To Chat with me click here

Monday, August 6, 2012

LEMA AIPELEKA CHADEMA LONDON

M4C LONDON.


ALIYEKUWA Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amepeleka harakati za Movement For Change (M4C) zinazoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nchini Uingereza.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka London Uingereza, Lema alisema kuwa moja ya shughuli atakazofanya akiwa huko ni kufungua matawi ya CHADEMA.
“Nilipofika tu Watanzania wengi wanaoishi hapa walionyesha nia ya kutaka kuwa na tawi katika jiji la London na tutakuwa na mikutano kadhaa ya ndani ya kubadilishana mawazo,” alisema Lema.

Lema ambaye amepata kuwa mbunge machachari ndani ya Bunge la Muungano, alisema CHADEMA itatumia nafasi hiyo kupata mawazo ya Watanzania wanaoishi nje ambao mara nyingi hawakuwa na fursa ya kutoa mawazo yao.

“Ingawa nimekuja kwa shughuli binafsi, nitatumia nafasi hiyo kueneza harakati zetu za Movement For Change na kubwa zaidi kupata maoni na michango ya mawazo ya Watanzania wanapenda mabadiliko nchini,” alisema Lema.

Kutakuwa na mkutano wa ufunguzi  wa tawi la CHADEMA LONDON ambapo utafanyika siku ya tarehe 07/08/2012 na Mhe. Godbless Lema. Mkutao huo utafanyika THATCHED HOUSE PUB iliyopo BARKING majira ya saa 2 kamili usiku, siku hiyo ya Jumanne.

Tangu alipovuliwa ubunge na Mahakama, Lema amekuwa akiendesha mikutano mingi ya Movement For Change ambayo imekuwa na mafanikio makubwa nchini tangu harakati hizo zilipoanzishwa.

Hivi sasa CHADEMA inatarajia kuvamia mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi kupitia harakati zao za Movement For Change.

No comments:

Post a Comment