Rais Jakaya Kikwete akihutubira wazee wa mkoa wa
Dar es Salaam
kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini hapa.
|
Dar es Salaam. Rais Jakaya
Kikwete amesema fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa
zinafikia Sh306 bilioni, bali ni Sh202 bilioni na zilikuwa mali ya Kampuni ya
Kufua Umeme ya IPTL.
Akijibu
swali alilojiuliza mwenyewe katika hotuba yake ya zaidi ya saa mbili kuwa:
“Fedha hizi mwenyewe nani, umma au IPTL?” Rais Kikwete alisema kumekuwapo na
maneno mengi, kila mtu anasema yake na wenzangu Wakwere tunasema ‘tunazoza
sana’ akimaanisha waongea sana.
Alisema,
“Kimsingi fedha hizi ni za IPTL, katika swali pesa za nani, Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipoulizwa na Kamati ya Bunge alisema humu
yawezekana zipo za umma pia zipo za IPTL.
“Nilipomuuliza
maana, akasema zamani walikuwa wanalipa moja kwa moja kwa Tanesco lakini baada
ya mzozo walikubaliana kwanza waziweke Benki Kuu ya Tanzania (BoT).”
Akielezea
maana ya escrow, alisema, “Ni tofauti kidogo na akaunti zetu tatu tulizozizoea,
ni akaunti maalumu ya kazi maalumu na kazi hiyo maalumu ikiisha inafungwa.
Inasimamia na wakala na wakala pia ana jukumu la kumlipa mwenye fedha wakati
ukifika.”
Ukumbi
uliojaa wazee na wasio wazee wakimsikiliza kwa umakini ulikuwa umetulia kimya
alipoanza kuzungumzia sakata hilo, akisema akaunti hiyo ilifunguliwa BoT kwa
ajili ya kuweka fedha za tozo ya uwekezaji, ili kutoa nafasi kwa pande mbili
kushughulikia tofauti zao.
“Kama
mgogoro ungetatuliwa na madai ya Tanesco yakakubaliwa na tozo kupunguzwa,
katika kiasi kilichopunguzwa kuna pesa za Tanesco ambazo lazima zirudi, bahati
mbaya miaka saba baadaye hilo (la maelewano) halikuwa limefanyika.”
“Kama
katika fedha hizo ipo kodi ya Serikali na kwa mujibu CAG kulikuwa na Kodi ya
Ongezeko la Thamani (Vat) ambayo haikulipwa, IPTL hawakuilipa na uthamini
ulikuwa zaidi ya Sh21.7 bilioni na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepeleka
madai yake kwa PAP,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza:
“CAG aliwaelekeza Tanesco kuacha kuhesabu fedha walizolipa kwenye Akaunti ya
Escrow kama yao, pesa hazikufikia sifa kuhesabika kama mali ya Tanesco.
Mahakama Kuu ya Tanzania ilifanya uamuzi katika shauri la maombi ya VIP,
kusimamisha mchakato wa ufilisi wa IPTL na Mahakama ikakubali.”
Alisema
Wizara ya Nishati na Madini ilimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (wakati
huo), Jaji Frederick Werema kuomba ushauri na aliwashauri; “walipeni, uamuzi
uko sawa na hauna matatizo na BoT waliuliza maswali hayohayo na majibu yakawa
yaleyale.”
Alisema:
“Kwa kuzingatia ushauri huo akaunti ikafungwa na pesa kukabidhiwa PAP. Mjadala
ukaendelea bungeni na kwenye mablogu. Hata Tanesco ilipewa ushauri huohuo,
uamuzi ule umetiliwa shaka na kuonekana haukuwa sahihi na umeitia hasara nchi.
Ukaibua hisia na ni kwa sababu nzuri tu kwamba si bure na iko namna kama ya
rushwa na watu kunufaika binafsi. Mara kuna watu wamekwenda benki na kubeba
pesa viroba, kwenye sandarusi, lumbesa na mengineyo.”
Alisema,
“Nilipokutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema hakukosea katika ushauri
wake na wala Mahakama haikufanya makosa na huo ndiyo ulikuwa msimamo wake na
mpaka sasa bado anaamini hivyo kuwa fedha si mali ya umma.
“Kuhusu hasara
iliyopatikana alisema hakuna hasara yoyote iliyopatikana kwa sababu fedha
ililipwa kwa mtu halali. Kwa upande wa kodi ya Serikali ambazo hazikulipwa, AG
alipoulizwa alisema hakuna kodi iliyochelewa kulipwa. Yamesemwa mengi na bado
hatujamaliza kuyasoma, rushwa ni kosa la jinai. Nilielekeza taarifa
walizozipata wazipeleke Takukuru. Nimeambiwa wanaendelea na mchakato wao.
No comments:
Post a Comment