Waziri
wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu
Mkuu wa wizara hiyo kuwa lengo la agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26
ya utafutaji mafuta na gesi asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu
katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya
baadaye” kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa
rasilimali za taifa.
Ufafanuzi
uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini unatoa mwanya kwa
mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna madai tuliyotoa toka mwaka 2011
kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi na mwaka huu wa 2012
zimeibuka tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti
zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi asili.
Tafsiri
ya ufafanuzi huo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni
kwamba hata kama mikataba iliyopo ina mapungufu yasiyozingatia maslahi ya
taifa, matokeo ya mapitio hayo hayatarekebisha mikataba iliyopo bali mikataba
ya baadaye.
Taarifa
hiyo ya Katibu Mkuu wa Wizara ni ya kurudi nyuma tofauti na kauli za awali za
Waziri Muhongo zilizokubaliana na madai yetu ya toka mwaka 2011 ndani na nje ya
bunge ikiwemo kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ya kutaka
mikataba yote ipitiwe upya, isiyozingatia maslahi ya taifa ivunjwe au ifanyiwe
marekebisho makubwa na mikataba mipya isiingiwe mpaka kwanza kuwepo sera na
sheria bora zenye kulinda uchumi na usalama wa nchi.
Itakumbukwa
kwamba tarehe 15 Septemba 2012 wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi
ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) Waziri wa Nishati na Madini
aliagiza bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili
ili kujiridhisha endapo maslahi ya taifa yalizingatiwa.
Agizo
hilo la Waziri limeendana na mapendekezo niliyotoa mwaka 2011 ya kutaka mapitio
ya mikataba yote ya mafuta na gesi asili ambapo pamoja na mambo mengine
niliitaka Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake kuacha
kuingia mikataba ya muda mrefu ya utafutaji wa mafuta na gesi asili
katika maeneo mbalimbali nchini yenye mianya ya kuhujumu uchumi wa nchi na haki
za wananchi masuala ambayo yalipingwa na Waziri wa zamani.
Kutokana
na kutozingatiwa kwa mapendekezo hayo tarehe 21 Februari 2012 nilitoa kauli ya
kutaka Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo William Ngeleja kuwajibishwa
kwa kuendelea kuruhusu kusainiwa kwa mikataba bila maagizo ya msingi
kuzingatiwa na kueleza kwa umma sababu za serikali kuendeleza usiri na kuacha
kufanya mapitio ya mikataba mibovu iliyopo.
Nilitoa
kauli hiyo baada ya tarehe 20 Februari 2012 Serikali kusaini mkataba wa
kutafuta mafuta na gesi asili na kampuni ya Swala katika maeneo ya Kilosa
Mkoani Morogoro na Pangani Mkoani Tanga na Januari 2012 Serikali kuweka saini
mikataba na kampuni za kimataifa za Petrobras Tanzania Ltd, Heritage Rukwa
Tanzania Ltd na Motherland Industies Ltd na Oktoba 2011 Serikali kusaini
mikataba mingine na kampuni za Ndovu Resource na Heritage Oil za Uingereza kwa
ajili ya utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi katika kisiwa cha Songosongo na
Ziwa Rukwa huku nchi ikiwa haina mwelekeo sahihi wa sera, sheria, mipango na
usimamizi wa sekta hizo nyeti kwa usalama na uchumi wa nchi na maisha ya
wananchi kwa ujumla.
Waziri
Muhongo na Katibu Mkuu Maswi wanapaswa kuendelea kuonyesha kwa maneno na
matendo tofauti yao na viongozi waliowatangulia katika Wizara ya Nishati na
Madini Waziri Ngeleja na Katibu Mkuu Jairo kwa kutoa ufafanuzi wa ziada na
kuchukua hatua zaidi vinginevyo taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa
tarehe 21 Septemba 2012 itakuwa ni mwendelezo wa kulinda udhaifu wa kimfumo
uliojikita katika Wizara hiyo na serikali kwa ujumla.
Ni
vizuri Waziri na Katibu Mkuu wakaendelea kuzingatia ushauri niliwapa bungeni
kwamba sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na
sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na
kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali wenye dhamana na watendaji wengine na
hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi;
hivyo nguvu zielekezwe katika kurekebisha hali hiyo.
Imetolewa
tarehe 4 Oktoba 2012 na:
John
Mnyika (Mb)
Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini
No comments:
Post a Comment