RPC ADAI ANAKARIBIA
KUSTAAFU, HAWEZI KURUHUSU MIKUTANO YA CHADEMA
Marehemu Daudi Mwangosi |
KATIKA
hali inayoonyesha watawala wamedhamiria kuigeuza nchi hii dola ya kipolisi,
jana Jeshi la Polisi liliua mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha
Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyekuwa anaripoti habari za ufunguzi wa matawi
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani hapa.
Habari
za awali zilisema Mwangosi aliuawa kwa bomu lililorushwa na polisi waliotaka
kuzuia CHADEMA kufungua tawi katika Kijiji cha Nyololo.
Wakati
viongozi na wanachama walipokuwa wakiendelea na ufunguzi wa tawi la pili
kijijini hapo, ghafla walivamiwa na askari polisi, ambao walianza kuwashambulia
wananchi. Askari wapatao wanane ndio walimvamia Mwangosi.
Wakati
askari hao wakiendelea kumshambulia, ghafla lilirushwa bomu kuelekea eneo
walikokuwa, likampiga Mwangosi na kumkata vipande vipande na kutoa utumbo wake
nje.
Mwandishi
wa habari hizi alishuhudia askari hao wakimshambulia mwandishi huyo na wananchi
wengine, huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michale Kamuhanda akiwa eneo
la tukio.
Baadhi
ya akina mama walikatika miguu, wakakimbizwa hospitali kwa ajili ya kupata
matibabu. Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwapo nao walijeruhiwa kwa
kipigo, wakiwamo Hamad Yusuph, Benson Kigaila, Deogratius Sihale na wengine.
Wengine
wakiwamo mwandishi wa habari hizi aliyejeruhiwa mkono, Godfrey Mushi wa gazeti
la Nipashe na Oliver Moto wa Star TV, walikimbilia katika pori la Nyololo.
Alipopigiwa
simu Kamanda wa Polisi hakutaka kuzungumza lolote zaidi ya kusema kuwa yupo
kwenye mwendo wa kasi, hivyo hawezi kuzungumza. Akakata simu yake ghafla.
Gazeti
hili lilitaka kumuuliza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, kama
vitendo hivi vya polisi kuua wananchi ni agizo la serikali au utashi binafsi wa
polisi kuzuia wananchi kufanya kazi zilizo haki yao kikatiba, simu ilipokewa na
mtu aliyejitambulisha kama PC Seleman, akasema ofisi ya IGP haikuwa na taarifa
za tukio hilo. Ilikuwa saa 12:21 jioni.
Alisema,
“mwandishi nitakupigia baadaye IGP hadi sasa yupo katika mkutano ngoja tuanze
kufuatlia kujua maana hatuna taarifa hadi sasa.” Hadi tunakwenda mitamboni,
hakupiga simu kama alivyokuwa ameahidi.
Kabla
ya tukio hilo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, alizungumza na
waandishi wa habari alisema msisimko wa mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea
hivi sasa nchini hauwezi kusimamishwa na Serikali ya CCM, hata kama wataamua
kuwaua viongozi wote wa CHADEMA.
Dk.
Slaa alikuwa akizungumzia hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yao ya
ujenzi wa chama inayoendelea mkoani hapa. Aliahidi kuendelea, licha ya jeshi
hilo kuapa kuizuia kwa gharama yoyote.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda, alisema awali kwamba anaipenda kazi
yake, hivyo hawezi kuruhusu mikutano katika mkoa wake mpaka atakapopata maelezo
ya ziada.
Alisema:
“Ni kweli jana saa mbili tuliwapa barua ya kuruhusu shughuli zao ila hili ni
agizo na mimi ninakaribia kustaafu na kazi yangu ninaipenda, hivyo siwezi
kuruhusu maandamano kinyume na maagizo yaliyopo.”
Alisema
CHADEMA hawawezi kufanya mikutano kwa kuwa hawana jeshi wala vifaa vya
kupambana na Jeshi la Polisi, hivyo wakijaribu kutotii sheria ni lazima
washurutishwe.
Dk.
Slaa alisema alipopata taarifa za kusitisha mikutano juzi, alimpigia IGP Mwema
kutaka ufafanuzi kwani makubaliano yao ya awali yalikuwa kwamba wasitishe
mikutano kwa siku nne au tano kisha waendelee na ratiba yao.
“Katika
nia njema nilimpigia IGP kujadiliana juu ya hili. Hakupokea simu mpaka
nilipomtumia ujumbe mkali, akaniambia angepiga saa mbili usiku; pia hakufanya
hivyo. Na nilipomtafuta alisema zuio linaendelea.
“Nikamuuliza
kwa nini watu ambao ni asilimia tano ya Watanzania wote, tena wakiwa
wameelekezwa wawatafute waandikishaji wa sensa kwa namba za simu, wawe sababu
ya kuzuia shughuli zetu halali? Mwema hakuwa na jibu,” alisema Dk. Slaa.
Alisisitiza
hata baada ya kushindwa kutolea maelezo hoja hiyo, IGP alisema hilo ni agizo na
ni lazima litekelezwe kwa sababu ni amri iliyotolewa kisheria.
Dk.
Slaa alisema hata alipomuuliza ni sheria gani inayozuia hali hiyo, hakumjibu
huku akisisitiza amri yake ifuatwe.
“Sisi
hatuna bunduki, hatuna mabomu wala majeshi, lakini Serikali ya CCM na polisi
wanapaswa kutambua haya tunayoyafanya ni sawa na gharika. Kuyazuia ni vigumu,
hata kama watatuua viongozi wote, watambue mioyo ya Watanzania itaendelea
kulilia mabadiliko haya,” alisema Dk. Slaa.
Alisema
kuwa hata barua ya awali ya msajili wa vyama vya siasa haikutoa agizo la
kusimamisha shughuli za kisiasa, bali ilikuwa ikitoa rai juu ya umuhimu wa
suala hilo, jambo alilosema walilisikiliza kwa ajili ya uzalendo wao kwa nchi.
Naye
Mkuu wa Operesheni ya M4C, Benson Kigaila, alisema kuwa mikakati ya polisi
kuzuia mikutano ya CHADEMA ni mipango ya CCM.
Alisema
Agosti 4, 2012, walipokuwa wakijiandaa kufanya mikutano yao katika Mkoa wa
Morogoro, Jeshi la Polisi lilizusha sababu mbalimbali zisizo za msingi na
kwamba hata walipotumia busara ya kukubaliana nao bado waliendelea kubuni hila
chafu za kuzuia mikutano ya CHADEMA.
Wachambuzi
wa kisiasa walisema hii ni dalili kwamba serikali imezidiwa, na sasa imeamua
kuigeuza Tanzania kuwa dola ya kipolisi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Vox Media, Ansbert Ngurumo, alisema katika dola za namna hiyo,
serikali hutumia nguvu polisi kuzima na kunyamazisha harakati za kisiasa,
kijamii na kiuchumi za watu wake, kwa kisingizio cha usalama.
Katika
dola ya kipolisi, serikali huzuia mijumuiko, mikutano na maandamano ya
wananchi, ili kudhibiti wananchi kuipinga au kukosoa.
Alisisitiza:
“Katika kufanya hivyo, polisi huumiza na kuua wananchi, ikidhani kwa kufanya
hivyo inaua upinzani. Lakini historia imeonyesha kuwa mahali pote ambapo
serikali imetumia mabavu kutisha na kunyamazisha wapinzani, chama tawala
kimeanguka, ama katika sanduku la kura au kwa mapinduzi ya aina yoyote.”
Jukwaa
la Wahariri, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Neville Meena, lilisema, “tunalaani
kitendo cha polisi kutumia nguvu kiasi cha kusababisha kifo cha mwandishi.
Kitendo hiki hakikubaliki, na kinadhihirisha ukiukwaji mkubwa wa haki za
binadamu.” Hata hivyo, Meena alisema Jukwaa litatoa taarifa rasmi baadaye leo.
Mwanahabari
na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Ndimara Tegambwage, alisema: “Sasa polisi
wamewageukia waandishi wa habari. Mabavu yao haya yataishia wapi? Mwandishi
kafia vitani; mazingira ya kisiasa hapa Tanzania yanazidi kuwa mabaya. Hii sasa
ni vita; ni muhimu waandishi wa habari wapewe mbinu za kuandika habari za
kivita.” Baadaye aliandika onyo kwa polisi.
No comments:
Post a Comment