Mtunzaji wa Mbwa Mwitu akiandaa mlo wa mwisho kwa
wanyama hao 11 kabla hawajarejeshwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti 30,
2012 baada ya kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi huo,
katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
mkoani Mara.
Mbwa
mwitu hao wakijipatia mlo wao wa mwisho kabla ya kuachiliwa huru
Ni vuta nikuvute
Si ugomvi bali ni
namna yao ya kupata mlo
Mkuu wa
Vodacom Foundation Bw Yesaya Mwakifulefule akiangalia
Mbwa Mwitu
hao wakijipatia mlo wa mwisho
Hatimaye Mbwa Mwitu
hao wakiondoka bomani na kuingia mbugani wakiwa wanyama huru baada ya
kuhifadhiwa kwa mwaka mmoja katika boma hilo la mradi wa kuhifadhi mbwa
mwitu katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mradi unaojulikana
kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project
Rais Jakaya Mrisho
Kikwete akimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom hapa nchini Bw.
Rene Meza, Ikulu Dar-Es-Salaam, walipokutana jana jioni, Ijumaa
Agosti 31,2012 kwa mchango wa kampuni hiyo ya simu za mkononi
katika mradi wa kuhifadhi mbwa mwitu katika hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, (Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project),
ambayo ilichanga dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
=============================================
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru
kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kwa kuchangia katika mradi wa kuhifadhi
mbwa mwitu katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mradi unaojulikana
kama Vodacom Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project, kwa
dola za Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Rais ametoa shukrani hizo Kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom hapa nchini Bw. Rene Meza, Ikulu
Dar-Es-Salaam, walipokutana jana jioni, Ijumaa Agosti 31,2012
”Napenda kutoa shukrani zangu kwa
Vodacom kwa msaada huu mkubwa, tunashukuru kwa jitihada zenu kubwa katika hili”
Rais amesema.
Naye Mtendaji Mkuu wa Vodacom
amemhakikishia Rais kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na serikali
katika miradi mbalimbali ya maendeleo, elimu na Afya.
“Tunajisikia faraja sana kuwa miongoni
mwa washirika wa mradi huu. Ni heshima kwetu na tuko makini nao, tunataka
kuendelea na mradi huu” Bw, Rene Meza amemhakikishia Rais.
Tayari mbwa mwitu kumi na Moja,
wamerudishwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012 baada ya
kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi huo, katika eneo la
Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
Wadau wengine walioshiriki na
kufanikisha zoezi hilo ni pamoja na Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Frankfurt
Zoological Society , Grumeti Fund na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kuachiwa kwa Mbwa Mwitu hao 11
walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani Loliondo ni mojawapo ya juhudi
za kurudisha tena makundi ya wanyama hao katika mbuga hiyo maarufu duniani.
Hivi sasa kuna makundi 11 yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu
katika Hifadhi ya Ngorongoro, yakifanya jumla ya Mbwa Mwitu 200.
Mtafiti wa Magonjwa ya Wanyama kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Wanyama (TAWIRI) Dkt. Ernest Mjingo, alimwambia Rais
Kikwete kwamba katika Hifadhi ya Serengeti makundi ya Mbwa Mwitu yalikuwa
yakionekana kwa wingi, lakini sasa yametoweka na mara ya mwisho Mbwa Mwitu
wawili walionekana mwaka 1998.
Mtafiti huyo alisema Mbwa
Mwitu wamekuwa wakitoweka kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula
mifugo yao na kuugua magonjwa mbalimbali kama kichaa cha mbwa.
Dkt. Mjingo alisema baada ya kuachiwa
Mbwa Mwitu hao, waliovishwa collar maalumu zenye redio, juhudi zitaendelea
ili kupata makundi sita yenye Mbwa Mwitu takriban kumi kila moja, ikiwa ni
hatua endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha uwepo wa wanyama hao mbugani
humo.
Mbwa Mwitu ni miongoni mwa wanyamapori
ambao wapo hatarini kutoweka duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa katika
Bara la Afrika kuna Mbwa Mwitu wanaofikia 8,000 na Tanzania pekee inakadiriwa
kuwa wanyama hao 3,500 katika mbuga mbalimbali nchini. Katika Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti walitoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha
kuanza.
No comments:
Post a Comment