DK. KIGWANGALA, BASHE
WATISHIANA BASTOLA NZEGA
KATIKA
kile kinachoonekana kama vita ya urais wa mwaka 2015, makundi yanayokinzana
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yamedaiwa kuanza mkakati wa kujiimarisha
kwa kutumia uchaguzi wa ndani unaoendelea sasa.
Hatua
hiyo vile vile inaelezwa kuwa ni mwendelezo wa visasi vya Uchaguzi Mkuu uliopita
katika baadhi ya maeneo, ambapo wagombea wanaokubalika waliachwa na kuchukuliwa
wengine.
Mathalani
katika Jimbo la Nzega, mkoani Tabora, visasi hivyo vimedumu baina ya Mbunge wa
sasa, Dk. Hamis Kigwangala na kada aliyeenguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa,
Hussein Bashe, akidaiwa si raia wa Tanzania.
Wawili
hawa juzi wanadaiwa kutishiana bastola katika ofisi ya CCM wilayani humo wakati
wakirejesha fomu za kuomba kuwania nafasi mbalimbali.
Taarifa
kutoka vyanzo vyetu vya ndani ya chama hicho, zinaeleza kuwa miongoni mwa
vigogo wanaotajwa kuutaka urais, makundi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa na lile la Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ndiyo yanamsuguano
mkali.
Wakati
uchaguzi wa ndani wa CCM ukizidi kupamba moto, makundi hayo yanadaiwa kuwa kila
moja linahaha kuhakikisha wale wanaoliunga mkono wanaibuka kidedea katika
nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu, Mkutano Mkuu na jumuiya za Wanawake,
Wazazi na Vijana kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.
Tanzania
Daima limedokezwa kuwa katika kuweka mambo sawa, mmoja wa vigogo hao amebaini
kutoungwa mkono na wenyeviti wanaomaliza muda wao katika mikoa ya Shinyanga,
Mwanza, Dar es Salaam na Arusha, hivyo amesuka mkakati ili wasichaguliwe tena.
“Mkakati
huu mchafu na hatari kwa ustawi wa demokrasia unatumia mamilioni ya fedha,
maarufu kama ‘mamilioni ya Gadaffi’ na unaratibiwa na mmoja wa vigogo
anayetajwa kuwa na lengo la kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM,” kilisema
chanzo chetu.
Mabilioni
hayo ya fedha yanadaiwa kuanza kumwagwa katika mikoa husika ikiwa ni lengo la
kuhakikisha wenyeviti hao, Clement Mabina (Mwanza), Hamis Mgeja (Shinyanga),
John Guninita (Dar es Salaam) na Ole Nangole wa Arusha hawarudi tena katika
nafasi zao.
Baadhi
ya makada wa CCM waliozungumza na gazeti hili, wamewaomba wenyeviti wastaafu wa
chama hicho, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kuingilia kati na kumsadia
Rais Jakaya Kikwete kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi.
“Ili
kuinusuru CCM katika anguko la kihistoria, tunawaomba sana Mwinyi na Mkapa
waingilie kati kuhakikisha wanadhibiti kabisa matumizi ya fedha katika chaguzi
zote za ndani,” alisema kada mmoja.
Chanzo
chetu kimebaini kuwa kundi hilo limeanza kujipenyeza mikoani kuwachafua
viongozi wa CCM wasiofungamana nao, hivyo kuandaa safu yao mpya.
Kigwangala vs Bashe
Kuhusu
wawili hawa wanaowania ujumbe wa NEC Wilaya ya Nzega, taarifa zinasema kuwa
tukio hilo la aibu lilitokea katika ofisi za CCM saa 09:30 alasiri baada ya Dk.
Kigwangala kumwambia Katibu wa wa chama wa Wilaya, Kajoro Vyohoroka, asiipokee
fomu ya Bashe kwani alikuwa amechelewa kuijaza na kuirejesha.
Tanzania
Daima lilitonywa kuwa baada ya Dk. Kigwangala kumwambia katibu maneno hayo,
Bashe akatoa lugha ya matusi kwa mbunge huyo.
“Kufuatia
matusi hayo, Dk. Kigwangala alinyanyuka ghafla na kutaka kumpiga Bashe huku
akimtishia kumtandika bastola...lakini baadhi ya wanachama wakawaamulia,”
kilisema chanzo chetu.
Katibu
wa CCM wa Wilaya ya Nzega, Vyohoroka, alikiri kutokea kwa tukio hilo ofisini
kwake juzi na kwamba awali Dk. Kigwangala alikuwa akijaza fomu hiyo ofisini
hapo na Bashe alikuwa ofisini kwa Mwenyekiti, Francis Shija.
Alifafanua
kuwa Bashe alirejesha fomu saa 09:50 na Dk. Kigwangala naye alirejesha saa
09:48 lakini kwa mshangao mbunge huyo alitamka kuwa fomu ya Bashe imechelewa
hivyo isipokewe.
Alisema
kuwa baada ya hapo ndipo maneno makali yalipoanza hadi kufikia vitisho vya
silaha.
Bashe
alizungumza na gazeti hili akisema kuwa Dk. Kigwangala alimtishia kwa bastola
akidai fomu yake isipokewe kwani muda wa kurejesha ulikuwa umekwisha.
“Si
kweli kuwa muda ulikuwa umeisha, bali huyu ndugu yangu ana visa na chuki dhidi
yangu, ni kweli alichomoa bastola yake lakini wanachama walituamua,” alisema
Bashe.
Naye
Dk. Kigwangala alikanusha akisema hakuna kitu cha namna hiyo, bali Bashe ni
mzushi anayetaka kuyakuza mambo hayo.
“Si
kweli na hamna kitu cha namna hiyo…Bashe anataka kuyakuza tu, ni kweli katibu
amembeba muda wa kurejesha fomu ulikuwa umekwisha,” alisisitiza.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, aliliambia gazeti hili kuwa taarifa
za tukio hilo anazo lakini atafuatilia kujua chanzo.
Arusha waenguana
Mizengwe
ya uchaguzi wa ndani ya CCM imeanza mkoani Arusha ambapo Halmashauri Kuu (NEC)
ya mkoa huo, imepinga uteuzi wa wagombea wa nafasi za uongozi wa jumuiya
katika wilaya tatu.
Wilaya
hizo ni pamoja na Monduli, kwa madai kuwa waliopitishwa ni watiifu wa kundi
fulani la kisiasa ndani ya chama mkoa.
Akizungumzia
uamuzi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, alisema kwa Monduli
NEC imeukataa uteuzi wa wagombea wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM).
Alisema
Wilaya ya Longido na Karatu, NEC imeukataa uteuzi wa wagombea wa nafasi za
Jumuiya ya Wazazi kutokana na sababu za mgawanyiko wa makundi.
Kufuatia
kasoro hizo, kikao hicho kimeagiza vikao husika vya uteuzi katika wilaya hizo
kupitia upya na kuzirekebisha ndani ya wiki moja na kisha kukabidhi mapendekezo
hayo kwa kamati ya siasa ya mkoa.
Chatanda
aliongeza kuwa kikao hicho pia kilipitisha majina ya wagombea watano wa nafasi
ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, ambao ni Dk. Salash Toure, Hamis Shaaban,
Onesmo Metili, Adam Chora na anayetetea nafasi yake, Onesmo Nangole.
Dodoma watishana
Mkoani
Dodoma, wagombea wameanza kutishia kuburuzana katika kamati za nidhamu kutokana
na baadhi yao kudaiwa kukiuka taratibu za uchaguzi.
Mbunge
wa Afrika Mashariki, Adam Kimbisa, ambaye pia ni mgombea uenyekiti wa mkoa,
alisema kuwa ikithibitika kwamba wajumbe wawili wa Kamati ya Siasa ya mkoa,
walimsindikiza mwenyekiti anayemaliza muda wake, William Kusila, kuchukua fomu,
atawashtaki katika vikao vya juu.
Akizungumza
na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Kimbisa alisema kitendo cha
kuonesha kumuunga mkono mmoja wa wagombea wakati wao ni watoa maamuzi katika
kikao kinachowachuja, ni kumbeba.
Kauli
hiyo inakuja siku moja baada ya Katibu Mwenezi wa chama hicho, mkoani hapa,
Donald Mejetii, kusema kuwa wajumbe hao wamevunja kanuni na taratibu za
uchaguzi kwa makusudi kwa kuwasindikiza wagombea kuchukua fomu.
Naye
Mbunge wa Chilonwa, Ezekiah Chibulunje, alijitetea kuwa hakumsindikiza Kusila
kama kiongozi bali kama ndugu yake.
Katibu
wa CCM wa Mkoa wa Dodoma , Albert Mgumba, alipoulizwa juu ya sakata hilo,
alisema halina umuhimu wowote kwani ni la kawaida.
Diallo amvaa Mabina
Katika
Mkoa wa Mwanza, jumla ya wanachama 53 walijitokeza kuwania nafasi mbalimbali,
huku mchuano mkali kwenye nafasi ya uenyekiti ukiwa baina ya mwenyekiti
anayemaliza muda wake, Clement Mabina na mbunge wa zamani wa Ilemela, Anthony
Diallo.
Katibu
wa CCM mkoani hapa, Joyce Masunga, alisema kuwa nafasi ya uenyekiti wa mkoa
wameomba wanachama 23 waliochukua na kurejesha fomu hadi siku ya mwisho.
Aliwataja
baadhi ya wanachama hao kuwa ni Mabina, Diallo, Evanus Laurian, Theodora Ihuya,
Barnabas Mathayo, Alfred Wambura na Zebedayo Athumani.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment