikuwa akimtuhumu Hilaly na wafuasi wake kutoa rushwa kwa wapiga kura
mbalimbali ili wamchague.
Tuhuma
nyingine alikuwa akizieleka kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuwa alibadilisha baadhi
ya vituo vya kupigia kura kupelekwa mbali zaidi kati ya kilomita tano hadi
nane, jambo ambalo ilichangia kuathiri matokeo ya uchaguzi huo.
Katika
uamuzi wake, Mahakama Kuu ilikubaliana na baadhi ya hoja zilizotolewa na
mlalamikaji na hatimaye kutengua ushindi wa Hilaly.
Akisoma
hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi Betwell Mmila, alisema kuwa baada ya kupitia hoja
zote, anashawishika kusema kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa si wa haki
na huru.
Jaji
Mmila alieleza kuridhika kuwa kulikwepo na mazingira ya rushwa na kutokuwapo
kwa mazingira huru katika kampeni kwa baadhi ya maeneo.
Katika
uchaguzi huo, Hilaly alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 17,328, huku
Yamsebo akipata kura 17,132.
Kwa uamuzi huo, Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), itapaswa kuitisha upya uchaguzi ndani ya siku 90 ikiwa
Hilaly hatakata tena rufaa kupinga uamuzi huo wa jipo la majaji hao.
No comments:
Post a Comment