ADAI
NI MNAFIKI, MWONGO, NI KUTOKANA NA KAULI YAKE KWAMBA CHADEMA HAKINA
VIONGOZI
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta ni mtu hatari ambaye
CHADEMA kimegundua kuwa anaweza kufanya lolote kupata madaraka.
Dk.
Slaa alisema Sitta hatakiwi kuaminiwa kwa kuwa hata alipokuwa spika, huku akiwa
mwana CCM, mara kadhaa alijaribu kuomba kujiunga na CHADEMA iwapo CCM
ingemtosa.
“Huyu
mtu haaminiki hata katika dhamira yake, kwa kuwa tulikutana zaidi ya mara 100
na hata tukawa tunaandikiana vimemo, yeye akiwa katika kiti cha spika. Kama
anabisha leo akanushe juu ya uhaini wake dhidi ya CCM,” alisisitiza Dk. Slaa.
Dk.
Slaa alitoa kauli hiyo jana mjini Iringa wakati akizungumza na waandishi wa
habari, akijibu kauli iliyotolewa na Sitta aliyedai kwamba CHADEMA
hakijastahili kupewa madaraka kwa kuwa hakina watu wenye uzoefu wa uongozi.
Sitta
alidai mwenye uzoefu wa uongozi ndani ya CHADEMA ni Dk. Slaa pekee; akashutumu
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwamba uzoefu pekee alionao ni kuongoza
kumbi za disko.
Sitta
ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), na ambaye yumo katika fitina za
kimakundi ya wanaoutaka urais ndani ya CCM, alisema hayo mjini Karagwe wiki
hii, kama njia ya kijikweza mbele ya umma; na kuwashusha viongozi wa CHADEMA,
ambacho chini ya uongozi wa Mbowe kimejengeka kuwa chama kikuu cha upinzani
kinachotishia kuiondoa CCM madarakani.
Akijibu
hoja hiyo, Dk. Slaa alidai kuwa mara kadhaa walizokutana, Sitta akiwa Spika wa
Bunge alimweleza kuwa ana kundi la wabunge 55 waliokuwa tayari kuondoka katika
CCM, na kwamba wangefanya hivyo siku tatu kabla ya Bunge la mwaka 2010
kumalizika.
Aliongeza
kuwa, ukigeugeu wa Sitta, haukuishia baada ya uchaguzi, bali hata wakati wa
mchakato wa kumpata spika ambapo baada ya kutoswa na CCM, alihangaika kuwapigia
simu viongozi wa CHADEMA akiwaomba wampe nafasi ya kugombea nafasi hiyo kupitia
chama chao.
“Alikuwa
akinipigia simu saa sita usiku baada ya kutoswa na CCM na kwa bahati mbaya simu
yangu ilikuwa ‘silence’, lakini saa 12 asubuhi nikapokea simu ya mke wake,
Magreth Sitta akiniambia ‘Dk. baba anataka kuongea na wewe na anakutafuta
kuanzia usiku’,” alisema.
Aliongeza
kuwa, wakati alipopokea simu ya Sitta, jambo la kwanza aliomba amzuie Mabere
Marando kugombea uspika ili agombee yeye na kwamba, angeitisha mkutano na
waandishi wa habari kwa ajili ya kutangaza kujiondoa CCM kwa kuwa ametoswa
kwenye uspika.
Dk.
Slaa alisema, katika hali ya kushangaza na inayoonesha kuwa kiongozi huyo ni
mtu wa kuogopwa, wakati wakijiandaa kukutana na waandishi wa habari kwa nia ya
kutangaza kujiondoa CCM, Sitta alimueleza kuwa amepigiwa simu kutoka kwa
wakubwa akiahidiwa kupewa nafasi ya unaibu waziri ambayo hata hivyo, alidai
hakubaliani nayo.
Alisema,
wakati alipoambiwa hivyo na Sitta kuwa hakubaliani na nafasi ya unaibu waziri,
akaanza kupata shaka ya kama anaweza kuwatumikia Watanzania kiuadilifu kwa kuwa
alionesha dalili kuwa anachowaza ni nafasi ya juu zaidi badala ya kuwatumikia
watu.
Aliongeza
kuwa, mwaka 2010 Sitta akiwa na Dk. Harrison Mwakyembe pamoja na Fred Mpendazoe
wakiwa ni waanzilishi wa Chama cha CCJ, walikutana na viongozi wa CHADEMA
katika ofisi za spika mjini Dodoma na akawaeleza kuwa wanaanzisha chama hicho
na ikishindikana watahamia CHADEMA.
Alibainisha
kuwa, baada ya kukubaliana na kuiangalia katiba ya CCJ na kubaini kuwa ilikuwa
inalingana na ya kwao, wakakubaliana Sitta awe mgombea urais kupitia CHADEMA.
Dk.
Slaa alisema, hata hivyo Sitta akawageuka wenzake na akaendelea kubakia CCM. Alizidi
kumshambulia Sitta kuwa ni mtu asiye na uadilifu unaoweza kulingana hata na
kiongozi wa ngazi ya kata wa CHADEMA kwa kuwa ndiye aliyekuwa kinara wa kuzuia
hoja mbalimbali za ufisadi zilizotolewa na wabunge wa upinzani kwa sababu ya
kuilinda Serikali ya CCM.
“Mnakumbuka
hoja ya Buzwagi aliyoitoa Zitto kuwa waziri amesema uongo kwa kulidanganya
Bunge, yeye akapindua kuwa ni hoja ya Zitto na wakamtoa nje ya Bunge kwa miezi
minne, kisha wakamrudisha kinyemela baada ya mwezi mmoja na Sitta alishupalia
kuzima hiyo hoja?” alihoji Dk. Slaa.
Alisema,
Sitta ndiye spika aliyezuia hoja ya ufisadi wa BoT ya EPA licha ya kujua ukweli
wa nyaraka zilizotolewa kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Akizungumzia
kauli ya Sitta aliyedai kuwa Mbowe ni muongoza disko, hivyo hafai kuwa
kiongozi, Dk. Slaa alisema Sitta kama mwanasheria na waziri aliyepewa fadhila
ya kuongoza wizara, anazidi kuiaibisha serikali kwa kuwa mamlaka na leseni ya
kuendeshea kumbi za starehe zinatolewa na Serikali ya CCM.
Alisema
katika hali ya kawaida, Sitta amewatukana vijana na wapiga kura waliomchagua
kwa kuona kitendo cha kuwepo kwa kumbi za disko ni uhalifu.
Dk.
Slaa alisema CHADEMA ina utaratibu wa kupata viongozi na ndiyo maana alipoogopa
kwa mara ya kwanza kujiunga na CHADEMA, zilifanyika taratibu nyingine za kuteua
mgombea na chama kikazidi kufanikiwa.
Alisema
Sitta hakumbuki hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakati alipopata uongozi
hakuwa na wazoefu wa nchi bali aliendelea kuwatumia watendaji wa serikali ya
kikoloni ambao walilazimika kufuata maagizo ya Serikali ya Tanganyika.
“Hakuna
chuo cha uongozi na sisi hatuna ugomvi na watendaji wa serikali, bali
tutawataka wawajibike kwa nafasi zao. Siasa na utendaji wa serikali tutaweka
mbalimbali na atakayeshindwa kasi hiyo atakaa pembeni,” alisema Dk. Slaa.
Waraka mchafu wasambazwa
Katika
hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed,
amewataka Waislamu nchini kutopumbazwa na ujumbe wa simu unaosambazwa na watu
ukilenga kuwachonganisha na chama hicho.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Iringa, Issa Mohamed alisema kuna kundi la
watu kwa sababu wanazozijua wenyewe wameamua kusambaza ujumbe wenye lengo la
kuichafua CHADEMA, huku wakijua huo ni uchochezi wa kidini.
Ujumbe
huo ambao Tanzania Daima imeuona umeandikwa; “Wapendwa katika bwana tumejipanga
vyema kuchukua nchi 2015, Haleluyaa. Operesheni vua gamba vaa gwanda itasaidia
kuwatia mkononi Waislam. Uingereza na Ujerumani zimeahidi kuwapa vijana wetu
mafunzo ya uongozi na ya kivita, tusiache maandamano kwani yanajenga chama
zaidi, mawakala wetu waliomo ndani ya CCM na CUF wanafanya kazi vyema
tuliyowatuma, vyombo vya habari vimeahidi kutubeba hadi kieleweke, watangazie
waumini wetu kuwa ule mpango wa KICHUNGAJI unaendelea vyema kafiri kakosea
namba sambaza ujumbe huu kwa Waislamu tujipange.”
Issa
alisema kwa sababu ya tishio, Serikali ya CCM na wapambe wake wameogopeshwa na
nguvu ya CHADEMA katika mikoa wanayopita, hivyo wameamua kubuni mbinu za
kuwachonganisha na wananchi pasipo kujua hali hiyo inaliangamiza taifa.
Alivitaka
vyombo vya usalama kuacha ushabiki wa kisiasa na badala yake vifuatilie hiyo
meseji kwa kuwa ni sawa na uchochezi mwingine. Kiongozi
huyo aliwataka Waislamu kuzifanyia utafiti kila taarifa watazopewa ili wasije
wakajuta baadae.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Operesheni Sangara katika ziara ya CHADEMA maarufu kama M4C
inayoendelea, Benson Kigaila amesema kitendo cha serikali kuwaomba wasimame
kupisha zoezi la sensa kimekuwa na manufaa kwao kwa kuwa wameweza kufanya kazi
kubwa ambayo wasingeweza kama wangeendelea na ratiba yao.
Alisema
wamefika katika kata 46 za majimbo ya Iringa mjini, Mufindi Kusini na Kaskazini
na kutembelea zaidi ya vijiji 200 kwa ajili ya mikutano ya ndani na kukutana na
wanachama.
“Hawa
polisi na CCM ni makatibu uenezi wetu wametusaidia sana katika kutuomba
tusimame kazi tuliyofanya, hakika watajuta kwanini walibuni mchezo wao huo,”
alisema Kigaila.
No comments:
Post a Comment