Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimehadharisha walaji wa nyama ya nguruwe
nchini, kuwa wanakabiliwa na hatari ya kupata kifafa.
Utafiti
wa kisayansi uliofanywa na SUA, umebaini kuwa baadhi ya nguruwe wana minyoo
aina ya tegu ambao nyama yao ikiliwa bila kuiva vizuri, mlaji atapata minyoo
hiyo ambayo huingia kichwani na kusababisha kifafa.
Akizungumza
na mwandishi hivi karibuni, Mhadhiri na Mtafiti wa Idara ya Sayansi ya Wanyama
na Uzalishaji ya SUA, Profesa Faustine Lekule, alisema sampuli za utafiti huo
kutoka Mbeya, zimebaini nguruwe wengi wakiwamo wanaosafirishwa katika miji
mikubwa wameathirika na minyoo hiyo.
Kwa
mujibu wa Profesa Lekule, wataalamu wa SUA wanaosimamia Mradi wa Utafiti wa
Kuboresha Ufugaji wa nguruwe kwa mkoa wa Mbeya ili kuinua pato la kaya,
unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA),
walibaini hatari hiyo baada ya kuchukua sampuli ya nyama ya nguruwe kwa ajili
ya vipimo.
“Majibu
ya sampuli ambazo wataalamu wamezichukua kutoka kwa nguruwe wa wafugaji kwenye
baadhi ya vijiji, wamebainika kukumbwa na hatari hii.
“Lazima
jitihada za makusudi zichukuliwe katika kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa tatizo
hili kati ya watafiti na Serikali,” alisema Profesa Lekule.
Alisema
maambukizi ya tegu au minyoo ya nguruwe yanatokana na tabia za baadhi ya
wafugaji kutozingatia ufugaji bora kwa kuwaacha kujitafutia chakula na maji
mitaani na kula kinyesi cha binadamu.
Kwa
mujibu wa Profesa Lekule, baadhi ya wafugaji wamekuwa wakijisaidia vichakani na
kuwaacha nguruwe kutafuta malisho katika vichaka na kula kinyesi chao, hali
inayochangia ongezeko la maambukizi ya minyoo ya tegu hao.
Baada
ya kula kinyesi minyoo humwingia mwilini na kumdhoofisha na baadaye binadamu
anapokula nyama ambayo haijaiva vizuri, minyoo hiyo humwingia na kusababisha
kifafa baada ya kuingia kichwani.
Alisema
athari za kuenea kwa maambuziki hayo inaweza kutokea katika miji mikubwa
ikiwamo Dar es Salaam kwa kuwa nguruwe wa Mbeya husafirishwa na kuuzwa maeneo
hayo.
“Hatua
hii inaweza kusababisha kusambaa kwa ugonjwa huu, hivyo ushirikiano kati ya
wafugaji, wafanyabiashara, Serikali na wataalamu wa afya katika kufikia hatua
ya kumaliza changamoto hii unahitajika,” alibainisha Profesa Lekule
No comments:
Post a Comment