WABUNGE WAGAWANYIKA,
MBOWE AOKOA JAHAZI
Mhe. Theodosia James Mdee |
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemlipua
hadharani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akidai ni miongoni mwa viongozi wa ngazi
za juu ambao wametajwa kuhusika katika kushinikiza ugawaji huo wa ardhi.
Mdee ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati
akiwasilisha hoja binafsi inayolenga kuitaka Serikali kusitisha ugawaji wa
ardhi kwa wawekezaji kutokana na hofu wanayoipata katika mazingira yasiyo
halali ikiwamo kuwatumia vigogo serikalini.
Alisema katika baadhi ya maeneo nchini, uwekezaji
umekuwa ukifanywa kutokana na shinikizo la viongozi wa ngazi za juu serikalini
huku pia akiwataja wawekezaji waliogeuka kuwa ni matatizo.
Katika hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wa
upinzani na pomoja na wawili wa CCM, Lekule Laizer (Longido) na Dk. Faustine
Ndugulile (Kigamboni), Mdee alitaka ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nje na
ndani usitishwe hadi hapo tathimini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiasi
gani kipo mikononi mwa wawekezaji.
Hoja hiyo pia inataka tathmini ya kina ifanyike
kuweza kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi kinyemela kupitia
Serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi Na. 5 ya mwaka 1999.
Mdee alisema kwa muda mrefu kumekuwapo na uwekezaji
usiokuwa na tija kwa taifa, hivyo akawataka wabunge kuunga mkono hoja yake ili
kunusuru taifa.
Alisema kumekuwa na ubabaishaji mkubwa katika sekta
hiyo na kwamba katika mazingira mengine Serikali imekuwa kuwadi wa wawekezaji.
Mdee alisema inakadiriwa kuwa kati ya mwaka 2001
hadi 2010 kulikuwa na maombi ya wawekezaji kutaka ardhi zaidi ya hekta milioni
203 katika nchi zinazoendelea barani Afrika.
“Hii ni sawa na maombi ya hekta 55,616 kila siku
katika kipindi cha miaka 10. Halikadhalika nchini Tanzania katika miaka ya
karibuni takriban hekta milioni nne zimeripotiwa ‘kuombwa’ na wawekezaji wa nje
kwa kilimo cha mazao ya mafuta na chakula.
“Mheshimiwa Spika, ninaliomba Bunge lako tukufu,
likubaliane na hoja ya kuitaka Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi ili kuweza
kutoa fursa kama nchi kuweza kujitahmini kwa kina, wapi tulikosea ili tuweze
kujipanga upya kwa manufaa ya nchi na wananchi,” alisema.
“Sote tunajua ni kwa namna gani dhahabu, almasi na
Tanzanite zimetumika kujenga uchumi wa mabeberu! Hatuwezi kufanya makosa tena
kwenye rasilimali hii muhimu ya ardhi inayopanda thamani kwa kasi sana. Uchumi
hauwezi kuachwa uendeshwe na watu wa nje,” alisema.
Kwamba kuna haja kubwa kwa wabunge kutambua kuwa
matatizo ya ardhi yanayoikumba Rufiji, Kilombero, Bagamoyo, Kisarawe na Lugufu
yanaikumba pia Muheza, Pangani, Katavi, Meatu, Kinondoni, Njombe na Ngorogoro.
“Maeneo mengi ardhi yanayochukuliwa na wawekezaji
hao huwa hayaendelezwi kama inavyopasa na yale ambayo yanaendelezwa,
yanaendelezwa kwa kiwango kidogo sana huku wananchi wengi wakiachwa pasi na
ardhi ya kutosha kwa kilimo.
“Katika hatua nyingine, wawekezaji baada ya kupata
/kumilikishwa ardhi kwa bei ya kutupa, hawaitumii, wanasubiri ipande thamani,
kisha kuiuza kwa faida kwa wawekezaji wengine,” alisema.
Mdee alisema Kampuni ya kimarekani ya Agrisol
imepewa eneo kubwa mkoani Rukwa linalohusisha hekta 80,317 (Katumba) na 219,800
( Mishamo).
”Katika eneo hili majadiliano yanaratibiwa na
viongozi wakubwa sana serikalini. Mradi huu umejikita kwenye uendelezaji wa
mashamba makubwa na matumizi ya mbegu zenye viini tete (GMO).
Kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, alisema maeneo
makubwa ya ardhi yameuzwa kwa kampuni za AGRISOL na FELISA.
Alisema FELISA amenunua ekari 3,000 katika Wilaya
ya Uvinza Kijiji cha Basanza Kata ya Uvinza. Wawekezaji hawa wamewakuta
wakulima na wafugaji katika maeneo haya.
“Mwekezaji wa AGRISOL amepewa hekta elfu 10,000
eneo la Lugufu. Eneo hili ndio ili kuwa kambi ya wakimbizi. Eneo hili ndio
limetengwa kuwa makao makuu ya wilaya,” alisema.
Mdee alifafanua kuwa kwa kuwa rasilimali ardhi ndio
urithi pekee wa asili ya Mtanzania katika kujitafutia riziki na kuendesha
maisha yake uwekezaji katika ardhi unaofanywa na makampuni ya nje haujawasaidia
wananchi kwa maana ya fursa za ajira na upatikanaji wa chakula, analiomba Bunge
liazimie kusitiza ugawaji huo.
Baadhi ya wabunge waliochangia waliunga mkono hoja
hiyo, huku wakisema kuwa migogoro ya ardhi ni tatizo sugu nchini na kwamba
limetokana na kiwango kidogo cha ardhi kilichopimwa.
Laizer katika mchango wake alisema suala la ardhi
halina itikadi ya kichama, hivyo akawataka wabunge wenzake kuunga mkono hoja
hiyo ili kutoa fursa kwa taifa kujipanga na kufanya tahimini upya.
Naye Waziri wa Mahusiano, Steven Wassira, alisema
kuwa anakubaliana na hoja ya Mdee ya kufanya upya tathimini huku akisisitiza
kuwa wakiendelea na mfumo uliopo ambao umejaa rushwa, watabaki bila ardhi.
“Huko kwenye ngazi ya vijiji, kuna watu wanapigwa
rushwa kijiji kilichokaa kupitisha ardhi kina majina ya marehemu na sahihi zao
mimi nafanya kazi Ikulu haya mambo yapo,” alisema Wassira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na
Uwezeshaji) Dk. Mary Nagu, naye alisema kuwa hawawezi kukataa wawekezaji ambao
wanafuata taratibu huku akisisitiza kuwa wapo wasio matapeli.
Hata hivyo, kabla ya hoja ya Mdee haijafanyiwa
mabadiliko na kupita, Waziri wa Ardhi, Prof. Anna Tibaijuka, aliomba azimio
hilo libadilishwe badala ya kusitisha ugawaji ardhi ibaki hoja ya kufanya
tathimini tu ambayo itabaini wawekezaji wa raia wa kigeni waliojipatia ardhi
kinyemela. Kauli hiyo ilizua mjadala kwa wabunge wa upinzani wakikataa huku
wale wa CCM wakiunga mkono.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA)
aliungana na Mdee akisema kuwa hoja ya kusitisha haihitaji fedha ila tathimini
ndiyo inayohitaji fedha.
“Ukiruhusu tathimini wakati bado unaendelea kugawa
ardhi, utakuta umegawa yote. Halima alikuwa muungwana hakusema wawekezaji
wanyang’anywe,” alisema. Msimamo huo wa Zitto ulionekana kuungwa mkono na
wabunge wengi wa upinzani huku mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka
aliyekuwa akiungwa mkono na wenzake wa CCM alipinga hali ambayo iliendelea
kuzua mjadala.
Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu wa Bunge) William Lukuvi, alilazimika kusimama akisema serikali
inaunga mkono hoja hiyo na kwamba kama wangekuwa hawaiungi mkono wangekataa
kwani kanuni inawaruhusu.
Lukuvi aliwataka wabunge waunge mkono hoja ya
kufanya tathimini tu na kuasa kuwa endapo watasimamisha ugawaji ardhi kuna watu
watakwenda mahakamani na kuhoji kwanini wanataka kujifedhehedha.
Mbowe aokoa Jahazi
Hata hivyo baada ya kauli ya Lukuvi, bado wabunge
walionekana kutokubaliana, hali iliyomlazimu Kiongozi wa Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kusimama na kuokoa jahazi.
Mbowe aliwataka wabunge wote wakubali mapendekezo
yaliyowasilishwa na Waziri Tibaijuka na kupendekeza tathimini tu ifanyike na
kuiagiza serikali iilete bungeni Aprili kisha bunge lione mambo gani yafanyike.
No comments:
Post a Comment