To Chat with me click here

Saturday, December 27, 2014

KRISMASI NI ESCROW KILA KONA!



Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dk Alex Malasusa
akimbariki mtoto baada ya kumalizika kwa ibaada ya Krismasi iliyofanyika katika
Usharika wa Azania Front, Dar es Salaam.
Dar/mikoani. Kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow inayoendelea kulitingisha Taifa, jana ilitawala mahubiri ya Sikukuu ya Krismasi katika makanisa mbalimbali nchini, viongozi wa dini wakionyesha kutoridhishwa na maelezo na hatua zinazochukuliwa. Wakihutubia waumini wao, viongozi hao walitumia siku hiyo kukemea vitendo vya ufisadi, wizi na uzembe.
 
Hofu ya Escrow
Ujumbe wa Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) wa Kanisa la Anglikana, Dk Dickson Chilongani ulilenga kueleza hofu ya wananchi kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, kukosa uhakika wa huduma bora za matibabu na elimu pamoja na wimbi la viongozi waandamizi wasiokuwa waaminifu na waadilifu.

Akihubiri katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu mjini Dodoma, Askofu Chilongani alisema mbali na maisha ya ufukara na ukosefu wa huduma, sakata la Escrow na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Jumatatu vimezidi kuzidisha hofu kwa Watanzania na kuwafanya waonekane kama hawana tumaini.

Akitumia mtindo wa kuhoji, Askofu Chilongani alianza kwa kuhoji, “Kitu gani kinakutia hofu unaposherekea sikukuu hii, watu wengi tunaishi katika ulimwengu wa hofu kutokana na ufukara, ukosefu wa huduma, tunajiuliza tutawasomeshaje watoto wetu, tutapataje huduma bora za matibabu, yaani kila mmoja wetu ana hofu,” alisema.

Askofu Dk Chilongani alisema ingawa kila mtu ana hofu yake lakini sakata la akaunti ya Escrow limejenga hofu kwa mwananchi, kila mmoja akihoji na kutengeneza majibu yake jambo linalotoa picha kuwa jibu sahihi halijatolewa au kupatikana.

“Mimi siyo mwanasiasa wala mtaalamu wa masuala ya siasa lakini kuna hili sakata la Escrow ambalo juzijuzi Rais amelitolea ufafanuzi, hili nalo linazidi kuwajengea wananchi hofu, wengine wanakosoa maazimio ya Bunge, wengine wanataka Serikali itoe maamuzi yenye tija kwa umma, yaani ni hofu tu,” alisema.

Escrow ni fedha za umma
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo alisisitizia kuwa fedha zilizochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow ni mali ya umma kutokana na taarifa iliyowasilishwa na PAC bungeni.

Kauli hiyo inakuja baada ya Rais Kikwete kusema fedha hizo ni mali Kampuni ya IPTL na zilikuwa Sh202 bilioni na si Sh306 bilioni kama inavyodaiwa.
Akihubiri katika kanisa hilo jana, Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema: “Niliisikiliza kwa makini mwanzo hadi mwisho (hotuba ya Rais) leo nimeona niseme machache kwamba fedha hizo ni mali ya umma. Mimi siungani na hao wanaodai fedha hizi siyo za umma lakini kwa hali hii hakuna jinsi inabidi tumwachie Mungu maana yeye ndiye atakayeweza kutuvusha kutoka hapa tulipo,” alisema.

Padri: Viongozi wa dini waliotajwa wajipime
Paroko wa Parokia ya Mugumu, Serengeti, Padri Aloisi Magabe amesema viongozi wa dini ambao wametajwa kuhusika na fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow wanatakiwa kujipima kwa kuwa maadhimisho ya Krismasi yana maana kubwa, hivyo kuwa sehemu ya watu wanaotuhumiwa si jambo jema.
Akihutubia katika ibada ya Krismasi, Padri Magabe alisema vitendo hivyo vinazidi kushika kasi lakini hatua hazichukuliwi.

Alisema ufisadi ulijichomoza kwa nguvu kwenye Richmond, Epa na sasa Escrow, huku viongozi wa dini wakihusika, hatua ambayo ni hatari huku akisema juhudi za kuwashughulikia wahusika huchukua muda mrefu, chanzo kikiwa ni kulindana na rushwa. “Sina hofu ya kusema waziwazi matukio kama hayo, nimefuatilia magazeti jinsi wanavyojitetea, bado kuna haja ya kuwa wazi zaidi, maana nchi yetu ni ya haki na usawa, tutaupataje usawa kwa ‘skendo’ kama hizi?”

Askofu Mkude: Nina imani kubwa na JK
Askofu wa Jimbo la Morogoro, Telesphol Mkude amesema ana imani kubwa na Rais Kikwete kwa namna anavyolishughulikia suala la kuwajibisha waliotajwa katika sakata la Tegeta Escow na kuwaomba Watanzania kumpa muda wa kutosha ili aweze kuendelea kutoa uamuzi ulio sahihi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa katika ofisi ndogo ya Kanisa Kuu la Mt Patrick, Mkude alisema suala la Escrow limepita katika mchakato mrefu na baadhi ya wameanza kuchukuliwa hatua, wakiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliyefukuzwa.

“Haya mambo yanaenda na uchunguzi, sidhani kama Rais anaweza kutoa uamuzi pasipo kujiridhisha, pamoja na kuwapo kamati iliyojiridhisha na uchunguzi na kubaini uchotaji wa fedha za umma, lakini na yeye kwa nafasi yake anapaswa kujiridhisha kupitia jopo lake,” alisema Askofu Mkude.

Hofu ya Mungu na ufisadi
Hofu ya Mungu imeelezwa kuwa ndiyo pekee itakayoondoa wizi na ufisadi miongoni mwa viongozi na watendaji badala ya kutegemea sheria pekee.
Hayo yalisemwa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa wakati akihubiri katika ibada ya Krismasi katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo inafanana na ile iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Gloryland International la jijini Tanga, Manase Maganga. Malasusa alisema kutokuwapo kwa hofu ya Mungu miongoni mwa Watanzania, ndiyo sababu ya kuongezeka kwa vitendo vya ufisadi.
“Wakristo tunahitaji kusimama kwa ujasiri na kukemea mabaya yote katika jamii yetu hata kama yanafanywa na marafiki zetu kwa kuwa neno linatuagiza kufanya hivyo. Bwana anasema ‘woga ni dhambi’, hivyo tuwe makini ili kuepuka dhambi hii yenye madhara kwa watu wengi katika Taifa hili,” alisisitiza Dk Malasusa.

Vijana na siasa
Askofu Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya akiwataka vijana kujitosa kwenye siasa ili kuondoa giza nene ambalo limetawala katika nchi.
“Vijana mliopo ndani humu leo, mshughulike na siasa kwa kuingia katika chama ambacho mnaona kitachochea amani, utulivu, uvumilivu, ustahimilivu miongoni mwa wafuasi wenu lakini siyo chama kinachowakumbatia mafisadi, wabinafsi na wenye kujilimbikizia mali na kitakachosababisha chokochoko yoyote ya kutoweka kwa amani,” alisema Askofu Chengula bila kutaja jina la chama hicho.

Aliongeza: “Furaha imetoweka miongoni mwa Watanzania na furaha tunayoizungumzia hapa siyo kunywa, kucheza na kula, bali ni kuwa na amani, utulivu ndani ya mioyo yetu. Kutoweka kwa amani si lazima watu wapigane vita na damu imwagike, hapana, hata wale walioko maofisini wanaposhindwa kutimiza wajibu wao, mtu akabaki akinung’unika moyoni mwake huo ndiyo mwanzo amani wa kutoweka.

Tatizo uongozi mbovu
Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa amesema umaskini unaolikabili Taifa kwa sasa unatokana na sera mbovu za nchi pamoja na uongozi mbovu.

Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alitoa kauli hiyo katika ibada ya Krismasi huku akisisitiza kuwa Taifa la Tanzania linao utajiri mkubwa unaoweza kuwasaidia wananchi wake kuishi bila ya matatizo.

“Tanzania siyo nchi maskini, bali kinachosababisha iwe hivyo ni sera mbovu zilizopo na uongozi mbovu. Hivi kweli sisi hatuna mahali pa kuwahifadhi watu wetu? Ardhi? (waumini wakajibu tunayo), madini? (tunayo) misitu? (tunayo), mahindi? (tunayo), unawezaje kusema Taifa hili ni maskini?

“Mimi nimekuwa nikishangaa na hata ninyi mmesikia haya mabilioni ya fedha unayochukua mtu mmoja utakula hadi lini, umaskini tulionao unatokana na mtu mmoja kula chakula kinachoweza kuliwa na watu zaidi ya milioni moja, katika mazingira kama hayo ni lazima watu wengine wawe maskini,” alisema.

Uchaguzi wa mitaa
Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemuguzi aliwataka waumini wa Kikristo na watu waliopewa nafasi za utendaji kuwa wavumilivu na kuwajibika bila kuwakwaza wenzao.

Akihubiri katika ibada ya mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mt. Francisco wa Asiz, Parokia ya Ngara Mjini, juzi usiku, Askofu Niwemugizi aliwataka waumini kutimiza wajibu wao wakitanguliza subira, kutokata tamaa na kuwa makini kuzikabili changamoto za dunia.

Katika mahubiri hayo, askofu huyo ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), alisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika hivi karibuni, haukufanyika vizuri kama ilivyotarajiwa, taratibu zilivurugwa na tathmini yake inatia shaka.

Kutenda haki mwakani
Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay Dar es Salaam, Padri Stephano Kaombe aliwataka Watanzania kuacha woga wanapotekeleza majukumu yao na kuhakikisha wanafanya mambo hayo kwa kiasi na haki.

Katika mahubiri yake ya dakika 15 kwenye mkesha wa Krismasi kitaifa juzi usiku, Padri Kaombe alisema waumini wanafunzwa kuwa watenda haki na katika mwaka ujao ambao utakuwa na mambo mengi yanayohitaji kiasi na haki.

“Tunapoalikwa kwenye daftari la wapigakura tutende haki, katika kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa tutende haki, tunapofanya uchaguzi napo tutende haki na tunaweza kuyafanya hayo iwapo tutakuwa na kiasi na hatuna woga.”

Viongozi na amani
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema hatakuwa tayari kuhubiri amani inayoshinikizwa na viongozi wa Serikali wakati wao ndiyo wanaoivuruga: “CCM imekuwa na hofu ya kuondolewa madarakani, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulikuwa umejaa ujanjaujanja na hata kuwafukuza wakurugenzi ni kiini macho.”

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Anglikana, St Albano, Aidano Mbulinyingi akihubiri katika mkesha wa Krismasi aliwataka Watanzania kuwaombea viongozi wa nchi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Tusiwe na vinyongo, tukunjue mioyo yetu tuwaombee Rais, mawaziri na viongozi wengine ili Taifa liendelee kuwa na amani na utulivu,” alisema Mbulinyingi na kusisitiza kuwa bila kuwaombea hawawezi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Akizungumza kwenye ibada ya misa iliyoadhimishwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa alitoa wito kwa jamii kusherehekea sikukuu hii kwa upendo na amani bila kuwasahau watu wasiojiweza ili na wao wajisikie kuwa ni sehemu ya jamii.

No comments:

Post a Comment