To Chat with me click here

Thursday, December 27, 2012

BAVICHA KUWATIMUA VIONGOZI WASIO NA NIDHAMU

BARAZA la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limesema limewagundua wanachama na baadhi ya viongozi ambao ni ‘virusi’ na litaanza operesheni nchi nzima ya kuwachukulia hatua za kinidhamu. 

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratus Munishi, alisema hawapo tayari kulea kirusi ndani ya chama ambacho kipo kwa maslahi ya chama kingine na kuongeza kuwa, wameagiza kwa viongozi kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya kuwadhibiti.

“Kuna uvumi umekuwa ukienezwa kwamba ndani ya Bavicha Taifa kuna mgogoro, hili si kweli kwani viongozi wote wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na tupo tayari kumfukuza mtu yeyote yule anayekwenda kinyume na malengo, dhima na dira yetu.

“Kama tunavyofahamu Bavicha ndio nguzo kubwa ndani ya Chadema, kwani vijana wengi Tanzania ni wanachama wetu, hii inatokana na sera yetu ya kupigania ajira, mfumo wa elimu na matatizo yanayowakabili wananchi wote.

“Kuendeleza Bavicha tunataka kuisafisha kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu ila hatua zetu hatuzichukui katika majukwaa tutafanya vikao vya kisheria dhidi yao, tunaomba kama mtu anajijua ni kirusi ajiondokee mapema kabla ya kukumbwa na fagio linalokuja.

“Tumekwisha fahamu kwamba wanafadhiliwa na CCM kwa kuanzisha chokochoko zisizo na maana ikiwamo ya Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa kumiliki kadi mbili.

“Tunawaomba vijana wote nchini watambue kwamba Bavicha makao makuu hatupo tayari kuona chama kinaingia kwenye migogoro, kutokana na watu wachache, tunachotaka kila mmoja lazima awe na uzalendo, uwajibikaji, utu na ubunifu ndani ya chama vinginevyo huyo hatufai,” alisema Munishi.

Aliwataka vijana kupuuza propaganda zinazoendelea kuenezwa juu ya Dk. Slaa kumiliki kadi ya CCM kwa kuwa haina tija.

No comments:

Post a Comment