To Chat with me click here

Tuesday, October 2, 2012

LOWASSA, NGELEJA WANG’ARA


DK. MAHANGA, MASABURI, NGWILIZI WAKWAMA

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amedhihirisha umwamba wake katika siasa za ndani ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo katika nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa kupitia Wilaya ya Monduli.

Wakati Lowassa aking’ara Monduli na kumpiku kigogo mwenzake, Frederick Sumaye, aliyegaragazwa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja naye amechomoza wilayani Sengerema.

Hata hivyo hali si shwari kwa Naibu Waziri, Dk. Makongoro Mahanga, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi na Hassan Ngwilizi, kwani licha ya ukongwe wao ndani ya CCM safari hii kura hazijatosha.

Uchaguzi huo umetawaliwa na vituko vya kila aina ambapo wilayani Kahama wajumbe walijikuta wakishinda na kulala njaa huku wengine wakishikiliwa kwa muda na kuhojiwa kwa tuhuma za rushwa.

Taarifa kutoka Monduli zilisema kuwa Lowassa alijizolea kura 709 katika uchaguzi huo uliofanyika jana na kuwaacha washindani wake, Dk. Suleshi Toure aliyepata kuwa saba na Nanai Taon Konina aliyeambulia kura nne.

Pamoja na Dk. Toure kutangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumpigia debe Konina, bado umoja wao haukuweza kufua dafu kwa Lowassa.
Akijinadi mbele ya wapiga kura waliokuwa wakimshangilia muda wote, Lowassa alijivunia mafanikio makubwa ambayo Wilaya ya Monduli imeyapata katika sekta ya elimu, afya na barabara.

Pia alisema uhai wa chama umekuwa mkubwa tofauti na wilaya nyingine za Mkoa wa Arusha ambazo zimekuwa ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Mtu akiniuliza kwanini nagombea tena nafasi hii ya ujumbe wa NEC, nitamjibu kwa jeuri kwamba nimefanikiwa kuifanya Monduli kuwa moja ya wilaya bora nchini,”' alisema na kushangiliwa.

Wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Ngeleja ameibuka shujaa katika nafasi ya NEC huku aliyekuwa mbunge wa Misungwi, Dalali Shibiliti naye akifanya hivyo wilayani Misungwi.

Ngeleja alijizolea ushindi wilayani Sengerema kwa kupata kura 1,060 na kuwabwaga Joah Kasika (317), Philemon Lugumiliza (132) na Renatus Nchali (11).

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Jaji Tasinga, aliangushwa na Chasama Makata aliyepata kuwa 888, huku yeye akiambulia kura 661 na Palelia Ngotezi alipata kura sita tu.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa waliochaguliwa ni Joseph Yared, Julius Butogwa, George Kazungu, Ahmed Jaha na Zena Mbisu, huku nafasi ya Katibu wa Uchumi ikitwaliwa na Onesmo Mashili, Katibu wa Uenezi na Itikadi ilikwenda kwa Masumbuko Bihemo.

Wilayani Misungwi, Shibiliti alishinda ujumbe wa NEC kwa kura 667 na kuwabwaga Alexender Mnyeti (457) na Mwamba Makune (14).

Nafasi ya mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, ilichukuliwa na Judith Mlolwa aliyepata kura 574 huku aliyekuwa mwenyekiti, Daud Samwel Gambadu akipata kura 420.

Wajumbe watano wa mkutano mkuu wa taifa, waliochaguliwa ni Amina Ali Juma (425), Daud Katambi (532), Medadi Mwijage (437), Musa Mnyeti (655) na Mwamba Makune (777).

Mahanga, Masaburi nje
Jijini Dar es Salaam katika Wilaya ya Ilala, vigogo wawili, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga na Meya wa Jiji hilo, Dk. Didas Masaburi, nao wameonja joto ya jiwe baada ya kutupwa nje ya ulingo na wapinzani wao.

Dk. Mahanga ambaye alikuwa akiwania nafasi ya ujumbe wa NEC Taifa, alidondoshwa na mpinzani wake, Ramish Patel, aliyeibuka na kura 664 dhidi ya kura 411 za naibu waziri huyo, huku wakifuatiwa na Simba Ulanga (135) na Seleman Ditopile.

Katika nafasi ya wajumbe watano wa mkutano mkuu taifa, Meya Masaburi alishika nafasi ya saba akiwa na kura 418 hivyo kupigwa kikumbo na Athuman Chilu (689), Aisha Sululu (635), Bona Kiruwa (516), Yona Mwansuku (461) na Ramish Patel (442).

Nako mkoani Tanga, waziri wa zamani na mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi, naye amekula mweleka katika nafasi ya ujumbe wa NEC Taifa.

No comments:

Post a Comment